Simu ni muhimu shuleni ikitumika vizuri

By Sabato Kasika , Nipashe
Published at 07:51 AM Jul 02 2024
Mtumiaji wa simu ya mkononi.
Picha: Mtandao
Mtumiaji wa simu ya mkononi.

MOJA ya masharti katika fomu za wanafunzi wanaojiunga na kidato cha kwanza kwenye baadhi ya sekondari, ni kuonywa kuwa hawaruhusiwi kuwa na simu shuleni na pia mtumishi au mwalimu ni marufuku kutunza simu za wanafunzi.

Suala hilo la baadhi ya shule  kukataza  simu shuleni, limeibua  mjadala  katika jamii, wakiwamo watu wanaoona si vibaya kuwa na simu na wengine wakiunga mkono katazo hilo.
 Watu wasiishi kwa mazoea  nadhani ipo haja ya kulegeza masharti ambayo yanawabana  wanafunzi kuhusu matumizi ya simu wawapo shuleni, hasa kutokana na kwamba katika karne ya sayansi na teknolojia, matumizi ya simu yamekuwa ni muhimu hata kwa wanafunzi.
 
 Kwa kutumia mfumo wa Teknolojia , Habari na Mawasiliano (TEHAMA), unaweza kuwasaidia  wanafunzi kupata vitabu vya kujifunzia unaofahamika kama Maktaba Mtandao kutoka Taasisi ya Elimu Tanzania.
 
 Ili mwanafunzi aweze kuupata na kuutumia, ni lazima atumie kifaa kama simu , kompyuta au kishikwambi, hivyo ni wazi kwamba kuna umuhimu wa kulegeza masharti ili wanafunzi watumie simu shuleni.
 
 Jambo la msingi ni kuweka utaratibu wa kuhakikisha hawavitumii kwa mambo mengine yasiyoendana na elimu. Simu zitunzwe sehemu moja ili mwanafunzi anapohitaji kuitumia kupakua vitabu, apewe kisha arudishe.
 
 Hapa maana yake ni kwamba mwanafunzi asiende na simu shuleni kwa kificho, bali kila mwanafunzi ajulikane na kuelekezwa jinsi ya kuzitumia, ili waweze kufaidika na TEHAMA.
 
 Ninaamini kwamba kwa kuzingatia matumizi ya sahihi ya simu janja, kuna faida nyingi kuliko madhara hasa kipindi hiki ya sayansi na teknolojia ambacho kila kitu kiko mtandaoni.
 
 Kimsingi, shuleni ni mahali ambako kuna sheria, kanuni na taratibu wake, hivyo kila jambo likisimamiwa ipasavyo kwenye matumizi sahihi ya simu janja wanafunzi wanaweza kufanya vizuri katika masomo.
 
 Ninadhani si vibaya kama simu zikiwa maslumu kwa ajili ya0 wanafunzi kwa kuwekwa program zinazohusiana na masomo yao tu badala ya kuangalia programu nyingine zinazoweza kuwaweka katika matatizo.
 
 Ninatambua kuna sababu mbalimbali zinazochangia kuzuia shuleni, ikiwamo kuhofia wanafunzi kufeli kutokana na kuendekeza simu zaidi kuliko masomo. Hilo ni kweli hasa simu zikitumiwa vibaya.
 
 Lakini ikumbukwe kuwa kwa sasa simu sio chombo tu cha kuzungumza bali pia ni chenye zana mbalimbali muhimu katika maisha ye kila siku, hivyo ni vyema tukaendana kulingana na taknolojia ilivyo.
 
 Kama yapo ambayo tumerithi kutoka kwa wakoloni na tunaamini yamepitwa na wakati, basi hatuna budi kuyaacha, ili wanafunzi waweze kuonyesha ujuzi wao kupitia TEHAMA, lakini kwa kuwasimamia.
 
 Suala la matumizi mazuri au mabaya ya simu, yako pande zote kwa watoto (wanafunzi) na hata watu wazima, hivyo jambo la msingi kwa wanafunzi na kuwafundisha matumizi sahihi na kuwasimamia.
 
 Ninaamini kuna haja ya kuruhusu matumizi ya TEHAMA kwa faida ya wanafunzi, walimu, shule na jamii husika kwa ujumla. Jambo la kuzingagtia ni usimamizi. Kila mwanafunzi mwenye simu ajulikane na aitumie kwa wakati maalum awapo shuleni. 
 
 Ukiwapo usimamizi, ni wazi mwanafunzi hatatumia simu kwa mambo binafasi, badala yake ataitumia kwa ajili ya mambo ya shule tu. Wale watakaoshindwa kufuata utaratibu, basi wasiruhusiwe kuwa nazo.
 
 Kwa sasa somo la TEHAMA yanafundishwa shuleni, hivyo wanafunzi wataendelea kuzuiwa kuwa na simu shuleni, wataendeleo kubaki nyuma, hasa kutokana na ukweli kwamba sio kila shule ina komyuta za kutosha kufundishia somo hilo.