Mwezi Mtukufu umeanza, tujifunze na kujirekebisha jamii ivutiwe nasi

By Pilly Kigome , Nipashe
Published at 09:51 AM Mar 14 2024
Mwezi.
PICHA: MTANDAO
Mwezi.

SIKU ya Machi 12, waumini wa dini ya Kiislamu Tanzania na duniani kote kwa ujumla, wameanza kutekeleza ibada muhimu ya kutimiza Nguzo ya Nne katika Nguzo Tano, zinazosimamisha dini hiyo ambayo ni kufunga Mwezi Mtukufu wa Ramadhani.

 Kwa mujibu wa maandiko ya dini ya Kiislamu, kuna nguzo tano ambazo ni msingi zinazosimamisha imani ya dini hiyo na kila muumini wa dini hiyo, anatakiwa atekeleze nguzo hizo, ndipo ahesabike kuwa ni miongoni mwa waumini wa dini hiyo.

Kati ya hizo tano, kuna moja ambayo si lazima muumini kuitekeleza japo ni muhimu kwa walioamini, kwa kuwa maandiko yanasema ni ‘kwa wale wenye uwezo pekee wa kufanya hivyo.’

Nayo ni ile ya kwenda kuhiji Mji Mtakatifu wa Makka, kwenye nyumba tukufu. Maandiko yanasema, hii ni kwa wale wenye uwezo wa kifedha na afya, ni lazima wafanye hivyo, ili waweze kwenda kutekeleza ibada hiyo muhimu.

Ngoja nizitaje nguzo hizo tano muhimu kwa mtiririko maalum kwa mujibu wa maandiko kutoka katika Kitabu Tukufu cha Quruan.

Nguzo ya kwanza, ni kumuamini Mwenyezi Mungu na mjumbe wake Muhammad (SAW). Ya pili ni kuswali swala tano katika vipindi tofauti, vilivyopangwa katika mtiririko maalum pasipo kuuvuruga.

Nguzo ya tatu, ni kutoa zaka na ya nne, ni Kufunga Mwezi Mtukufu wa Ramadhani na ya Tano, ni kwenda Kuhiji Mji Mkukufu kwa wale wenye uwezo.

Hebu naomba tukumbushane nikiwa ni mmoja wa muumini wa dini hiyo mwezi huu tunatakiwa tutende mambo yaliyo mema, kufanya mambo ya kheri na isiwe tufanye tu katika mwezi huu la hasha, bali iwe ni mwendelezo katika kuyaendeleza hayo mambo mema na mazuri.

Imekuwa na mazoea ya waumini hao kujisahau kwa kiwango kikubwa sana kwa kumuongopea Mungu dhahiri, shahiri kwa kipindi hiki kujifanya ama kujinasibu ni watu bora na kipindi hiki kiisha wanarudi na kufanya mambo ya hovyo.

Kwa pamoja, tukishirikiana kufanya mambo mazuri na safi basi naamini hakutakuwa na mambo ya uvunjifu wa amani nchini, hakutakuwa na ukatili wa kijinsia, hakutakuwa na aina yoyote ya wizi na nchi itabaki kuwa na amani na salama.

Ukweli ni kwamba, katika kipindi hiki cha mwezi Mtukufu wa Ramadhani, ndicho kinachowakumbusha Waislamu walio wengi kufanya mambo mema na  mazuri.

Kutokana na ukweli huo hata viongozi wa dini wa kiislamu kutoka maeneo tofauti tofauti wamekuwa wakitumia kipindi hiki katika kuwajenga waislamu kwani kumekuwa na wingi ama mafuriko wa waumini katika nyumba za ibada.

Hii inatokana na kujiangalia kwa matendo yao maovu hivyo wengi kuonekana kumrudia mungu na kubadilika kitabia.

Mufti Mkuu wa Tanzania, Abubakar Zuberi, wakati akiwatangazia waislamu kuanza kwa kutekeleza ibada hiyo aliwataka Waislamu kote nchini kuishi kwa upendo na amani na kuwataka wazidishe kuomba msamaha kwa Mwenyezi Mungu, pasi na kuiombea nchi iendelee kuwa na amani isiingie migogoro.

Aliwataka na kuwaomba waumini wa dini ya Kiislamu kuwaombea viongozi wetu wakuu wa nchi, ikiwamo na kuiombea nchi kuepukana na mabalaa na maradhi makubwa katika nchi yetu.

Mbali na dini ya Kiislamu, dini zote nchini zinahubiri amani, upendo, kusamehemana kuomba sana Mungu, unyenyekevu kutendeana mema.

Rai yangu mbali na kuutumia mwezi huu mtukufu wa Ramadhan vizuri mimi napenda kusema ndugu zangu Waislamu wenzangu tuendeleze mazuri yetu na mema yetu hata kama mwezi huu utaisha.

Nirudi kwa upande wa wazazi tunatakiwa tujitahidi katika malezi ya watoto yetu kwani kumekuwa na mmomonyoko wa maadili katika jamii yetu basi tuutumie vyema mwezi huu pia katika kujenga tabia zilizo njema kwa watoto wetu.

Ramadani Mubaraqa!