Uwekezaji majengo ya ubalozi nje utapunguza gharama

Nipashe
Published at 07:40 AM Jun 20 2024
Majengo pacha Kenya.
Picha: Mtandao
Majengo pacha Kenya.

UZINDUZI wa majengo pacha ya ubalozi nchini Kenya yatakayotumika kama Ofisi ya Ubalozi wa Tanzania umeeleza kuwa ni kitega uchumi kwa ajili ya kuongeza fedha za kigeni nchini.

Ofisi nyingi za balozi za Tanzania nchi za nje ni za kupangisha ambazo pia zinatengewa bajeti ili ziweze kujiendesha.

Kwa sasa imeelezwa kuwa Tanzania inatumia Sh. bilioni 29 kwa mwaka kulipia kodi kwa ajili ya balozi na makazi ya watumishi wake wanaofanya kazi nje ya nchi.

Kwa hiyo kwa ujenzi huo wa majengo pacha ni mkakati wa Serikali ya Rais Samia Suluhu Hassan kutumia viwanja na majengo yake kuongeza mapato ya nchi.

Kwa mujibu wa Waziri wa Mambo ya Nchi za Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, majengo hayo ambayo ujenzi wake utagharamiwa na Mfuko wa Hifadhi ya Jamii wa NSSF, yataipa Tanzania fursa ya kutumia majengo hayo kupangisha kwa makazi na ofisi ili kupata fedha.

Eneo litakalojengwa majengo hayo limitolewa bure na Serikali ya Kenya ikiwa ni kujibu ukarimu wa namna hiyo uliofanywa na Tanzania kwa kuipa Kenya bure eneo iliyojenga ofisi za ubalozi wake, Oysterbay, jijini Dar es Salaam. 

Ushirikiano wa nchi hizi mbili ni wa muda mrefu kuanzia kwa watu wenyewe, kibiashara na kidiplomasia.

Eneo ambalo Tanzania imepewa kujenga ubalozi wake ni mojawapo ya maeneo ya kimkakati jijini Nairobi, kukiwa na ofisi nyingi za serikali. 

Kwa mujibu wa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi, Ajira, Vijana na Walemavu), Deo Ndejembi, uamuzi wa kujenga majengo hayo ulizingatia upembuzi yakinifu uliofanywa na wataalamu na kuona namna mradi utakavyoingiza mapato kwa serikali.

 NSSF ina Kamati ya Uwekezaji ambayo kwa kushirikiana na Bodi ya Wakurugenzi na wataalamu wa masuala ya uwekezaji waliutazama mradi huo na kuona utakuwa na faida kwa Tanzania. Kwa sasa, mwelekeo ni kutazama miradi yenye faida na maslahi kwa taifa.

Miradi kama hii ya majengo ni uwekezaji mzuri na kwa NSSF, itawasaidia kutunisha mfuko wake ili wastaafu wafaidike na michango yao kwa kupata pensheni kwa wakati.

Kuwekeza kwenye miradi inayoleta faida inaleta matumaini hata kwa wafanyakazi wanaochangia kwenye mifuko ya jamii kwa kuelewa kuwa fedha zao zinakwenda kufanya uzalishaji.

Wakati uzinduzi wa majengo hayo ukifanyika, Waziri Mkuu na Waziri wa Mambo ya Nje wa Kenya, Musalia Mudavadi, ameipongeza hatua ya Tanzania kujenga jengo hilo akisema litakuwa mojawapo ya alama za kudumu za uhusiano wa kirafiki baina ya nchi hizo mbili. 

Amesifia ubunifu wa majengo pacha kwa sababu utakuwa kielelezo na kumbukumbu kwamba Tanzania na Kenya ni pacha kwenye uhusiano.

Kwa ubunifu huo pia serikali ya Kenya imejifunza kitu kuhusu namna ya kutumia fedha za taasisi kama NSSF kwa kufanya uwekezaji ili zizalishe.

Tanzania ina jumla ya majengo 109 na viwanja 11 duniani. Pia ina jumla ya balozi 45 na Konseli Kuu tano duniani na kwa mujibu wa mkakati mpya uliopitishwa na Wizara ya Mambo ya Nje hivi karibuni, lengo la serikali ni kutaka kuona inatumia mali zake hizo kuingizia nchi mapato.