Klabu zitumie 'pre season' kujenga vikosi kuwa imara

By Adam Fungamwango , Nipashe
Published at 10:11 AM Jul 01 2024
Timu ya Simba ikiwa kambini Morocco kwa ajili ya maandalizi ya msimu wa 2023/24.
Picha: Maktaba
Timu ya Simba ikiwa kambini Morocco kwa ajili ya maandalizi ya msimu wa 2023/24.

YANGA ilianza Ligi Kuu msimu uliopita kwa kuitwanga KMC mabao 5-0 katika mechi ya kwanza ya ufunguzi.

Simba nayo iliiadhibu Mtibwa Sugar mabao 4-2, ikiwa pia ni mechi ya ufunguzi, raundi ya pili Yanga ikarudia kile ilichokifanya raundi ya kwanza, ikiifanyia mauaji JKT Tanzania kwa idadi kama ile ile ya mabao 5-0 iliyoifunga KMC.

Labda hapa tujiulize ni kwa nini timu hizo zilichapika mabao mengi mwanzoni tu mwa msimu.

Ukweli ilionekana hazikufanya maandalizi mazuri ya msimu, na kwa bahati mbaya sana zinakutana na timu kubwa na ngumu.

Siyo hizo tu, hata kama zingekuwa timu zingine ambazo zingekuwa hazijafanya 'pre season' yao vizuri zingepigwa nyingi.

Vipigo vile vinazikumbusha klabu zinazojiandaa na msimu mpya wa mashindano kwenda kujiandaa kisawasawa na wiki hizi za kambi ya mwanzo, inayoitwa kwa lunga la kigeni 'pre season.'

Hiki ni kipindi cha kutengeneza timu bora ya msimu mzima, na iwapo kitachezewa basi wachezaji hawatofanya vema msimu mzima.

Hiki ni kipindi cha wachezaji kutengeneza pumzi, na stamina ambayo humfanya kuweza kuhimili mikikimikiki ya msimu mzima wa ligi na mashindano mengine.

Ni kipindi ambacho wachezaji hufanya mazoezi magumu kuliko yote watakayoyafanya baada ya hapo, kwani watakachotakiwa ni kuilinda pumzi na stamina iendelee kuwapo na si kuitafuta tena.

Mchezaji anapoyakosa au kutoyafanya sawasawa, hata awe na kipaji kizuri vipi hawezi kuwa bora au kwenye kiwango chake kilichozoeleka kwa msimu mzima.

Moja ya vitu vilivyoisaidia zaidi Yanga misimu hii mitatu kutwaa ubingwa ni wachezaji wake kuwa na utimamu mzuri wa mwili.

Ndiyo maana hata wale ambao hawakuwa sehemu ya kikosi cha kwanza, bado walikuwa na msaada mkubwa wanapoingia kwani hata kama hana kiwango kikubwa sana, lakini fiziki ilikuwa inawasaidia kutimiza malengo.

Simba ilikuwa ni timu ambayo haikuwa na utimamu mkubwa sana wa mwili kwa wachezaji wake, na ulikuwa unashuka kile mechi zinavyoendelea.

Nazishauri klabu ambazo mwezi huu wa saba zinaanza maandalizi kuwa siyo kipindi cha mbwembwe na 'pikniki', bali ni cha kujiweka fiti kwa msimu unaokuja.

Kwa viongozi hiki ni kipindi ambacho wanatakiwa kuwa wamekamilisha vitu vyote kuanzia usajili, makocha mpaka vifaa vya mazoezi, ili kuepusha kile kilichoonekana msimu uliopita baadhi ya timu zikiwa mpaka na wachezaji watano tu kambini, wengine hawajaja kwa kutopewa pesa zao za usajili, au kuendelea kusajili.

Hiki siyo kipindi cha kufanya usajili na mchezaji anakuja siku chache kabla ya maandalizi kukamilika.

Siyo kipindi ambacho klabu inakuwa na wachezaji halafu haina kocha ambaye anakuja wiki moja kabla ya ligi kuanza.

Klabu yoyote itakayofanya hivyo, haitofanya vema kwenye ligi kwani kinakuwa ni kipindi cha kucheza mechi, kutengeneza mfumo wa kukabiliana na timu husika na kusafiri tu, si cha kutengeza fiziki.

Mara nyingi viongozi wa klabu wanakosea kufanya hivi, badala yake zigo wanawaangushia makocha.

Huwezi kuwa na wachezaji kambini kipindi cha 'pre season' halafu ndiyo unatafuta kocha, au unaye lakini bado hajawasili kwa sababu hajalipwa chake, au ndiyo unaendelea kusajili.

Nadhani viongozi wa klabu wanatakiwa wanielewa, ili ligi ikianza msiseme kuwa sijawaambia.