CHAMA cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) kimelalamika kunyimwa nafasi ya kutoa salamu za pole katika hafla ya kuuaga mwili wa Waziri Mkuu mstaafu, Edward Lowassa.
Katibu Mkuu wa chama hicho, John Mnyika, ameelekeza malalamiko kwa Itifaki ya Kamati ya Maandalizi kuwa haikuwapa nafasi ya kufanya hivyo kama vyama vingine vilivyopewa.
Akizungumza jana katika viwanja vya Karemjee, ambako hafla ya kuuaga mwili wa Lowassa ilifanyika, alisema haikuwa sawa kutopewa nafasi ya kuzungumza kwa kuwa Lowassa alitumikia chama hicho kwa kipindi kìrefu na alikuwa mwanaharakati wa kutaka mabadiliko mengi akiwa katika chama hicho.
Mnyika alisema Lowassa alihamia katika chama hicho mwaka 2015 akitokea Chama Cha Mapinduzi (CCM) baada ya kukatwa kwenye kinyang’anyiro cha urais na kuteuliwa kugombea urais kupitia Umoja wa Katiba ya Wananchi (UKAWA).
"Imenishangaza kwa kunyimwa nafasi hiyo kwani mimi kama katibu mkuu niko hapa ningeweza kukisemea chama na wanachama wa CHADEMA kwa ujumla kwa mazuri yake aliyoyafanya akiwa na chama chetu," alisema Mnyika.
Alisema pamoja na mambo mengine kiongozi huyo alikuwa muumini wa mabadiliko ya mfumo wa utawala kwa kupitia katiba mpya, hivyo namna nzuri ya kumuenzi ni kufanya marekebisho ya katiba ili kuwe na uchaguzi huru na wa haki.
"Ndiyo maana alipopeperusha bendera ya CHADEMA. Kipaumbele namba moja ni kuwa na katiba mpya, hivyo amefariki (dunia) bado katiba mpya haijapatikana, hivyo ni muhimu mchakato huo uendelee," alisema Mnyika.
Aidha, alisema Lowassa aliingia katika chama akiwa na sera nzuri ambazo alizisemea kwa lugha yake ikiwamo uchumi imara na shirikishi unaogusa maisha ya watu kwa kuleta unafuu.
VYAMA VYA SIASA
Mwenyekiti wa Baraza la Vyama vya Siasa Tanzania, Juma Khatibu, aliwasihi wananchi wawe wastahimilivu katika kipindi hiki kigumu kilicholikumba Tanzania.
Naibu Katibu Mkuu wa CCM, Anamringi Macha, alisema kila mmoja kwa nafasi yake arejee mema ya kiongozi huyo ili kulijenga taifa.
Alisema chama hicho kimejifunza mengi kutoka kwake na watayarejea kwa ajili ya kuijenga nchi, chama na siasa ya nchi.
MAHAKAMA YATOA NENO
Akizungumza kwa niaba ya Jaji Mkuu, Prof. Ibrahim Juma, Jaji Jacob Mwambwgele, alisema Mahakama ya Tanzania inamfahamu Lowassa kama mwanasiasa mwenye moyo wa uvumilivu, mwenye ngozi ngumu ya kisiasa.
Jaji Mwambegele alisema kiongozi huyo alikuwa akiuishi msemo wa kuwa ‘ukimya ni dhahabu’ na mahakama hiyo imelichukua hilo kama funzo katika maisha hao ya duniani.
Waziri wa Fedha, Mwigulu Nchemba alisema kiongozi huyo alikuwa mwenye kiu ya kupenda matokeo zaidi kuliko maneno na pia si mchoyo wa mawazo.
"Nimepoteza rafiki, nimepoteza kiongozi nakumbuka alinijenga katika mambo mengi hasa bungeni alikuwa ananielekeza mambo mengi na kunipa mwongozo," alisema Nchemba.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED