Chama cha Wafanyakazi wa Serikali na Afya Tanzania (TUGHE) kimesisitiza kuwa ili kuleta tija katika maeneo ya kazi ni lazima wafanyakazi watimize wajibu wao ipasavyo huku waajiri nao wakiwajibika kutimiza haki za watumishi wao kulingana na makubaliano katika mikataba yao.
Akizungumza na Waandishi wa Habari mara baada ya ufunguzi wa Mkutano wa Baraza Kuu TUGHE kwa mwaka 2024, uliofanyika jijini Mwenyekiti wa TUGHE Taifa, Joel Kaminyoge ameeleza kuwa endapo kila upande yaani mwajiri na mfanyakazi utatimiza wajibu wake itasaidia kufanya sehemu za kazi kuwa salama na kupelekea kukua kwa uzalishaji na hatimaye kufikia malengo yanayokusudiwa.
Naye Katibu Mkuu wa TUGHE, Hery Mkunda ameeleza kuwa Chama kinapoadhimisha Miaka 30 tangu kuanzishwa kwake, kinajivunia kuwa mstari wa mbele katika kusikiliza kero za wafanyakazi hususani wanachama wao na kuzitafutia ufumbuzi kwa kushirikiana na Serikali pamoja na wadau.
Katika hatua nyingine, TUGHE imesaini mkataba wa ujenzi wa jengo la kitega uchumi na kumkabidhi mkandarasi ambapo ujenzi wake utaanza hivi karibuni.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED