Aina hii ya uzembe wetu katika taka, tujue tunakaribisha maradhi wenyewe

By Tuntule Swebe , Nipashe
Published at 07:44 AM Jun 20 2024
Taka.
Picha:Mtandao
Taka.

NI jambo la kawaida sana kwa jamii inayotuzunguka kutupa taka sehemu ambazo wala sio sahihi mathalani kwenye mitaro inayotumika kusafirisha maji. Niseme, jambo hili haliko sawa.

Watu wengi wanapokuwa barabarani au majumbani mwao, imekuwa ni kawaida yao kutupa taka pasikofaa, wakikwepa gharama za kulipia taka, hivyo, inawalazimu watupe kwenye mitaro jirani. 

Kuna baadhi yao, wanaona shida kutembea na taka  aliyoizalisha, kama baada ya kunywa soda, kula matunda, kunywa maji. Hivyo, anaona ni bora atupe kwenye mtaro, wakisahau kuwa wakati mwingine, taka zina mbadala wa kumnufaisha, ikitumika kwa busara.

Kwa taka zinazotupwa kwenye mitaro majumbani, watu wanaokaa karibu na wanakuwa hatarini na maradhi kama ya tumbo na kipindupindu.

Uchafu unaotupwa, unachangia maji kukwama na ndio unakuwa mwanzo wa simulizi za mlipuko wa maradhi.

Mbu wakienea, tayari wanajamii mnakuwa jirani na maradhi kama matende na malaria, hivyo watu wanaoishi jirani, wanabaki kuishi kwa hofu na mtu akigua, shughuli za maendeleo husita au kusuasua, kila kona na hata kuna baadhi wanaweza kupoteza uhai.

Tusisahau pia, kunapokuwapo mvua kubwa, kunaweza kuwapo mafuriko. Je, tumewahi kujiuliza na sisi wenyewe ni wapi tunapokosea? 

Kuna baadhi ya sehemu zinazotiririsha maji zinahitaji marekebisho. Kama, wananchi tutaendekeza utupaji taka mitaroni, inachangia maji yasiende na mvua inapokuwa kubwa, maji hujaa mitaroni au  ikafurika, ikihamia kwenye makazi ya watu.

Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam, sasa inatambua ongezeko la aina tofauti za taka ngumu, zikiwamo taka za majumbani, viwandani na taka za hospitalini zinatupwa maeneo mbalimbali, hivyo kuweza kusababisha uchafuzi wa mazingira (hewa, maji na ardhi).

Dar es Salaam linakadiriwa kuzalisha zaidi ya tani 4,600 za taka kwa siku. Kati ya hizo, asilimia 45 hadi 50 tu zinazopokelewa katika dampo, sawa na tani 2,070 hadi 2,300, kwenye maeneo ya wazi, mitaro ya maji, barabara na makazi. 

Usafi wa Dar es Salaam, hususani udhibiti taka ngumu, ni tatizo la muda mrefu na lenye changamoto nyingi. 

Tabia iliyozoeleka miongoni mwa jamii kutupa ovyo taka katika maeneo yasiyostahili, imechangia uchafu wa Dar es Salaam.

Kuzagaa taka kunaweza kuwa kichocheo cha milipuko ya magonjwa, kama vile kipindupindu ya kuhara na kutapika. 

Uchafu wa Dar es Salaam, unachangiwa pia na elimu ndogo kuhusu usafi wa mazingira na kutotii sheria zilizopo kwa upande wa wananchi na usimamizi hafifu wa sheria za usafi wa mazingira.

Ili kupunguza uchafuzi wa mazingira, Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam, imeandaa sera ya kurejeleza taka ngumu, itakayokuwa msingi kwa taasisi za nchini kutambua na kurasimisha sekta ya urejelezaji taka, ambao awali iliendeshwa na taasisi binafsi, pia vikundi visivyokuwa rasmi.

Katika kuhakikisha hilo linafanyika, Halmashauri ya Jiji la Dar Es Salaam inalenga kufanya mambo kadhaa: 

Kwanza, inabuni miradi ndani ya jiji itakayohusisha wadau kurejeleza taka, pamoja na kupatikana masoko ya uhakika kwa bidhaa zitakazozalishwa kupitia uchakataji huo.

Ingependeza, jamii ikahamasishwa umuhimu wa kurejeleza taka, ikishirikiana na halmashauri za manispaa kuhakikisha utenganishaji taka ufanyike kuanzia ngazi za uzalishaji (sorting at source).

Lingine linatajwa ni kuwatambua na kuwaunganisha wadau wanaojihusisha na teknolojia za urejelezaji taka ndani ya Dar es Salaam, kukitengwa maeneo.  

Hapo ndani yake kuna suala la kuwezesha wananchi wa maisha ya chini, wakiwamo vijana na wanawake, wakashiriki katika ubunifu na utumiaji teknolojia za urejelezaji taka, hatimaye kufikia suala la usafi.

Urejelezaji huo wa taka una faida nyingi kama vile; kuongeza thamani ya taka na kipato katika jamii, kupunguza marundo ya taka katika mitaa na maeneo ya jamii, kupunguza gharama za uendeshaji wa dampo, kupunguza gharama za udhibiti taka. 

Hivyo, kama wanajamii kwa pamoja tukemee utupaji taka kwenye mitaro, kwani mvua ikinyesha, maji yanasimama na kukosa mwelekeo.