KESI ya Jinai inayomkabili Mwanamziki na Rapa maarufu wa Marekani Sean John Combs maarufu kama P-Diddy inatarajiwa kusikilizwa Manhattan mjini New York Marekani, Mei 5, 2025.
Tarehe hiyo imepangwa jana Alhamis Oktoba 10, 2024 na Jaji wa Mahakama ya Wilaya ya Marekani Arun Subramanian ikiwa ni mara ya tatu kwa rapa huyo kufika mahakamani tangu kukamatwa kwake.
Mwendesha mashtaka wa serikali, Emily Johnson alimweleza hakimu kwamba serikali itahitaji wiki tatu kuwasilisha kesi yake.
Wakili wa utetezi Marc Agnifilo alisema timu ya rapa huyo itahitaji wiki kwa ajili ya kesi hiyo.
Hivi karibuni P-Diddy alikamatwa na kufikishwa mahakamani kwa mashtaka ya utumwa wa ngono na ulaghai. vilevile anashtakiwa na makumi ya watu ambao wamemshtaki kwa unyanyasaji wa kijinsia, ubakaji na unyanyasaji wa kingono.
Katika kesi ya jinai ya shirikisho, P-Diddy ameshtakiwa kwa utekaji nyara, dawa za kulevya na kulazimisha wanawake katika shughuli za ngono, wakati mwingine kwa kutumia bunduki au kuwatishia kwa vurugu.
Hata hivyo P-Diddy alikana tuhuma hizo na mara kwa mara mawakili wa rapa huyo wameshikilia msimamo kuwa hana hatia, wakiziita tuhuma dhidi yake kuwa za uwongo na kashfa.
Kesi hiyo ilipoahirishwa siku ya jana baadhi ya wafuasi wa P-Diddy pamoja na familia yake walibakia katika mlangoni wa Mahakama hiyo wakisubiri kumwona rapa huyo alipokuwa akisindikizwa kurejeshwa rumande.
P-Diddy alionekana akiwa amevalia sare ya gereza ambako hata hivyo Hakimu alijadili kuweka zuio dhidi ya mawakili au waendesha mashtaka kujadili kesi hiyo hadharani au na vyombo vya habari.
MITAZAMO KINZANI.
Katika mitandao ya kijamii baadhi ya watu wamekuwa wakijadili suala hilo kwa mitazamo tofauti huku sehemu kubwa wakimtuhumu kuhusika na vitendo hivyo.
Hata hivyo kundi la pili linalojadili suala hilo linalihusisha na masuala ya ubaguzi nchini humo likienda mbali na kufananisha na kesi ya msanii maarufu R.Kelly na kuwa utajiri na umaarufu wake ndilo tatizo.
"Watu wote walikuwa wakishiriki 'party' za P-Diddy ni watu wazi na Marekani ni wahumini na watetezi na vitu anvyohusianishwa navyo sasa inakuwaje kwa Diddy hata kama kafanya liwe kosa," alihoji mmoja wa wachangiaji katika mitandao ya kijamii.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED