BAADA ya kuanza kazi na ushindi, Kocha Mkuu mpya wa Singida Fountain Gate, Jamhuri Kihwelo 'Julio', amesema kilichokuwa kinaiathiri timu hiyo kiasi cha kushindwa kupata ushindi kwenye mechi nane mfululizo ni wachezaji wake kutokuwa na utimamu wa mwili.
Akizungumza baada ya kumalizika kwa mechi ya Ligi Kuu Tanzania Bara kati ya timu hiyo na Namungo, Uwanja wa CCM Kirumba jijini Mwanza na timu yake kushinda bao 1-0, Julio amesema baada ya kuingia tu kwenye timu hiyo, kitu alichobaini ni ukosefu wa fiziki kwa wachezaji ndiyo ulikuwa ukiwatafuna.
"Nimegundua timu hii ilikuwa na matatizo kadhaa, kikubwa hawako vizuri kwenye utimamu wa mwili, lakini kutokana na maelekezo niliyowapa wameweza kutekeleza na kupata ushindi.
"Leo tumeshinda, kilichobaki sasa ni kuwaandaa vizuri kwa sababu nitakuwa nao kwa mwezi mzima kwenye mazoezi wakati ligi imesimama, nafikiri ile Singida ya mwanzo itarudi sasa hivi," amesema Julio, akiiongoza timu hiyo kushinda kwa mara ya kwanza baada ya mechi tisa.
Awali timu hiyo ilicheza mechi nane bila kupata ushindi, ambapo mara ya mwisho kushinda ilikuwa ni Novemba 27, mwaka jana, ilipoifunga Coastal Union mabao 2-1 nyumbani, na baada ya hapo ikicheza mechi nane, ikipoteza tano na sare tatu.
Ilianza kwa sare ya mabao 2-2 dhidi ya JKT Tanzania, na sare nyingine na mechi inayofuata ikatoka suluhu dhidi ya KMC, kabla ya kwenda kukutana na kipigo cha bao 1-0, Uwanja wa Nyankumbu, Geita, dhidi ya Geita Gold.
Ikafungwa bao 1-0 dhidi ya Kagera Sugar, kabla ya kupata kipigo kingine cha mabao 3-1 dhidi ya Prisons na kwenda kutoa sare ya bao 1-1, dhidi ya Taboara United.
Baada ya hapo ikachapwa bao 1-0 dhidi ya Azam kabla ya kubamizwa mabao 2-0 dhidi ya Mtibwa Sugar.
Kocha Mkuu wa Namungo, Mwinyi Zahera, kwa upande wake alilalamikia maamuzi, akidai wamelazimishwa kufungwa.
"Tumelazimishwa kufungwa, timu yangu imecheza vizuri sana kama kungekuwa na uchezeshaji mzuri wala tusingefungwa, hata kama tusingeshinda, lakini tusingepoteza," amesema.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED