Majaji lindeni mchezo wa ngumi, si kuwabeba mabondia

By Adam Fungamwango , Nipashe
Published at 11:23 AM Mar 04 2024
Glavu za ndondi.
PICHA: MTANDAO
Glavu za ndondi.

UKIPITA mitaani utakuta kila mmoja akiwa hakubaliani na sare aliyoipata bondia Mtanzania, Selemani Kidunda.

Bora ningelala kuliko hiki nilichokiona. Mimi ni Mtanzania na nilipenda bondia wetu ashinde, lakini kwa hiki nilichoshuhudia, bondia wetu amepoteza pambano, na wala si sare, imeniuma sana, mtoto wa watu wamemnyima ushindi," alisikika akisema bibi huyo akiwaambia wajukuu zake.

Hata watoto nao ukiwauliza wanakwambia, bondia Mtanzania alikuwa amepoteza pambano na hawaelewi kwa nini imekuwa sare.

Watanzania pamoja na uzalendo wao wote, lakini hili wameonekana kutokubaliana nalo, na inaonekana kama unaongea na raia wa Afrika Kusini.

Nilimsikia mama mmoja mtu mzima akisema anajuta kwa nini amepoteza usingizi wake.

"Bora ningelala kuliko hiki nilichokiona. Mimi ni Mtanzania na nilipenda bondia wetu ashinde, lakini kwa hiki nilichoshuhudia, bondia wetu amepoteza pambano, na wala si sare, imeniuma sana, mtoto wa watu wamemnyima ushindi," alisikika akisema bibi huyo akiwaambia wajukuu zake.

Kila unapopita asubuhi ile ya Machi 2, utasikia watu wanalalamikia juu ya maamuzi ya pambano lililopigwa usiku wa Machi Mosi, mwaka huu, Masaki jijini Dar es Salaam kati yake dhidi ya Asemahle Wellem kutoka Afrika Kusini.

Lilikuwa ni pambano la uzito wa Super Walter lililokuwa na raundi 12 ambazo ziliisha zote.

Kilichotokea hapo ni kwamba Watanzania hawakuridhika na maamuzi. Licha ya watu kulalamika kila unapokata kona, kwenye mitandao ya kijamii ndiyo kabisa.

Ukisoma maoni ya watu utaona kabisa kuwa kuna kitu hakiko sawa kwenye pambano hilo na itabidi sasa majaji wabadilishe mitazamo yao.

Ni kweli ndondi ina ufundi wake katika upiganaji, ambapo kuna maeneo yana pointi nyingi kuliko zingine, unaweza kuona bondia kapiga ngumu nyingi, lakini hazina alama nyingi, lakini chache zikipigwa mwingine akipiga chache zenye alama nyingi, lakini kuna vitu vingine vinaonekana kwa macho, tena na watu wengi.

Kama ilikuwa ni kupiga kura kwa watazamaji na si pointi za majaji, bondia Wellem angeibuka na ushindi kutokana na umahiri wake aliokuwa akiuonyesha ulingoni na jinsi alivyokuwa akitawala, pia staili yake ya upiganaji na jinsi alivyokuwa akirusha ngumi zake kwa ufundi mkubwa.

Na wala haikushangaza kuona mwisho wa pambano hilo, Kidunda akiwa amechakaa uso, huku mwenzake akiwa kama ametoka disko.

Wengine wakaenda mbali zaidi na kusema kama Kidunda ndiyo angekuwa Wellem, basi ushindi ungeenda kwake.

Angalau malalamiko mitaani na kwenye mitandao ya kijamii yalipunguzwa na mechi ya Ligi ya Mabingwa Afrika kati ya Simba dhidi ya Jwaneng Galaxy, ambapo Watanzania na mashabiki wa michezo waligeukia huko na kuachana na matokeo ya ndondi ambayo yamepigwa na Watanzania wengi.

Kinachoonyesha huenda Watanzania wakawa wako karibu na ukweli, ni kwamba walikuwa nyuma na kuumuunga mkono bondia wao kwa namna ya uzalendo, lakini sare hiyo hawakukubaliana nayo.

Niliona hivi karibuni baadhi ya mashabiki wakipinga ushindi na baadhi ya mabondia wa Kitanzania wanapigana na mabondia kutoka nje hapa nchini.

Na kwa siku zinavyoendelea inaonekana wanakosa imani nao, wengine wakienda mbali zaidi wakitaka majaji kutoka nje ya nchi ndiyo wafanye kazi hiyo.

Binafsi, naona kama hicho ni kengele cha hatari kwa mchezo wa ngumi ambao kwa sasa unashika nafasi ya pili kwa umaarufu na kupendwa nchini.

Kutokana na kurejea kwa wadhamini na kuanza kuonyeshwa kwenye televisheni, mchezo wa ngumi umerudi kwenye chati kama ilivyokuwa zamani, hivyo kinachotakiwa si kuwalinda mabondia wa Tanzania, lakini si kuwasaidia kushinda.

Kwa sasa unaangalia na kufuatiliwa na watu wa rika zote, wengine wanakesha, sasa kama wameanza kuguna na unaanza kukosa mvuto na anayeshinda hapewi haki yake, wataanza kuudharau na kuendelea kufuatilia vitu vingine.

Kama hata kinamama wanaacha tamthilia na kufuatilia ngumi, halafu mwisho wa siku maamuzi hakubaliani nayo, kesho yake hawatofuatilia tena.

Kama mchezo huu utapoteza tena mashabiki basi ni majaji watakuwa wamefanya hivyo. Binafsi naomba waendelee kuulinda mchezo kwa kutoa maamuzi ya haki ili uendelee kupendwa na si kuwafurahisha wachache kwa kuwapa kisichostahili mabondia wa Tanzania.

Tuwaache washinde kwa uwezo wao na nina uhakika wanapopigwa ndipo wanakwenda kujipanga ili kushinda pambano lijalo. Wanapopata ushindi au sare isiyoeleweka wanabweteka.