Bunge laingilia kati mikopo halmashauri, unyanyasaji vikundi

By Jenifer Gilla , Nipashe
Published at 02:52 PM Feb 13 2025
Naibu Spika wa Bunge, Mussa Azzan Zungu
Picha: Mtandao
Naibu Spika wa Bunge, Mussa Azzan Zungu

NAIBU Spika wa Bunge, Mussa Azzan Zungu, ameiagiza Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, (TAMISEMI), kufuatilia na kukemea tabia za baadhi ya wanaosimamia mikopo ya asilimia 10 ya halmashauri, kuwanyanyasa wanavikundi.

Zungu alisema hayo jana bungeni, akichangia hoja iliyotolewa na Mbunge wa Viti Maalum, Sylvia Gisula, aliyehoji; Je, lini Serikali itarejesha mikopo ya asilimia 10 iliyokuwa ikitolewa kwa vijana, wanawake na watu wenye ulemavu?

Alisema kuna malalamiko kutoka kwa wanavikundi wanaokwenda kukopa mikopo ya halmashauri kuwa, baadhi ya wasimamizi wa mikopo hiyo katika ngazi za  kata, halmashauri, maofisa maendeleo kutowatendea  haki.

Alisema Rais Samia Suluhu Hassan, ametoa fedha hizo kwa ajili ya kuwasaidia na kuwainua Watanzania hivyo ni muhimu zitolewe kwa usawa bila kubagua wengine.

“Embu jaribuni kulifuatilia hili suala na mtoe tahadhari kwa yeyoye atayehusika kuonea kikundi bila sababu maana hizi pesa ni za mama (Rais Samia Suluhu Hassan) kwa watoto wake (wananchi), ” alisema.

Naibu Waziri Ofisi ya Rais – Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), Zainab Katimba, aliziagiza kamati zilizoundwa, kusimamia mikopo hiyo kutimiza wajibu wao kuhakikisha vikundi vinavyoomba mkopo vinapatiwa kwa wakati.

Aliwaagiza pia viongozi husika kuanzia ngazi ya kata, halmashauri, wilaya na   mkoa kutimiza  wajibu wao ili fedha hizo  ziyanufashe makundi hayo na wananchi wapate mitaji ya kuendesha shughuli zao za kiuchumi.

Alisema kwa mujibu wa kanuni hizo, vikundi vinavyoomba mkopo vinapaswa kupewa mikopo ndani ya miezi miwili, baada ya kukamilisha taratibu zote kwa mujibu wa kanuni.

“Naomba nitumie nafasi hii kwa niaba ya Waziri wa Ofisi ya Rais TAMISEMI, kutoa msisitizo kwa kamati zote, zile ambazo zimeundwa za usimamzi wa mikopo hii ya asilimia 10 ya mapato ya ndani, watimize wajibu wao kwa mujibu wa kanuni,” alisema.

Alisema kwa mujibu wa kanuni zinazosimamia maboresho ya mikopo ya asilimia kumi ya halmashauri, kikundi kitapewa mkopo kama dhamana, lakini wanakikundi wanaruhusiwa kutumia mikopo hiyo katika miradi yao binafsi.

“Serikali inatambua kama kuna vijana ambao wanataka wafanye miradi yao binafsi na ndio maana kwenye kanuni kipengele hicho kimetolewa na mikopo ya kikundi, itakuwa kama dhamana lakini wanakikundi wanaweza kuweka utaratibu kila mwanakikundi akawa na mradi unaojitegemea,” alifafanua.

Alisema mikopo ya vikundi vya wanawake, vijana na watu wenye ulemavu inayotolewa kutokana na asilimia 10 ya mapato ya ndani ya halmashauri ilisitishwa na serikali Aprili 13, 2023, ili kupisha maandalizi ya utaratibu mpya wa utoaji wa mikopo hiyo.

Alisema baada ya mfumo mpya kukamilika Julai Mosi, mwaka jana, serikali ilitangaza mikopo hiyo kuanza kutolewa tena, kwa mujibu wa sheria na kanuni za utoaji na usimamizi wa mikopo hiyo.

Alisema Ofisi ya Rais – TAMISEMI, inaendelea kuzisimamia mamlaka za serikali za mitaa kuhakikisha zinatoa mikopo, kwa mujibu wa sheria ambapo tangu mikopo kurejeshwa hadi Desemba, 2024, halmashauri 64 zimetoa mikopo ya Sh.  bilioni 22.07 kati ya Sh. bilioni 27.76 zilizoombwa na vikundi 2,726 vya wanawake, vijana na watu wenye ulemavu.

Alisema kati ya fedha hizo Sh. billioni 21.88 zimetolewa kutokana na michango ya halmashauri ya asilimia 10 ya mapato ya ndani na Sh. milioni 194.3 ni mikopo iliyotokana na fedha za marejesho.