Rehema apewe maua yake, siku yao awa na kinamama gerezani Segerea

By Halfani Chusi , Nipashe
Published at 03:29 PM Mar 20 2024
Gereza la Segerea.
PICHA: SWAHILI TIMES
Gereza la Segerea.

UKISIKIA kubeba agenda ya kuwainua wanawake ndio huku sasa, wanawake waishio Wilaya ya Ilala wako mikono salama kuwezeshwa kiuchumi na hata kupewa elimu ya ujasiriamali.

Msukani wa yote hayo, ni Mwenyekiti wa Jukwaa la Uwezeshaji Wanawake Kiuchumi katika Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam, Rehema Sanga.

Kwa wanawake wa wilaya ya Ilala jina lake sio geni masikioni mwao. Hiyo ni kutokana na ukubwa wa mambo anayoyafanya katika jamii yanayowabeba zaidi wanawake. 

Lililonikuna kwake zaidi, kusikia akisema Siku ya Wanawake Duniani, aliamua kusherehekea kwa kuwatembelea wafungwa wanawake walioko katika Gereza la Mahabusu Segerea na baadaye akaenda kutoa msaada katika Hospitali ya Bonyokwa, kusaidia ukamilishaji wa wodi ya kujifungulia kinamama.

Rehema anasema, katika kutekeleza hayo, alishirikiana na viongozi kutoka Ofisi ya Mkuu wa Wilaya Ilala, Idara ya Maendeleo Jamii Halmashauri ya jiji la Dar es Salaam. 

“katika kuadhimisha Siku ya Wanawake Duniani, mara nyingi tumekuwa ‘tunakula bata’, lakini safari hii tukasema tuwakumbuke wanawake waliopo katika Gereza la Segerea kwa kuwapatia msaada wa mahitaji mbalimbali. 

“kilichonishangaza zaidi, tumekuta mikoba mizuri ya baadhi ya wanawake waliokuwa kwenye hilo gereza, kuna ‘programu’ ya mafunzo inaendeshwa nimehamasika kwa kuona kuna wanawake wanazalisha bidhaa huko upande wa pili.

“Nikaona tunaweza kuwasaidia kukuza soko la bidhaa zao ikawasaidia kupata fedha kwa ajili ya uendeshaji, ndio maana tuliguswa tukaona twende huko,” anasema Rehema. 

Mwanamkwe huyo anawashauri wadau wengine wa maendeleo, waendelea kuwakumbuka wanawake walioko gerezani ili waweze kupata mahitaji muhimu.  

Anaisema anatamani wadau waguswe wapeleke vitu kama magodoro, sabuni za kuogea, kufulia na kuwasapoti kwa kununua bidhaa wanazozalisha ili wapate kipato.

“Sisi kama Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam, tutahakikisha bidhaa zao zinafika sokoni, pia zipate majina na wadau wazinunue kwa lengo la kusapoti miradi ya wanawake walioko gerezani. Tunaamini wakimaliza vifungo vyao watautumia huo ujuzi kwa nia ya kujiendeleza. 

“Wana miradi mingi ya bustani, kushona kwa hiyo tunaangalia namna gani tutawasaidia bidhaa zao kutoka nje zikauzwa,” anasema Rehema.           

Ni simulizi kwamba, akaongozana na kutoa msaada huo katika gereza la Segerea aliongozana na Mbunge wa Jimbo la Segerea, Bonnah Kamoli kutoa msaada wa kifedha katika Zahanati ya Bonyokwa, kwa ajili ya kurekebisha wodi ya kujifungulia kinamama na kuepeleka vifaa vyake.

Ni aina ya misaada ambayo jamii inapaswa kutoa, kuwakumbuka wenye uhitaji maalumu kama watoto yatima, wajane, kama ambavyo Jukwaa la Uwezeshaji Kiuchumi Halamashauri ya Jiji la Ilala limethubutu.

Ni jambo lililoukosha uongozi wa hospitali na wana - Bonyokwa kwa ujumla kwamba msaada huo utasaidia kuboresha upatikanaji wa huduma ya afya kwa mjamzito.