Balozi Uingereza azuru IPP Media, aahidi biashara na uwekezaji zaidi

By Jenifer Gilla , Nipashe
Published at 12:02 PM Feb 13 2025
Mhariri wa Habari wa gazeti Nipashe na Meneja wa Kitengo cha Dijitali cha TGL, Salome Kitomari (kushoto), akifafanua jambo kwa Balozi Marianne Young kuhusu shughuli mbalimbali zinazofanywa na kitengo hicho. Kulia ni Naibu Meneja Mkuu wa TGL, Jackson Paul
Picha:Miraji Misala
Mhariri wa Habari wa gazeti Nipashe na Meneja wa Kitengo cha Dijitali cha TGL, Salome Kitomari (kushoto), akifafanua jambo kwa Balozi Marianne Young kuhusu shughuli mbalimbali zinazofanywa na kitengo hicho. Kulia ni Naibu Meneja Mkuu wa TGL, Jackson Paul

SERIKALI ya Uingereza imesema itaendeleza ushirikiano wa biashara, uwekezaji na kuunga mkono miradi ya maendeleo nchini ili kusaidia wananchi kuijiinua kiuchumi.

Balozi wa Uingereza nchini, Marianne Young, alisema hayo jana alipotembelea vyombo vya habari vya IPP kujionea vinavyoendesha shughuli za kuuhabarisha umma.

 Balozi Young alisisitiza kuwa licha ya changamoto inayopitia Tanzania kwa sasa kutokana na usitishwaji wa misaada ya maendeleo, ushirikiano kati ya Uingereza na Tanzania utaendelea kuwa  imara.

 Alisema nchi hiyo imejizatiti kuendelea kuisaidia katika misaada ya kibinadamu kama vile elimu, na afya, huku ikiendelea kupanua wigo katika sekta mpya kama vile mabadiliko ya tabianchi.

 Alisema  serikali ya Uingereza inaendelea kushirikiana na wafadhili wengine wa kimataifa ili kutathmini athari za mabadiliko ya misaada ya maendeleo kwa Tanzania  na kuhakikisha ushirikiano endelevu unaendelea kuimarika.

 “Tumejizatiti kikamilifu kuendelea na kazi ya maendeleo ya kimataifa na misaada ya kibinadamu hapa Tanzania. Ushirikiano huu siyo tu kati yetu na serikali ya Tanzania, bali pia unahusisha kanda nzima,” alisema Young.

 UHUSIANO KIDIPLOMASIA

 Pia alisema uhusiano wa kidiplomasia kati ya nchi hizo unaendelea kuimarika, kutoka utegemezi wa misaada ya kimaendeleo kwenda ushirikiano mpana unaojumuisha biashara, usalama na maendeleo.

 Alisema Uingereza inaendeleza dhamira yake ya kupanua fursa za kiuchumi kupitia Mpango wa Biashara kwa Nchi zinazoendelea (DCTS) unaotoa fursa kwa bidhaa za Tanzania kuingia kwenye soko la Uingereza bila ushuru au vikwazo vya kibiashara.

 “Tumezindua ushirikiano wa ustawi wa pamoja wenye malengo makubwa ya kuongeza biashara yetu kwa zaidi ya Pound milioni 100 katika miaka michache ijayo na kufungua uwekezaji wa pauni bilioni moja unaoungwa mkono na serikali ya Uingereza,” alisema.

 Alisema hivi karibuni, ujumbe kutoka Soko la Hisa la London ulitembelea Tanzania kuchunguza njia za kuongeza ushirikiano kati ya Soko la Hisa la Dar es Salaam na taasisi za kifedha za Uingereza hatua inayokusudia kuvutia wawekezaji wa kimataifa zaidi na kutoa fursa za kifedha kwa kampuni za Kitanzania.

 Pia aliipongeza nchi hiyo  kwa hatua kubwa inayopiga kiuchumi hadi kushiriki katika majukwaa makubwa duniani, akitaja ushiriki wa Rais Samia Suluhu Hassan katika Kikao cha G20 huko Rio kama ishara ya kuimarika kwa ushawishi wa Tanzania katika masuala ya kimataifa.

 TABIANCHI
Kwa kutambua changamoto kubwa zinazotokana na mabadiliko ya tabianchi, Marianne alisisitiza kuwa Uingereza itaendelea kusaidia Tanzania kutengeneza mikakati ya kuhimili athari zake.

 “Tunaongeza kasi ya mpango mkubwa wa kusaidia juhudi za kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi ili kukabiliana na changamoto kubwa za kimataifa na kufanikisha Malengo ya Maendeleo Endelevu, tunapaswa kufanya kazi kwa ushirikiano,” alisisitiza.

 Kuhusu uchaguzi mkuu, alisema  Uingereza kama jumuiya zingine za kimataifa, inafuatilia kwa makini hali ya kisiasa nchini hasa kuelekea uchaguzi mkuu wa Rais, Wabunge na Madiwani,  unaotarajiwa kufanyika Oktoba, mwaka huu.

 “Tumesikia Rais Samia akithibitisha tena dhamira yake kwa kanuni nne za maridhiano, ustahimilivu, mageuzi na ujenzi mpya. Hii ni ishara njema kwa mchakato wa kidemokrasia huru na wa haki.” alisema.

 Katika kuhakikisha wanawake nchini hawaachwi nyuma katika ushiriki kwenye siasa, Balozi Young alisema Uingereza ilianzisha programu mbalimbali za kuwasaidia si tu kushiriki bali pia kuhakikisha wanapata msaada wa kutosha mara wanapochaguliwa kushika nafasi za uongozi.

 “Tumekuwa na majadiliano na Spika wa Bunge, Dk. Tulia Ackson, kuhusu kuongeza ushiriki wa wanawake bungeni na kuhakikisha wanapata msaada mara baada ya kuchaguliwa,” alisema. 

Balozi Young alisema ni muhimu sana kuwapa wanawake nafasi kwenye siasa ili kuhakikisha kuwa kuna uwakilishi sawa wa nafasi za uongozi ili kupata wawakilishi wa kundi hilo katika ngazi za juu za kufanya uamuzi.