Wageni wanaosajiliwa wapimwe afya kuepuka wachezaji 'pancha'

By Adam Fungamwango , Nipashe
Published at 11:03 AM Jun 29 2024
Wageni wanaosajiliwa wapimwe afya kuepuka wachezaji 'pancha'.
Picha: Mtandao
Wageni wanaosajiliwa wapimwe afya kuepuka wachezaji 'pancha'.

HIKI ni kipindi cha usajili, huku timu zote zikisaka wachezaji kwa ajili ya kuboresha vikosi vyao.

 Nimeona klabu nyingi za Ligi Kuu nchini  zikisaka wachezaji kutoka nje ya nchi.

Hata Mashujaa FC nayo hivi karubuni, baadhi ya viongozi wao walikaririwa wakisema iwapo watapata ruhusu kutoka kwa mabosi wao Makao Makuu, wanaweza kusajili wachezaji wa kigeni.

Ikumbukwe kuwa Mashujaa ni timu inayomilikiwa na Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ), hivyo kwa taratibu zao hairuhusiwi kuwa na wachezaji kutoka nje ya nchi, labda kama kibali kitatolewa, tusubiri tuone.

Kwanza kabisa nipende kuzipongeza klabu nyingi za Tanzania ambapo kwa miaka ya hivi karibuni wamekuwa wakileta wachezaji wenye uwezo mkubwa na kuiheshimisha ligi yetu.

Ligi ya Tanzania Bara kwa sasa inahesabika kuwa ni moja kati ya ligi bora barani Afrika, ikikamata nafasi ya sita.
 Imekuwa ikileta wachezaji ambao kila mwaka wanamezewa mate na klabu kubwa na tajiri barani Afrika.

Zamani huwezi kukuta eti mchezaji hata wa Simba au Yanga anatakiwa na klabu ya Mamelodi Sundowns, Kaizer Chiefs za Afrika Kusini, au Al Ahly na Zamalek za Misri, ila kwa sasa tunaliona hilo likitokea. 

Luis Miquissone, winga raia wa Msumbiji ni mfano wa hili, alisajiliwa na Al Ahly akitokea Simba.

Fiston Mayele, mshambuliaji raia wa Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo, alisajiliwa na klabu ya Pyramids ya Misri akitokea Yanga.

Cha kufurahisha, hata klabu kama za Singida Big Stars, Tabora United na Coastal Union kwa miaka ya hivi karibuni zimekuwa zikisajili wachezaji wa kigeni wenye uwezo mkubwa kiasi cha kutamaniwa hata na klabu kubwa za Simba, Yanga na Azam FC.

Pamoja na hayo yote kuna kitu bado naona hakijakaa sawa na kama kikiwekwa vizuri Ligi ya Tanzania inaweza kuwa ndiyo bora zaidi Afrika.
 Kuna baadhi ya wachezaji kutoka nje wanasajiliwa wakiwa na majeraha sugu na kuzipa hasara klabu, pamoja na ligi yenyewe.

Kama nafasi za hawa magonjwa zingechukuliwa na wachezaji waliofiti ingawezekana kabisa ligi ingekuwa ya kuvutia zaidi.
 Simba, Yanga na Azam, ambazo zinasajili wachezaji wote 12 wa kigeni wanaoruhusiwa kwa kiasi kikubwa si wote wanaokuwa fiti kwa asilimia 100.

Wengine wanatoka huko walikotoka wakiwa na majeraha ya kudumu, kiasi kwamba wanapofika kwenye klabu hizi wanazifanya kama wodi za wagonjwa, huku wakiwa wanapokea mishahara.

Mfano mdogo tu Simba ilimsajili Aubin Kramo mwanzoni mwa msimu uliopita, lakini hadi leo hawajafaidi matunda yake. Alicheza mechi moja tu ya Simba Day dhidi ya Power Dynamos, baada ya hapo hakucheza tena kwa kile kilichodaiwa kuwa na majeruhi.

Ukiangalia kwa umakini utagundua kuwa siyo majeraha ambayo aliyapatia Simba bali alitoka nayo huko, ila alikuja nchini na kujitonesha.
 Azam FC imekuwa mara kwa mara ikilazimika kuwasafirisha wachezaji wake nchini Afrika Kusini kwa matibabu. 

Wengi wao ni majeraha ambayo wametoka nayo huko, hii yote ni ukosefu wa umakini katika kuwapima afya.
 Wakati wenzetu nje huko wako makini kuwapima kwa manufaa ya mchezaji mwenyewe na klabu, huku inafanywa kama fasheni tu, sijui huwa wanapima nini.

Sijawahi kusikia mchezaji hakufuzu vipimo, ila huko Ulaya wachezaji kadhaa wanafeli vipimo, huku klabu inaogopa kumpoteza mchezaji. Matokeo zinakuwa na wachezaji 'pancha' ambao wanakula tu pesa ya klabu bila kuzalisha chochote.

Hivyo nashauri kuelekea Ligi Kuu msimu ujao, klabu zifanye vipimo vya ukweli ili kuondokana na kusajili wachezaji wenye majeruhi wa kudumu.
 Ni bora kuwa na wachezaji pungufu ya 12, kuliko kuwa na wafanyakazi hewa  kutokana tu na kushindwa kufuatilia historia zao, pamoja na kutowafanyia vipimo kamilifu.