Wanafunzi wote wanahitaji kula

By Sabato Kasika , Nipashe
Published at 02:04 PM Mar 13 2024
Wanafunzi wakiwa katika foleni ya chakula.
PICHA: MTANDAO
Wanafunzi wakiwa katika foleni ya chakula.

MIKOA ya Njombe, Kilimanjaro, Arusha, Pwani, Iringa na Manyara, imesifika kwa kutoa chakula shuleni, kuchochea ubora na ufaulu kwa wanafunzi.

Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, (anayeshughulikia elimu) Dk.Franklin Rwezimula, ndiye anayeitaja mikoa hiyo jijini Dodoma hivi karibuni kwenye maadhimisho ya Siku ya Afrika ya Chakula Shuleni.

 Kwa mujibu wa Naibu Waziri huyo, huduma ya chakula shuleni katika mikoa hiyo inapatikana kwa zaidi ya asilimia 80, na kwamba hatua hiyo inapunguza utoro kwa wanafunzi.

 Mbinu zilizotumiwa na mikoa hiyo hadi huduma ya chakula shuleni kupatikana kwa zaidi ya asilimia 80 ni ya kuigwa na mikoa mingine, ili hatimaye wanafunzi wa shule zote wapate mlo.

Inaelezwa kuwa chakula shuleni kinachochea ubora na ufaulu kwa wanafunzi, hivyo ni vyema mikoa mingine ambayo bado yako nyuma ikaangaalia uwezekano wa kuwepo kwa chakula.

 Kukosekana kwa chakula shuleni kunachangia utoro wa rejareja kwa wanafunzi na wengine kukatisha masomo, hivyo, serikali imeanzisha utaratibu wa kuishirikisha jamii kuchangia upatikanaji wa chakula.

 Tanzania bara ina mikoa zaidi ya 20, kwa nini ni mikoa sita tu ambayo chakula shuleni kipatikana kwa zaidi ya asilimia 80? Mikoa mingine ina changamoto gani hadi ishindwe kutoa huduma hiyo?

 Si vibaya mikoa ambayo bado iko nyuma, ikaanza kazi ya kuhamasisha jamii, wadau wa elimu wakiwamo wazazi ili kuweka mikakati ya kutekeleza afua za lishe shuleni, kwa kuzingatia ushauri wa wataalam wa afya, wa saikolojia kuwa yapo madhara makubwa ya kukosekana kwa chakula kuwa ni njaa, usikivu, utoro wa rejereja na kukatisha masomo.

 Ninaamini kuwa serikali imefanya uwekezaji mkubwa kwenye sekta ya elimu, lakini pia upatikanaji wa matokeo mazuri ya elimu hutegemea afya bora kwa wanafunzi, hivyo chakula shuleni ni muhimu.

 Ingekuwa ni vyema kwa kila mdau wa elimu kutambua ushauri wa wataalam wa afya kuwa chakula shuleni ni muhimu, kwa kuwa kinachochea ubora wa elimu na ufaulu kwa wanafunzi.

 Kwa kuwa jitihada za kuwasaidia wanafunzi kusoma vizuri na kupata matokeo mazuri ni kuwapo kwa chakula shuleni, basi jambo hilo lipewe uzito mkubwa ili kusiwe na shule ambayo haina huduma hiyo.

 Ikumbukwe kuwa mwaka 2021.Wizara ya Elimu ilizindua Mwongozo wa Kitaifa wa Utoaji wa Huduma ya Chakula na Lishe kwa Wanafunzi wa Elimu msingi ili kuweka utaratibu wa kitaifa ambao utawezesha wanafunzi kula chakula.

Kimsingui, upatikanaji wa chakula shuleni ni suala mtambuka ambalo linahitaji ushiriki wadau wote wa elimu hasa wazazi na walezi, lakini mtindo wa baadhi yao kujiweka kando, unasababisha baadhi ya wanafunzi kukosa huduma hiyo muhimu kwa wanafunzi.
 
 Wazazi na walezi wasiwe wazito kuchangia chakula na kusababisha watoto wao kushinda njaa, wakisingizia kuwa serikali ilishatangaza elimu bure, msimamo ambao ni wazi unawaathiri watoto wao kimasomo.
 
 Serikali inafanya sehemu yake katika huduma hiyo, wazazi na walezi nao wana sehemu yao katika kuhuduma shule hasa kwa kuzingatia kwamba shule hizo ni za umma, halafu wenyewe ndio umma.
 
 Ninadhani si sahihi mzazi au mlezi kugoma kupeleka shuleni kilo moja ya maharage na unga kwa ajili ya mtoto wake kwa kisingizio kuwa serikali inatoa elimu bure. Kama ndivyo, mchango wa watu wa aina hii katika shule zao ni upi? Ni vyema kila mmoja afanye sehemu yake.