WFP yasisitiza umuhimu kupunguza utapiamlo dira 2050

By Maulid Mmbaga , Nipashe
Published at 02:43 PM Jan 12 2025
Mkurugenzi wa Shirika la Chakula Duniani (WFP) nchini Tanzania, Ronald Tran Ba Huy.
Picha: Mpigapicha Wetu
Mkurugenzi wa Shirika la Chakula Duniani (WFP) nchini Tanzania, Ronald Tran Ba Huy.

MKURUGENZI wa Shirika la Chakula Duniani (WFP) nchini Tanzania, Ronald Tran Ba Huy, amesisitiza umuhimu wa sekta ya kilimo, kuweka ulinzi wa kijamii, na mikakati ya kupunguza utapiamlo kama maeneo muhimu ya kuimarishwa katika Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050.

Akizungumza jana katika mkutano wa ushirikiano na washirika wa maendeleo wa kuhakiki rasimu hiyo, uliofanyika mkoani Dar es Salaam, alieleza kuwa sekta ya kilimo ina mchango mkubwa katika ajira za vijana na ukuaji wa uchumi wa ndani na kikanda.

"Tanzania tayari ni kapu la chakula kwa ukanda huu, lakini inaweza kuwa kapu kubwa zaidi. WFP inanunua bidhaa nyingi za ndani kwa ajili ya shughuli zake za kikanda, na hivyo kuna fursa kubwa ya kukuza sekta hii," alisema Ronald.

Kuhusu mabadiliko ya tabianchi, alisisitiza haja ya kujumuisha miradi ya kukabiliana na maandalizi ya majanga kwenye sera za maendeleo. "Hatuongelei tu miundombinu mikubwa, bali pia miradi ya kijamii na maandalizi kwa ajili ya changamoto zinazotokana na tabianchi".

Ronald pia aligusia umuhimu wa kuimarisha mifumo ya hifadhi ya jamii ili iweze kukabiliana na majanga, akieleza kuwa mifumo hiyo inapaswa kuwa na uwezo wa kujibu changamoto za ghafla, ikiwa ni sehemu ya mikakati ya maendeleo.

Hata hivyo, moja ya changamoto kubwa aliyoitaja ni viwango vya juu vya utapiamlo miongoni mwa watoto, akibainisha kuwa hali hiyo inazuia watoto kufikia uwezo wao kamili.

"Tutafurahi kushirikiana nanyi kuhakikisha kuwa suala la kupunguza utapiamlo linapewa uzito katika dira hii," alisema Ronald.