FAINALI ya shindano la kusaka vipaji vya muziki Tanzania, Bongo Star Search (BSS), msimu wa 14, inatarajiwa kufanyika Januari 27, mwaka huu katika Ukumbi wa Were House jijini Dar es Salaam.
Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam, Mkurugenzi Mtendaji wa Benchmark 360, Ritha Paulsen, maarufu Madam Ritha, alisema mwaka huu BSS imekuwa ya tofauti kwa sababu wanawake ni wengi kuliko wanaume na wana vipaji.
"Washiriki sita wameingia fainali ya kusaka vipaji nchini BSS, mashabiki jitokezeni kushuhudia. Kipaji chako mtaji wako, washindi watapata zawadi.
"Mshindi wa kwanza kuondoka na Sh. milioni 20, kiwanja mita za mraba 500, mshindi wa pili atapa kiasi cha Sh. milioni tatu na mshindi wa tatu atapata kiasi cha Sh. milioni moja wengi kupata kifuta jasho," alisema.
Alisema kwa mwaka huu hawakwenda Dodoma, lakini walikwenda Kigoma, Arusha, Mwanza, Mbeya na kwingine na kwamba kulikuwa na washiriki wengi wakike wanaoimba na kufanya vizuri zaidi na kufika fainali hivyo ni msimu mzuri zaidi.
"Vijana 5,700 walishiriki katika shindano la BSS na hatimaye kubaki washiriki sita watakao chuana Januari 27 na mshindi kupatikana."
Ofisa Sanaa kutoka Baraza la Sanaa la Taifa (BASATA), William Makame, alisema sanaa wanayofanya BSS ya kutoa furaha kwa vijana ni kitu kikubwa na chakupongezwa kwani wanawasaidia vijana kufikia ndoto zao.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED