Tusikejeli anayofundisha Prof. Janabi kuhusu nafasi ya afya zetu ya kila siku

By Sabato Kasika , Nipashe
Published at 12:25 PM Feb 29 2024
 Profesa Mohamed Janabi.
PICHA: MTANDAO
Profesa Mohamed Janabi.

IDADI ya wagonjwa wanaofika katika Hospitali ya Taifa Muhimbili kwa ajili ya kupata huduma ya kusafisha figo kila siku, ni kati ya 120 hadi 130 na sababu kubwa inaelezwa inatokana na mtindo wa maisha.

Nadhani ni vyema kuheshimu taaluma ya mtu na kumsaidia kuhamasisha jamii kuzingatia mtindo mzuri wa maisha, ili kuepuka magonjwa kama hayo ya figo kwa kuepuka vitu vinavyokatazwa.

 Kutokana na hali hiyo, Mkurugenzi wa hospitali hiyo, Profesa Mohamed Janabi, anahimiza jamii kuchukua tahadhari na kufuata mtindo bora wa maisha kwa kuepuka vitu hatari  zaidi kwa afya mwilini.
 
 Prof. Janabi anataja vitu hatari vya kuepukwa kuwa ni sukari na wanga, huku akibainisha kuwa mafuta si hatari kama ambavyo baadhi ya watu wamekuwa wakidhani, na kwamba mwili hautunzi sukari wala wanga.
 
 Anafafanua kwa kawaida, mwili hubadilisha sukari na wanga kuwa mafuta, hivyo anahimiza watu kupunguza matumizi ya vitu hivyo, na kwamba ugonjwa wa sukari husababishwa na lishe.
 
 Hivyo, anasema, ni lazima jamii ibadilishe mtindo wa maisha na kwamba mtu akibahatika kuzungumza na mgonjwa anayesafishwa figo, ndipo  atajua umuhimu wa kujitunza kwa kubadili mtindo wa maisha.
 
 Prof. Janabi amekuwa akitoa mafundisho mara kadhaa kuhusu umuhimu wa kutunza afya, lakini baadhi ya watu wamekuwa wakimkejeli katika mitandao ya kijamii kana kwamba anachofundisha hakina maana.
 
 Nadhani ni vyema kuheshimu taaluma ya mtu na kumsaidia kuhamasisha jamii kuzingatia mtindo mzuri wa maisha, ili kuepuka magonjwa kama hayo ya figo kwa kuepuka vitu vinavyokatazwa.
 
 Kukubali ushauri au mafundisho ya Prof. Janabi ni sawa na kuepuka magonjwa yasiyoambukiza, hivyo, badala ya kukejeli tuchukue hatua zinazoelekezwa na mtaalamu huyo wa afya.
 
 Magonjwa yasiyoambukiza anayataja kuwa ni kisukari, shinikizo la damu, kiharusi na ugonjwa wa figo, ambayo yanaenezwa kwa njia mbalimbali yakitesa baadhi Watanzania.
 
 Itakuwa sahihi iwapo tutaendelea kufuatilia taarifa sahihi za namna ya kujikinga na magonjwa yasiyoambukiza na yanayoambukiza, ili kupata taarifa hizo kwa usahihi badala ya kukejeli.
 
 Njia mojawapo ya kufuatilia mafundisho ya Prof. Janabi, ambaye kila mara amekuwa wakitoa rai kwa Watanzania kuzingatia mtindo mzuri wa maisha, ili kuepuka magonjwa mbalimbali yakiwamo yasiyoambukiza.
 
 Serikali imekuwa ikijitahidi kuboresha huduma za afya na inaendelea na juhudi hizo ili kuokoa maisha ya Watanzania ambao wana magonjwa yasiyoambukiza ikiwamo kutoa matibabu na elimu, hivyo ni wajibu wetu kuzingatia elimu hiyo kwa ajili ya usalama wa afya zetu.
 
 Ikumbukwe, utafiti wa kitaifa wa viashiria vya magonjwa yasiyoambukiza uliozinduliwa na Wizara ya Afya mwaka jana, ulionyesha kuwa magonjwa yasiyoambukiza (NCDs) yanachangia takriban asilimia 33 ya vifo vyote nchini.
 
 Pamoja na hayo, takwimu za Shirika la Afya duniani (WHO) kwa mwaka 2020 zikionyesha kuwa magonjwa hayo yalichangia zaidi ya vifo milioni 41 sawa na asilimia 71 ya vifo vyote duniani ukilinganisha na vifo milioni 57 kwa mwaka 2016 duniani.
 
 Hayo ni kwa mujibu wa Waziri wa Afya wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, Nassor Mazrui, wakati wa uzinduzi wa utafiti wa kitaifa wa viashiria vya magonjwa yasiyoambukiza au ‘Steps Survey 2023’.
 
 Kwa maana hiyo, suala la kufuatilia mafundisho ya Prof. Janabi na  kuyafanyia kazi ni la muhimu, kuliko kukaa kwenye mitandao ya kijamii na kuanza kukejeli kuwa anatisha ili watu wasiendelee kufurahia maisha.
 
 Sasa kwa kuwa serikali inatekeleza mkakati wa kitaifa wa kukabiliana na magonjwa hayo kwa kutoa elimu kwa jamii ya jinsi kujikinga nayo, ninadhani ni wajibu wa kila mmoja kuzingatia elimu hiyo.