Klabu Ligi Kuu Bara kumiliki timu za wanawake iwe sheria

By Mhariri Mtendaji , Nipashe
Published at 10:58 AM Jun 29 2024
Klabu Ligi Kuu Bara kumiliki timu za wanawake iwe sheria.
Picha: TFF
Klabu Ligi Kuu Bara kumiliki timu za wanawake iwe sheria.

WAKATI msimu wa Ligi Kuu ya Wanawake Tanzania ulimalizika kwa Simba Queens ya Dar es Salaam kutwaa ubingwa bila kupoteza mechi hata moja, pazia la Ligi ya Mabingwa wa Mikoa (WRCL), lilifungwa rasmi jana.

Ligi hiyo iliyokuwa inachezwa jijini Dodoma inatoa timu mbili zinazopanda daraja kwenda Ligi Daraja la Kwanza kwa Wanawake (WFDL) katika msimu ujao wa mwaka 2024/2025.

Simba Queens sasa amepata tiketi ya kuiwakilisha Tanzania Bara katika mashindano ya kimataifa ya Klabu Bingwa Afrika Mashariki na Kati kwa Wanawake (CECAFA), yatakayofanyika baadaye mwaka huu.

Ili wawakilishi hao wafanye vizuri, wanahitaji kuwa wametoka katika ligi yenye ushindani na iliyoshirikisha idadi kubwa ya timu na si bingwa ambaye amebeba taji kwa kucheza na timu dhaifu.

Ukomavu wa mwakilishi wa nchi hupelekea kwenda katika mashindano ya kimataifa akiwa na kiwango bora na hapo haendi kwenye michuano hiyo kama msindikizaji, jambo ambalo halitakiwi kutokea.

Wakati tunalipongeza Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) na Chama cha Mpira wa Miguu cha Wanawake Nchini (TWFA), kwa kusimamia na kuendesha vizuri Ligi za Wanawake na mashindano mengine mbalimbali, tunaliomba shirikisho hilo kuweka kanuni ya lazima kwa kila klabu ya Ligi Kuu Bara kumiliki timu ya wanawake. 

Kwa kufanya hivyo, tutaongeza hamasa katika soka la wanawake kwa kuwa na idadi kubwa ya timu zitakazoshiriki Ligi Kuu kama ilivyo kwa upande wa wanaume. 

Tunaamini kuwepo kwa kanuni hiyo inayolazimisha kuandaa kikosi cha wanawake, kutaendelea kutoa fursa kwa wachezaji wanawake lakini pia itawaongezea ajira wachezaji na wafanyakazi wengine wote watakaoajiriwa na klabu husika. 

Wote tunafahamu michezo husaidia kuimarisha afya, hivyo timu za Ligi Kuu zinapomiliki klabu za wanawake kutawaongezea vipato kwa sababu baadhi ya mechi zimekuwa zinahudhuriwa ba idadi kubwa ya mashabiki ukilinganisha na wanapocheza wanaume. 

Lakini sheria ya kuzitaka timu zote za Ligi Kuu zimiliki timu za wanawake zitasaidia hata pale klabu mojawapo itakapokata tiketi ya kushiriki mashindano ya kimataifa yanayoandaliwa na kusimamiwa na Shirikisho la Soka Afrika (CAF), haitaumiza kichwa kusaka timu ya ‘kukodi’ ili kutimiza sifa. 

Tunashauri kuwepo kwa umiliki kwa sababu kuingia ubia au ushiriki, haifanyi klabu husika kushiriki kikamilifu katika shughuli za kila siku za uendeshaji tofauti na wanavyowajibika katika upande wa wanaume au timu za vijana. 

Lakini kama ambavyo tunaamini wachezaji wazuri wa timu za taifa hupatikana kutokana na kuwapo kwa misingi mizuri ya soka la vijana, huu ni wakati wa TFF kuweka kanuni hiyo ambayo itasaidia kuongezeka kwa idadi kubwa ya wachezaji wanawake. 

Itakuwa vigumu huko mbele kuziambia klabu zinazoshiriki Ligi Kuu Tanzania Bara kuwa na timu za vijana za wasichana za umri chini ya miaka 20 na  U-17, wakati hazikuwekewa kanuni za kumiliki timu ya wanawake. 

Mabadiliko ya kanuni yatasaidia zaidi kuzalisha wachezaji wanawake ambao waliotangulia wameonyesha uwezo mkubwa na kutangulia kushiriki fainali za Kombe la Dunia za umri chini ya miaka 17, wakati wanaume hawajawahi kukata tiketi ya kushiriki michuano yoyote inayoandaliwa na Shirikisho la Soka la Kimataifa (FIFA).