Ndiyo matokeo ya kuisifia pombe

By Sabato Kasika , Nipashe
Published at 10:40 AM Mar 05 2024
Pombe.
PICHA: MTANDAO
Pombe.

IKIWA wewe ni mtoto na tena bado ni mwanafunzi kumbuka huruhusiwi kugusa vilevi, hata kama utaimbiwa bia tamu. Jiepushe nayo.

Lakini  angalia, kwa msisitizo hata vifungashio vya vilevi na viongeza nguvu (energy booster), vimeweka onyo 'hairuhusiwi kutumika na mwenye  miaka 18'. Sembuse wewe mtoto wa miaka 12?

Hivyo kwa ujumla watoto na wengine ambao hawajajitambua tena hawajiwezi kimaisha ni marufuku kujihusisha na unywaji wa pombe.

 Wakati kukiwa na maelekezo hayo, inaelezwa kuwa baadhi ya watoto wakiwamo wanafunzi, wanakunywa  pombe, kitendo ambacho si sahihi kwa maendeleo na ustawi wao kiafya, kisaikolojia na kielimu.

 Kutokana na mazingira hayo, mkoa wa Kilimanjaro, umeruhusu kuanzishwa kampeni shuleni  kuhamasisha vita dhidi ya ulevi wa pombe unaofanywa na baadhi ya wanafunzi wa shule za sekondari.

 Kuanzishwa kampeni hiyo, kunaelezwa na mkuu wa mkoa huo Nurdin Babu kuwa kunatokana na utafiti uliofanywa mwaka 2019 katika mikoa ya Mwanza na Kilimanjaro na kubaini matumizi ya pombe kwa wanafunzi wa shule za sekondari wenye umri wa miaka 15 na zaidi.

 Bila kuwataja waliofanya utafiti, anasema, ulionyesha kuwa  kiwango hicho cha matumizi ya pombe kwa wasichana kilikuwa ni asilimia 12.9 mkoani Mwanza na asilimia 63.9 kwa wavulana mkoani Kilimanjaro.

Pombe za kienyeji zinazonywewa Kilimanjaro ni pamoja na ndegelua inayotokana na miwa na mbege inayotengenzwa kwa kimea cha ulezi au mbeke.

Wakati Mwanza pombe mashuhuri za kienyeji ni komoni na gongo.

 Kwa mujibu wa mkuu huyo wa mkoa, Tanzania ni miongoni mwa nchi za Afrika ambako vijana wengi huanza matumizi ya pombe mapema katika umri mdogo, wakiwamo wa kuanzia miaka 15.

 Babu alikuwa akizindua kampeni ya kuhamasisha vita dhidi ya matumizi ya pombe kwa wanafunzi shuleni, na kwamba kupitia kampeni hiyo iliyopewa jina la SMASHED inayoendeshwa na kampuni moja ya bia.

 Kampeni hiyo ingesambaa nchi nzima ili kunusuru wanafunzi waweze kutimiza ndoto walizojiwekea katika elimu, kwani kunywa pombe kuna athari hasi kwa wanafunzi.

 Mojawapo athari hizo ni wanafunzi kujikuta wakiweka mbele kunywa pombe na kuacha masomo, mwisho wake ni kushindwa kutimiza ndoto zao walizojiwekea katika taaluma na maisha.

 Kwa kawaida ulevi hauanzi mara moja, bali mnywaji anaanza taratibu na mwishowe anajikuta anakuwa mlevi wa kupindukia. 

Hivyo, ni vyema wanafunzi waondolewe katika janga hilo mapema, kampeni hiyo ikisambaa  italinda vijana na kuwaepusha na unywaji ambao kama hawatauacha, wanaweza kuwa waraibu badala ya kujitegemea, kumudu maisha yao  na  kuwa msaada kwa familia zao.

 Wataalamu wa afya walishaweka wazi kuwa miili ya watoto na vijana huendelea kukua na kwamba kunywa pombe katika umri mdogo kunaweza kuingiliana na ukuaji wa kawaida wa ubongo na viungo.

 Vilevile, wanaeleza kuwa inaweza pia kuathiri viungo muhimu na kusababisha matatizo ya kiafya baadaye maishani, hivyo, kutumia pombe kunaiweka miili yao katika hatari.

 Aidha, wanaeleza kuwa kunywa katika umri mdogo, hasa kunywa na kulewa kupita kiasi, kunaweza kusababisha shida za kisaikolojia na kunaweza kuongeza tabia mbaya ya uraibu wa pombe baadaye maishani.

 Lakini pia umefika wakati sasa kuzuia matangazo yanayohamasisha unywaji wa pombe au nyimbo zinazohamasisha unywaji  kwani inawezekana baadhi ya wanafunzi wamejikita katika unywaji wa pombe kutokana na hamasa hiyo.

Nyimbo na matangazo ya ulevi na uvutaji sigara huwasisimua vijana na kuwaweka katika mazingira ya kupenda kutumia vileo hivyo, ni vyema yakakomeshwa ili kuokoa taifa.

 Kwa mfano, kuna tangazo linaloonyesha bia huku kukiwa na maandishi yasomekayo 'fahari yetu', na pia kuna wimbo wa msaani unaosema; 'asikwambie mtu bia tamu'.

 Ni kupitia hamasa hizo, pengine  baadhi ya watoto wakiwamo wanafunzi, wamejikuta wakijiingiza katika unywaji wa pombe, ambao kama wasipozuiwa, wanaweza kuwa walevi wakubwa wa baadaye.