Kanuni hii ipitishwe Ligi Kuu kukomesha imani za kishirikina

Nipashe
Published at 10:05 AM Jul 01 2024
Ofisa Habari na Mawasiliano wa Bodi ya Ligi, Karim Boimanda.
Picha: Mtandao
Ofisa Habari na Mawasiliano wa Bodi ya Ligi, Karim Boimanda.

TAYARI Bodi ya Ligi Kuu imeendelea kupokea maoni kwa ajili ya maboresho la Kanuni za Ligi Kuu Tanzania Bara msimu wa 2024/25.

Ofisa Habari na Mawasiliano wa Bodi ya Ligi, Karim Boimanda, hivi karibuni alisema wameendelea kupokea maoni kwa njia mbalimbali za mawasiliano, huku akiahidi kuwatembelea pia wadau wa soka, vikiwamo vyombo vya habari kwa ajili ya kupata mawazo mengi zaidi yatakayofanya kuwe na kanuni bora msimu ujao.

Alikiri kuwa eneo la imani za kishirikina ndilo lililoonekana kuvutia wadau wengi kutoa maoni yao kuliko kanuni zingine.

Pamoja na mambo mengine, sisi tunaona imefika wakati sasa jambo hili lifanyiwe kazi kuelekea msimu ujao wa Ligi Kuu, ili hata kama halikuisha, tuone likipungua kwa kiasi kubwa kwani linachafua sana ligi yetu ambayo kwa sasa ni ya sita kwa ubora barani Afrika.

Hii ni kutokana na kuona ni kosa ambalo limekuwa likijirudia kama ambavyo wenyewe Bodi ya Ligi wanavyobainisha.

Kwa ujumla haturidhishwi na adhabu za faini zinazotolewa, ambapo klabu hazishtuki na hazioni shida kuilipa, hivyo kurudia mechi baada ya mechi, huku taarifa zikieleza hata hizo faini zenyewe hukatwa kwenye viingilio vya mechi.

Tunadhani umefika wakati sasa kupitishwa kanuni kwa klabu itakayobainika na kuthibitishwa imefanya vitendo hivyo ikatwe angalau pointi moja kwani suala la faini sasa linaonekana kuwa la kawaida kwao.

Pointi moja tu, inatosha kuitoa timu kwenye reli na isirudie tena mchezo huo, na kama hiyo haitoshi basi ikiwezekana iwe pointi na faini pia.

Kuzikata pointi ndiyo adhabu pekee inayoweza kuzitisha klabu kuacha mtindo huo kwani viongozi watawajibika kwa wanachama na mashabiki wao.

Timu inapokatwa pointi halafu ikaachwa nyuma na wenzake, au kuukosa ubingwa kwa sababu ya pointi moja au mbili zilizokatwa kwa sababu ya vitendo vya kishirikina, viongozi watakuwa na cha kujibu kwa wanachama na mashabiki wao.

Tunaamini kwa sasa viongozi wa klabu hizi hawaogopi adhabu hii kwa sababu nyingi sana. Chache ni kwamba haziwaumizi, yaani kuwanyang'anya ushindi wanaoupata, lakini pia hata pesa zenyewe hawatoi mfukoni, bali ni zile zinazokatwa moja kwa moja timu zao zinapocheza.

Tena klabu kubwa kama za Simba na Yanga huwa hazisikii maumivu kabisa kwani zinavuna pesa nyingi za kiingilio cha mashabiki, kwa hiyo hata pesa inayokatwa kwao hazioni tatizo.

Tunatambua maana ya adhabu ni kumfanya mtu ajutie kile ambacho alikitenda na asikirudie tena, hivyo ukiona mtu anapewa adhabu halafu anarudia tena na tena, ujue hiyo kwake siyo adhabu, unapaswa kubadilisha.

Kwa sababu lengo la kufanya vitendo vya kirishikina, kuingia kwenye mlango usioruhusiwa, kuruka ukuta na kufanya chochote kinachoonyesha kuwa si cha kawaida, ni kusaka ushindi, yaani pointi tatu, hivyo utakapozipata na kisha ukazinyang'anywa ulichokifanya hutakirudia tena.

Kama Bodi ya Ligi ikipitisha kanuni hiyo na kuisimamia ipasavyo, tunaamini wahusika wataacha vitendo hivyo.

Ila katika hilo tunapendekeza pia timu isikatwe kama vitendo hivyo vinafanywa na mashabiki badala yake wao nao wapate adhabu yao peke yao, kwani kwa kufanya hivyo kunaweza kujitokeza mashabiki wa upande wa pili wanaoweza kuvaa jezi za mpinzani wao kwa lengo la kwenda kuiharibia kwa kujifanya wanafanya vitendo hivyo vinavyoashiria ushirikina.

Hii ni kwa sababu kwenye soka la Tanzania kuna kitu kinaitwa kuhujumiana, inawezekana watakaofanya hivyo ikawa si mashabiki halisi wa timu ile.

Adhabu ya kukatwa pointi itolewe kwa makosa ya viongozi, wachezaji na watu ambao wanajulikana rasmi kuwa wapo ndani ya klabu.