Wachezaji epukeni migogoro kusajiliwa timu zaidi ya moja

Nipashe
Published at 07:14 AM Jun 22 2024
Mpira wa miguu.
Picha: Mtandao
Mpira wa miguu.

WAKATI wachezaji wanaotarajia kushiriki msimu ujao wa Ligi Kuu Tanzania Bara, Ligi ya Championship zamani Ligi Daraja la Kwanza, Ligi Kuu ya Wanawake na ligi nyingine zinazosimamiwa na Shirikisho la Soka Nchini (TFF), wakiwa wamepumzika, tayari dirisha la usajili limeshafunguliwa.

TFF ilitangaza dirisha la usajili lilifunguliwa tangu Juni 15, mwaka huu, hivyo huu ni wakati rasmi wa wachezaji na viongozi kufanya mazungumzo kuhusiana na usajili ikiwa ni maandalizi ya awali kuelekea msimu mpya wa mashindano ambayo utaanza ifikapo Agosti.

Lakini kama vile bado mchakato huu kwetu unaonekana mpya, kila mwaka hatutaacha kusikia migogoro na mivutano kati ya klabu na wachezaji.

Migogoro huanzia baadhi ya klabu kutangaza bado inammiliki mchezaji fulani na mchezaji huyo husika anayetajwa kusikika hadharani akikanusha yeye hana mkataba na timu iliyomtaja, akisema alishamaliza mkataba wa awali.

Lakini pia wakati mwingine tumesikia klabu au mchezaji akitangaza taarifa ambazo si sahihi, bila kujua athari zake za baadaye, maana hapo kuna kosa la udanganyifu au kwa kutokujua kwa sababu mikataba mingi huandikwa kwa lugha ya kigeni ya kingereza.

Kwa upande wa wachezaji wetu wa Kitanzania wanaokwenda kutafuta riziki nje ya nchi wao hukutana na baadhi ya mikataba imeandikwa kwa lugha ya  kifaransa huku bahati mbaya anasaini peke yake bila meneja au wakala na kujikuta amekubali kuweka saini au dole gumba katika mkataba wa muda mrefu, lakini maslahi finyu.

Hizi zama zimekwisha, tunatakiwa tufanye mchakato huu kwa weledi zaidi, ni aibu nchi ambayo ligi yake iko katika nafasi ya juu kwa ubora barani Afrika bado utasikia kuna kesi kuhusiana na kusajili wachezaji bila kufuata taratibu.

Kama ambavyo tumejifunza vitu vizuri kwa nchi zilizoendelea, umefika wakati michakato hii ya kusajili wachezaji ikawekwa wazi na klabu inayotaka kununua au kuvunja mkataba wa nyota ikafahamu taratibu anazotakiwa kuzifuata bila kufanya makandokando ya aina yoyote.

Ni aibu kwa klabu kubwa kama Simba kuanza kugombania mchezaji hadharani wakidaiwa kutotimiza masharti waliyopewa wakati wa kukamilisha usajili wa beki wa kati, Lameck Lawi.

Simba inadai ilipaswa kumpata mchezaji huyo ili kufanya vipimo vya afya kabla ya kukamilisha kiasi cha mwisho cha malipo ya uhamisho wake, nyota huyo alikosekana kwa sababu ya kuwa miongoni mwa wachezaji wa Taifa Stars waliokuwa Indonesia katika mechi za kirafiki za kimataifa, hivyo mchakato wa vipimo ulikwama.

Hata hivyo Simba ilikamilisha sehemu ya pili ya fedha walizotakiwa kulipa, lakini inashangaza Coastal Union ambayo inaongozwa na Mwenyekiti wa Bodi ya Ligi Kuu (TPLB), Steven Mnguto, kueleza beki huyo bado ni mchezaji wao halali.

Tumeshuhudia migogoro ya namna hii baadhi 'ikiwapoteza' wachezaji husika na kushindwa kuonyesha kiwango chake halisi kwa sababu muda wa maandalizi ya kujiandaa na msimu mpya ambao nyota wengine huanza mazoezi au husafiri kwenda ughaibuni, yeye hubakia nyumbani ili kusubiria hatima ya kesi yake.

Na shauri lake linapofanyiwa kazi, hujikuta baadhi ya wachezaji wanaangukia katika kikosi ambacho hakiko 'moyoni' kwake au anatua kwenye timu ambayo hapati namba na hali hiyo humvuruga na kuufanya msimu kwake kuwa mchungu.

Huu ni wakati wa uwazi, teknolojia, klabu zifanye usajili wa wachezaji kwa kufuata taratibu na kanuni zilizowekwa, klabu zisione dhambi pia kutoa ushirikiano kwa timu zinazohitaji kununua jumla au kwa mkopo wachezaji na kufanya zoezi hili kama biashara haramu, hupelekea kuzima ndoto za wachezaji wetu.