Watumishi wavumilivu kuishi vijijini kupewa motisha

By Augusta Njoji , Nipashe
Published at 02:59 PM Feb 13 2025
Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, Justin Nyamoga
Picha: Mtandao
Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, Justin Nyamoga

KAMATI ya Bunge ya Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, imebaini watumishi wa umma kukimbia maeneo ya vijijini kutokana na kuwapo na mazingira ngumu ya kufanyia kazi.

Kufuatia hali hiyo, Bunge limeazimia kuishauri serikali kuboresha mazingira ya kufanyia kazi katika halmashauri nchini, hasa vijijini na kutoa motisha kwa walimu na watumishi wa kada ya afya.

Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Justin Nyamoga, akiwasilisha jana bungeni, taarifa ya mwaka ya utekelezaji wa majukumu ya kamati, alisema kwa katika uchambuzi mbalimbali kuhusu msawazo wa walimu nchini, kamati imebaini kuwa maeneo mengi ya vijijini yana hali ngumu sana ya maisha.

“Kutokana na ugumu wa maisha vijijini, hasa huduma za maji, umeme na barabara (usafiri) watumishi wengi wa sekta ya elimu na afya, huhama ama kuhangaikia kuhama kutoka vijijini kwenda mijini.”

 “Kwa ujumla mazingira yasiyovutia yamekuwa yakisababisa watumishi wengi wa kada za afya na elimu katika halmashauri, huhama kwa kasi ama hata kuacha kazi wakati mwingine,” alisema.

Alisema kamati inashauri serikali kuboresha mazingira ya kufanyia kazi katika halmashauri nchini, hasa vijijini na Bunge linaazimia serikali iboreshe mazingira kwa kutoa kipaumbele katika uboreshaji wa huduma za watumishi katika maeneo hayo.

KILIO TARURA

Kuhusu Wakala wa Barabara Mijini na Vijijini (TARURA), alisema Bunge lilipitisha bajeti ya Sh. bilioni 886.3, kwa ajili ya kutekeleza shughuli zake kwa mwaka 2024/25.

Alisema matajio hadi Desemba, 2025 TARURA iwe imekwishakupelekewa Sh. bilioni 443.15 na hadi kufikia Desemba, 2024 ilipokea Sh. bilioni 92.49 sawa na asilimia 20 tu ya matarajio.

“Kamati inasikitika kwa uwasilishaji mdogo wa fedha kwa TARURA, ambao haukufikia hata nusu ya matarajio kwa kipindi cha Julai hadi Desemba, 2024,” alisema.

Hata hivyo, alisema taarifa ya TARURA inaonesha tathmini iliyofanyika juu ya uharibifu wa miundombinu uliosababishwa na mvua za El Nino na Kimbunga Hidaya, ilihitaji Sh. bilioni 883, ili kuirejesha miundombinu hiyo lakini kamati imebaini kuwa serikali imetenga na kutoa Sh. bilioni 83.

Alisema kamati ilifahamishwa TARURA imetekeleza jukumu lake la urejeshaji wa miundombinu iliyoharikiwa na mvua za El Nino pamoja na Kimbunga Hidaya, kwa asilimia 28 tu, hivyo asilimia 72 bado hazijatengenezwa.

Nyamoga alisema hali hiyo inasababishwa kutokana na Serikali kutokutoa fedha zinazotosha kwa ajili ya ukarabati huo na Kamati inashauri serikali kutoa fedha hizo za dharura kwa wakat, ili kuondoa uwezekano wa barabara hizo kuharibiwa zaidi na hivyo kuweza kuisababishia serikali kutumia fedha nyingi zaidi.

 “Bunge linaazimia kwamba, Halmashauri za Wilaya nchini, ambazo zinatakiwa kuchangia asilimia 10 kwa kutumia mapato yao ya ndani, waisaidiane na TARURA ili kurejesha barabara zilizoharibiwa na mvua nchin,” alisema.

Alisema upelekaji wa fedha kwenda TARURA unasuasua hata kama fedha hizo zinatengwa na kutokupeleka kwa wakati, kunaendelea kuifanya miundombinu kuharibika zaidi na kuleta usumbufu kwa wananchi.

“Bunge linaazimia kwamba, fedha zote zinazotengwa kwenye bajeti ya TARURA ziende kama zilizvyotengwa na kwa wakati,”alisema.

Katika hatua nyingine, Mwenyekiti Nyamoga alisema ofisi nyingi za wabunge majimboni hazina vitendea kazi na kunasababisha wabunge kushindwa kutekeleza majukumu yao ya kuwaletea maendeleo wananchi wao.

Alisema Bunge linaazimia serikali itenge bajeti, kwa ajili ya kununua vitendea kazi vya ofisi za waheshimiwa wabunge zisizo na vitendea kazi.

FIDIA ZA BRT ZILIPWE

Alisema Bunge linaazimia kwamba serikali iharakishe kulipa fidia katika maeneo yote yanayotakiwa kujengwa miundombinu ya Mradi wa Mabasi Yaendayo Haraka Dar es salaam (BRT), ambazo hazijalipwa, ili miradi hiyo ijengwe kwa wakati.

Pia, alisema Bunge linaazimia kwamba, serikali itatue mgogoro huo haraka, ili kuiwezesha DART kutekeleza majukumu yake kwa ufanisi.

WALICHOSEMA MAWAZIRI

Waziri wa Fedha, Dk. Mwigulu Nchemba, alisema bajeti ya serikali imeathirika mwaka jana na mwaka huu na imekuwa ikihakikisha hakuna shughuli za maendeleo zinazokwama.

Alisema mwaka jana, serikali ilikabiliwa na uharibifu mkubwa wa miundombinu ya barabara chini ya TARURA na TANROADS, hali iliyoathiri mtitiriko wa fedha.

Pia, alisema mwaka jana, barabara nyingi ziliharibuka kutokana na hali ya hewa, mgao wa umeme na kuna wakati walihitajika kuchagua kati ya kukodi mitambo au kuharakisha ukamilishaji wa Bwawa la Umeme la Mwalimu Nyerere (JNHPP).

“Kuna kipindi serikali ilikuwa inalipa zaidi ya Sh. bilioni 400 kwa mwezi, ili kuhakikisha mradi wa Bwawa la Nyerere, unakamilika haraka, hata hivyo baada ya mradi huu kukamilika, kasi ya utekelezaji miradi mingine ya maendeleo imerejea,” alisema.

Naye, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI, Mohamed Mchengerwa, aliagiza Wakuu wa Mikoa, Wilaya na Wakurugenzi wa Halmashauri, kupanga ratiba ya uzinduzi wa miradi mbalimbali, iliyosalia kwa kushirikisha wabunge.

USAILI WA WALIMU

Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Prof.Adolf Mkenda, alisema kasi ya kuajiri walimu imeongezeka, ili kuendana na mabadiliko ya sera na mitaala, huku akifafanua kuhusu usaili wa ajira za walimu na kwamba ni jambo la kawaida katika kutafuta walimu bora.

“Mageuzi ya walimu yanahitaji tuwe na walimu bora, nitoe wito kwa walimu ambao bado wapo mtaani waendelee kujiendeleza, kwa kuwa ajira zitakapotangazwa na kufanyiwa usaili, kwa mfano mwalimu wa kiingereza tukakuta huwezi kuzungumza kiingereza hatuwezi kukusaili,” alisema.