NFRA: Tumejipanga endapo upungufu sukari utajitokeza

By Mwandishi Wetu , Nipashe
Published at 03:41 PM Feb 13 2025
Mkurugrnzi Mkuu wa Wakala wa Taifa wa Uhifadhi wa Chakula (NFRA), Dk Andrew Komba
Picha: Mtandao
Mkurugrnzi Mkuu wa Wakala wa Taifa wa Uhifadhi wa Chakula (NFRA), Dk Andrew Komba

MKURUGENZI Mkuu wa Wakala wa Taifa wa Uhifadhi wa Chakula (NFRA), Dk Andrew Komba, amesema mamlaka imejipanga kukabiliana na upungufu wa sukari nchini, endapo utajitokeza na serikali imeshatoa kibali kwa wakala kuagiza, kusambaza sukari.

Akizungumza na waandishi wa habari, jijini Dar es Salaam, Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka hiyo, Dk Komba, alisema NFRA imepewa  jukumu la ununuzi wa sukari nje, kwa ajili ya kutosheleza soko la ndani pale uhaba utakapojitokeza.

Amesema lengo ni kuwa na akiba ya kutosha, kwa kipindi cha miezi miwili kama sheria ya sukari inavyosema.

"Sheria ya sukari inasema kwamba, endapo NFRA itagundua kuna uhaba wa sukari itatoa sukari yake iliyoihifadhi na kuiingiza sokoni.

“Lakini pia endapo mojawapo ya kiwanda au viwanda vyote vikashindwa kuzalisha, basi NFRA itatoa sukari yake iliyoiagiza na kuiingiza sokoni,” alisisitiza Dk Komba.

Dk. Komba alibainisha kwamba Bunge, lilipitisha sheria hiyo na kuipa nguvu taasisi hiyo, kuwa na sukari ya kutosha muda wote na siyo kusubiri mpaka pale kunapokuwa na uhaba wa bidhaa hiyo muhimu.

“Malengo ya Serikali ya Rais Samia Suluhu Hassan, ni kuona Watanzaia wanapata mahitaji muhimu na kuhakikisha uwapo kwa akiba ya chakula cha kutosha, ikiwamo sukari kwa usalama wa nchi.

“Ndiyo maana baada ya kujengewa uwezo wa kutosha na serikali, NFRA imeweza kuwa na akiba ya kutosha ya chakula ikiwemo sukari katika kukabiliana na upungufu wowote unaoweza kujitokeza,” alisema.

Alisema kuwa serikali imeipa taasisi yake mamlaka ya ununuzi na kuhifadhi sukari, kutokana na changamoto ya uhaba wa bidhaa hiyo kujitokeza mara kwa mara, miaka iliyopita na kuleta usumbufu kwa wananchi.

“Tumelipokea jukumu hili, kwa mikono miwili na utekelezaji wake unakwenda vizuri,” alisema Dk. Komba.

Mwaka jana, wakati Rais Dkt Samia  alipokuwa ziarani mkoani Morogoro, alifungua kiwanda cha sukari cha Mkulanzi ambacho kinamilikiwa na Mfuko wa Hifadhi ya Jamii (NSSF), kwa kushirikiana na Jeshi la Magereza, akisema kuwa lengo la uwapo wa kiwanda hicho, ni kuongeza kiasi cha uzalishaji sukari hapa nchini.

Viwanda vinavyozalisha sukari hapa nchini ni pamoja na Kilombero, Mtibwa, Bagamoyo, TPC Limited na  kiwanda cha serikali cha Mkulazi .