MANENO yanayodaiwa kutokuwa na staha kulingana na mila na desturi za Kizanzibari, yameelezwa kumponza msanii wa muziki wa kizazi kipya, Zuhura Othman (Zuchu), kufungiwa kufanya shughuli za muziki visiwani humo kwa miezi sita na kutozwa faini ya Sh. milioni moja.
Zuchu nampenda lakini akiwa kwenye ‘show’ hajiheshimu na kazi yake. Yeye ni michambo tu,” alisema mmoja wa wachangiaji aliyejitambulisha kwa jina la Sweetlylizzy.
Akitumbuiza katika tamasha lake alilofanya Februari 24, mwaka huu, Kendwa Mkoa wa Kaskazini Unguja, lililobeba jina la Usiku wa Fullmoon, Zuchu anadaiwa kutumia maneno yasiyo na staha yakiwamo matamshi na kuonyesha ishara mbaya kinyume cha maadili.
Akitoa taarifa ya kumfungia msanii huyo jana, Katibu Mtendaji wa Baraza la Sanaa, Sensa, filamu na Utamaduni Zanzibar, Omar Abdalla Adam, alisema imekuwa tabia ya msanii huyo kuimba nyimbo zisizo na maadili, kutofuata misingi na hazina njema kwa jamii ya Wazanzibari.
Pia alisema licha ya msanii huyo kutokuwa na usajili Zanzibar, amekuwa akiendesha shughuli zake za sanaa visiwani humo bila kupata kibali.
“Baraza lina wajibu wa kusimamia mila, silka, desturi na utamaduni wa Mzanzibari. Kwa hiyo linatamka rasmi kumfungia Zuhura kufanya shughuli yoyote ya sanaa kwa Zanzibar kwa kipindi cha miezi sita kuanzia Machi 5, mwaka huu,” alisema Adam.
Mbali na adhabu hiyo, pia msanii huyo ametakiwa kulipa faini ya Sh. milioni moja kwa baraza hilo pamoja na kuandika barua ya kuomba radhi na kuthibitisha kwamba hatafanya kosa hilo ndani ya kipindi alichofungiwa.
Katika barua yake ya kuomba radhi, Zuchu alisema hakuwa na nia mbaya ya kuleta mmonyoko wa maadili wala taharuki kwa yeyote bali alikuwa kwa lengo la kutoa burudani njema na kufurahisha mashabiki wake wote.
“Ninatoa ahadi leo kufanya kazi na timu yangu ili kuhakikisha matukio kama hayo hayatokei tena kwenye matamasha yajayo. Nawaomba radhi tena kwa jamii na Baraza la Sanaa ambao ndio walezi wangu,” alisema Zuchu.
Zuchu alitoa kauli hiyo jana saa chache baada ya baraza hilo kutangaza kumfungia kufanya shughuli zote za sanaa visiwani Zanzibar sambamba na kupiga marufuku nyimbo zake kupigwa katika redio na televisheni za visiwani humo kwa muda aliofungiwa.
Baada ya msanii huyo kuomba radhi na barua yake kuwekwa mtandaoni, baadhi ya watu walitoa maoni tofauti.
“Zuchu nampenda lakini akiwa kwenye ‘show’ hajiheshimu na kazi yake. Yeye ni michambo tu,” alisema mmoja wa wachangiaji aliyejitambulisha kwa jina la Sweetlylizzy.
Yef2007 aliandika: “Lazima uwe na uchaguzi wa maneno ya kutumia. Binafsi nilisikitika sana kwenye hicho anachosema kibwagizo(anakitaja) hongera kwa kutambua kosa na kuomba radhi.”
Naye Sylus Shany aliandika: “Hiyo radhi ni ya kinafiki kwani hukujua kama(anataja neno), ilikuwa lugha chafu, ulifanya kusudi. Tulishazoea wewe na huyo(anamtaja).
“Utukane kesho uje uombe radhi...mnafanya wazazi watukanwe kila siku, mama yako kaimba mziki miaka sijui 40 hatujawahi hata kusikia akitamka(anataja neno), acheni kujitoa ufahamu,” aliandika hivyo Digala.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED