Jamii jiepusheni matumizi ya dawa bila ushauri

By Mhariri Mtendaji , Nipashe
Published at 11:22 AM Jun 27 2024
Dawa za Hospitali.
Picha: Maktaba
Dawa za Hospitali.

HIVI karibuni wataalamu wa afya wameihadharisha jamii, kuhusu matumizi holela ya dawa za maumivu, ambayo mara nyingi watu huamua kujinunulia katika maduka ya dawa

Dawa hizo ni maalumu kwa ajili ya kutuliza maumivu ya muda au sugu, kama vile wanaougua selimundu na waliotoka kufanyiwa upasuaji.

Mtaalamu kutoka Hospitali ya Taifa ya Afya ya Akili Mirembe (MNMHH), amebainisha dawa kadhaa ambazo baadhi ya vijana hususan wanafunzi wa shule za msingi na sekondari, huzitumia bila ushauri wa kitabibu.

Vijana hao, hufika katika maduka yanayotoa huduma za dawa za binadamu, wakinunua lengo lao ni kustarehe.  Matumizi hayo hugeuka kuwa uraibu na kuwaingiza vijana katika kundi la matumizi ya dawa za kulevya.

Dawa za kulevya ni kemikali ambazo huingia katika ubongo na kumwathiri mtumiaji, kusababisha fikra, hisia, kuleta matendo tofauti kwa matarajio ya umma.

Wapo ambao huzitumia dawa za kulevya kwa njia ya kula/kunywa, kuvuta au kujidunga. Hatua ambayo ni hatari kiafya, hasa kwa kundi la vijana ambalo analitaja ni kuanzia umri wa shule hadi miaka 40.

Tabia ya kununua dawa za kutuliza maumivu kiholela na matumizi ya dawa hizo kwa zaidi ya siku 14 huwa ni uraibu na inaweza kumfanya mtumiaji kutaka kuitumia kila siku.

Uchunguzi wa hospitali hiyo umebainika zaidi ya vijana 600 wanawahudumiwa ili kuwaponya na athari za uraibu ikiwamo matumizi ya dawa hizo hata dawa za kulevya kama bangi.

Asilimia 80 hadi 90 ya wenye uraibu wanaotibiwa hospitalini hapo umri wao ni kati ya miaka 16 hadi 40.

Wanapohojiwa ama kufanyiwa tathmini kabla ya kuanza tiba wanabainika kwa asilimia 50 wameanza kutumia dawa za kulevya wakiwa shule ya msingi, sekondari na wachache wakiwa kazini.

Miongoni mwa dawa za kulevya ambazo wanabainika huzitumia ni pamoja na hizo za kutuliza maumivu, ambazo mtaalamu anafafanua kwamba utumiaji holela wa dawa za kutibu maumivu ni kinyume cha malengo na kugeuka kuwa uraibu.

Mirungi, cocaine nazo imebainika vijana hao hutumia.

“Hospitalini kuna dawa ambazo mtu anaandikiwa kutokana na changamoto ya maumivu kwa muda mrefu. Matumizi ya muda mrefu kama wiki mbili wa dawa kama valium, tramadol ni uraibu.

Zipo dawa ambazo zimeruhusiwa kutumika kwa utaratibu, kinyume chake kinaweza kuleta uraibu.

Kiwango hicho cha vijana ambao wanapatiwa tiba hospitalini hapo wapatao 600 ni idadi kubwa ambayo, inategemewa na taifa katika uzalishaji hasa ambao wana umri wa zaidi ya miaka 18.

Kadhalika vijana walio na umri wa kuwa suleni hadi ngazi ya vyuo, walijiingiza katika uraibu huo, hulisababishia taifa hasara kwa sababu muda wao mwingi huutumia kutumia dawa za kulevya badala ya kukuza uchumi.

Kukua kwa teknolojia, tangu miaka ya 2000 hadi sasa kunatajwa sababu kwa baadhi vijana kutumia ukuaji huo tofauti na malengo, kama vile kuwa chanzo cha ubunifu, fursa na ajira kwa kundi la vijana ambalo nchini ni zaidi ya asilimia 60.

Ni vyema vijana ambao baadhi huiga tamaduni zilizo kinyume na maadili, imani kupitia teknolojia tofauti, wabadili dhana hizo kwa kuacha kujikita katika starehe za muda mfupi ambazo ni hatari kwao na taifa.