KLABU ya Yanga imesema kuwa itawatangaza wachezaji wake iliyowasajili kipindi hiki cha dirisha dogo, itakaporejea nchini kutoka Mauritania ambako jana usiku ilikuwa na kibarua cha mchezo wa Ligi ya Mabingwa Afrika hatua ya makundi dhidi ya, Al Hilal Omdurman ya Sudan uliopigwa nchini Mauritania.
Ofisa Habari wa Klabu hiyo, Ali Kamwe, alisema mipango yote ya usajili wa wachezaji wapya imekwenda vema na watawatangaza wakirejea nchini.
Klabu hiyo inahusishwa kumsajili winga Jonathan Ikangalombo, akitokea AS Vita Club ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, ikiwa pia imemsajili, Israel Mwenda, pamoja na wengine ambao itawatangaza.
Kamwe alisema watakaporejea nchini kila kitu kitawekwa wazi na kuwaumbua wote ambao wanadai Yanga haiwezi kusajili mchezaji yeyote kwa sababu wanadaiwa.
"Wanasema Mwenda hawezi kucheza kwa sababu tunadaiwa, wakati anatakiwa apambane mwenyewe kuwania nafasi kwani eneo analocheza amekuta watu wanapiga kweli kweli, atacheza, lakini ni mpaka apambane," alisema.
Ikangalombo, alikuwapo jukwaani katika mchezo wa Ligi ya Mabingwa Afrika uliopigwa, Januari 4, mwaka huu, kati ya Yanga na TP Mazembe.
Ingawa Kamwe hajaongea lolote kuhusu mchezaji huyo, lakini ni mmoja wa wachezaji wanaotarajiwa kutambulishwa.
"Mmoja wa wachezaji tutakayemtambulisha anakimbia kama swala, na wengine wapo kutoka hapa hapa nyumbani tunawatambulisha," alisema.
Desemba mwaka jana, FIFA ilitoa taarifa ya kuthibitisha kuwa Klabu ya Bechem United ya Ghana imeshinda kesi dhidi ya mabingwa wa Ligi Kuu Tanzania, Yanga SC, kwa kushindwa kulipa dola 80,000 za Marekani kama ada ya usajili wa Augustine Okrah.
Kwa mujibu wa barua hiyo, FIFA ikaipiga marufuku kufanya usajili hadi itakapolipa kiasi hicho. Aidha, Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), nalo liliagizwa kuweka marufuku ya usajili wa ndani kwa klabu hiyo.
Kabla ya hapo, aliyekuwa mchezaji wa timu hiyo, Okrah ashinda kesi yake dhidi ya klabu hiyo, ambapo ilifungiwa hadi watakapomlipa
Ilitakiwa kumlipa Dola za Kimarekani, 24,400 (zaidi ya milioni 66). Pamoja na faini ya FIFA Dola za Kimarekani, 3,000 (zaidi ya milioni nane).
Akizungumzia hilo, Kamwe alisema hakuna kitakachoizuia Yanga isisajili kwani inajua inachokifanya.
"Kila siku watu anasema tuna madeni, lakini tunasajili na watu wanachezaji, sisi tunajua tunachokifanya wala hatuna wasiwasi wote, tutakaowatangaza watacheza," alisema Kamwe.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED