Producer wa Ditto atoa ushahidi Mahakama Kuu

By Mwandishi Wetu , Nipashe
Published at 05:00 PM Mar 22 2024
Lameck Ditto (mwenye kofia) akiingia kwenye moja ya chemba za Mahakama Kuu, kanda ya Dar es Salaam kusikiliza kesi yake ya madai dhidi ya DSTV.
PICHA: MWANANCHI
Lameck Ditto (mwenye kofia) akiingia kwenye moja ya chemba za Mahakama Kuu, kanda ya Dar es Salaam kusikiliza kesi yake ya madai dhidi ya DSTV.

MTAYARISHAJI wa muziki, Emmanuel Maungu, aliyetengeneza audio ya kibao kiitwacho Nchi Yangu cha msanii, Dotto Bernard maarufu Ditto, ametoa ushahidi wake akieleza Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam namna alivyotengeneza wimbo huo mwaka 2017.

Maungu ni shahidi wa pili kati ya watano katika kesi ya Ditto dhidi ya MultiChoice Tanzania Limited anayedai kampuni hiyo imetumia kibao chake kwenye matangazo yao ya biashara kipindi cha Kampeni ya fainali za Kombe la Afrika (AFCON 2019) bila ridhaa yake.

Ditto alifungua kesi akiiomba mahakama iamuru MultChoice Tanzania imlipe fidia ya Sh. bilioni sita kwa kutumia wimbo wake katika matangazo yao ya biashara bila ridhaa yake.

Pia ameiomba mahakama iamuru alipwe Sh. milioni 200 kutokana na madhara ya jumla, pia alipwe riba ya asilimia 25 tangu siku alipofungua shauri hilo.

Jana, kesi hiyo iliendelea kusikilizwa kwa mashahidi wa Ditto mbele ya jaji, Salma Maghimbi.

Producer wa Wimbo huo, Emmanuel Maungu aliieleza Mahakama kwamba aliutengeza wimbo huo mwaka 2017 na alipigiwa simu na Ditto mwaka 2019 kumuuliza endapo yeye (Maungu) ndiye alitoa idhini kwa DSTV kuutumia kwenye matangazo yao.

Akitoa ushahidi wake wa maandishi, alidai alimwambia Ditto sio yeye ndipo akamtumia links kuona walivyoutumia katika matangazo hayo.

Alisema, alianza kutengeneza wimbo wa Nchi Yangu uliombwa na Ditto pekee, kisha akafanya remix ya wimbo huo huo wa Ditto na kushirikishwa wasanii wengine baadhi baada ya Ditto kuombwa ifanyike Remix kwa ajili ya Tamasha la Urithi.

Baada ya kutoa ushahidi wake, Wakili wa DSTV, Thomas Mathias alimuuliza shahidi huyo.

Wakili: Nikisema wewe ndiye uliyeingiza biti kwenye wimbo wa Nchi Yangu niko sahihi?

Shahidi:Niliingiza sauti

Wakili:Unafahamu masuala ya haki miliki?

Shahidi:Nazijua za kwangu kama producer

Wakili:Tutajie haki kadhaa kama producer

Shahidi:Ni kuwa na umiliki sehemu ya muziki nilioingiza

Wakili:Unataka kuiambia Mahakama katika wimbo wa Nchi Yangu una haki?

Shahidi:Hayo ni makubaliano yangu na Ditto.

Wakili mwingine wa DSTV, alimuuliza shahidi

Wakili:Nitakuwa niko sahihi kwamba ulisema wimbo huu una version mbili?

Shahidi:Ndio

Wakili:Ni upi ulitumika na Dstv?

Shahidi:Nchi yangu version ya pili ulitumika

Wakili:Hiyo iliimbwa na nani?

Shahidi:Uliimbwa na Ditto kwa kushirikiana na wasanii wengine.

Kesi hiyo itaendelea tena leo katika mahakama hiyo.