Safi sana PASADA, hizo nyendo zenu zimewaokoa wenzetu wengi

By Halfani Chusi , Nipashe
Published at 12:22 PM Mar 29 2024
Nembo inayotumika katika kuhamasisha watu kujikinga na maambukizi ya Virusi vya Ukimwi.
Picha: PASADA.
Nembo inayotumika katika kuhamasisha watu kujikinga na maambukizi ya Virusi vya Ukimwi.

SHIRIKA lililo Chini ya Jimbo Kuu Katoliki la Dar es Salaam (PASADA), Linalojihusisha na utoaji wa huduma kwa watu wanaoishi na Virusi vya Ukimwi, kuanzia April. mwaka jana hadi Desemba, liliibua wagonjwa wa kifua kikuu 919 na kuwapatia matibabu bure katika mikoa ya Pwani na Dar es Salaam.

Shirika hilo liliibiua wagonjwa kupitia utambuzi na uchunguzi uliofanywa kupitia mradi wa wake uitwao ‘Stop TB Partnership.’ 

Mwishoni mwa wiki iliyopita mkoani Dar es Salaam na Meneja Mradi wa TB Pasada, Jacquline Mwaipaja, anasema katika idadi hiyo kati yao 111 walikuwa watoto wenye umri chini ya miaka 15, pia kuna wengine 256 waliogundulika na maambukizi ya Virusi vya Ukimwi na Kifua Kikuu.

Pia, akasema kwa mwaka uliopo, walifanikiwa kuwafikia wagonjwa wengine 622, hata wakawapatia huduma za kiugunduzi na matibabu ya kifua kikuu, akiwa na msisitizo alipata changamoto wagonjwa wengi walikuwa hawana gharama ya kulipia kipimo cha mionzi (X - Ray).

Ni jambo linaloungwa mkono na Mkurugenzi wake Mtendaji, Cayus Mrina, anayetamba kwamba kufanikiwa katika mradi huo, ni matokeo ya serikali ya sasa, kuweka mazingira wezeshi kati ya serikali na mashirika binafsi.

“Amejitahidi kuhakikisha huduma za afya zinafika mahali kote, kila mahali kuna vifaa na huduma za afya, tunatoa huduma za kimwili na kiroho ndio maana kauli mbiu yetu inasema ‘roho yenye afya na mwili wenye afya’ kwa hiyo watu wanapata huduma zote,” anafafanua.  

Anarejea historia, shirika hilo lilianzishwa mwaka 1992 kwa lengo la kutoa huduma kwa watu wanaoishi na Virusi vya Ukimwi, akikumbushia kipindi hicho kulikuwapo wagonjwa wengi, ndipo  jitihada za mapadri zikazaa kuwapo PASADA.

“Mapadri Wamisionari waliokuwa wanafanya kazi ya kuhudumia wagonjwa kiroho, wakaona kuna haja ya kuungana pamoja kupata sehemu ya kituo cha kuhudumia wagonjwa,” anasema  

Anasema mpaka sasa kuna vituo 25 katika mkoa wa Pwani na Dar es Salaam, ambavyo vinatoa huduma hizo, akisistiza kwa sasa wanafanya kazi hizo kwa kasi kubwa ili kuchangiza malengo ya serikali.   

Ni jambo linaloungwa mkono pia na mganga mkuu wa halmashauri ya Temeke aliyekuwa mgeni rasmi kwa niaba ya serikali Jonasi Lulandala, anayeahidi kuyafanyia kazi maombi yao ya kushusha gharama katika kipimo cha mionzi.

“Nitalifikisha kwa Mganga Mkuu wa Mkoa nione namna gani tutalifanyia kazi, ninawapongeza PASADA, kwa kazi mnazozifanya katika jamii, kwa kutibu wagonjwa na kuzuia maambukizi mapya, kwa hiyo kuna kazi kubwa ya kufanya kaungalia kwa nini wagonjwa wanaongezeka,” anasema 

Pia, walikuwapo wanufaika wa mradi huo waliotibiwa bure na kupona kabisa. Shabani Salumu, ni miongoni mwao akisema alikuwa mwathirika wa kifua kikuu alifikiwa na PASADA na kupatiwa matibabu na sasa amepona kabisa.

“Mara ya kwanza walinikuta kijiweni mimi ni mwathirika wa dawa za kulevya, wakanihoji wakachukua makohozi yangu, wakaenda kuyapima.

“Siku mbili baadaye wakanifuata, wakasema makohozi hayajaonyesha kama unakifua kikuu, wakaniambia inabidi tukupime kwa mionzi nikawaambia gharama hizo mimi sina wakasema tutakusaidia. 

“Baada ya hapo wakanifanyia hicho kipimo, nikagundulika nina tatizo la kifua kikuu na sasa ninatumia dawa naendelea vizuri ninawashukuru sana,” akatamka. 

Mnufaika mwingine, Hemedi Jumanne anasema amesumbuliwa sana na kifua kikuu kwa zaidi ya miezi miwili, alipopima makohozi katika hospitali mbalimbali, hayakuonyesha ugonjwa.

“Katika matembezi yangu nikakutana na PASADA, nikawasimulia wakaniambia inabidi nipime kipimo cha mionzi nikawaambia sina hela wakaniambia tutakupa msaada.

“Waliponipima nikakutwa nina kifua kikuu ninawashukuru sana waendelee na huduma hii kwa sababau huko mtaani wapo wengi wanaoumwa, lakini hawana uwezo wa kifedha” anashauri

Ni jambo linalopaswa kuungwa mkono kusaidia wenye uhitaji katika jamii kwenye nyanja mbalimbali sio afya pekee wapo wanaohitaji mitaji kukuza biashara, wajane, yatima na wenye ulemavu.