KLABU ya Yanga imesema haitouza au kuruhusu mchezaji yeyote tegemeo aondoke kwenye kikosi chake mpaka hapo watakapotimiza lengo lao la kutinga hatua ya nusu fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika, kufika fainali au kuutwaa ubingwa wenyewe.
Akizungumza jijini Dar es Salaam, Ofisa Habari wa klabu hiyo, Ali Kamwe, alisema kinachofanyika kwa sasa ni kutaka kuidhoofisha Yanga kama ambavyo klabu mbalimbali kubwa barani Afrika zimekuwa zikifanya kwa klabu ndogo hasa za Tanzania wanapoona zimekuwa hatari katika michuano ya kimataifa.
Alisema hayo kutokana na kile kilichoonekana klabu hiyo kumzuia straika wao, Clement Mzize, ambaye amekuwa akihitajika na klabu mbalimbali.
Klabu za Kaizer Chiefs ya Afrika Kusini, Wydad Casablanca ya Morocco, Aalborg BK ya Denmark na Crawley Town FC inayocheza Ligi Daraja la Pili Uingereza, zinadaiwa zimepiga hodi Yanga kutaka huduma za mchezaji huyo, lakini hazijajibiwa.
Taarifa zinaeleza Wydad ndiyo imekuwa ikimhitaji zaidi, kwani imepiga hodi mara tatu na mara zote hizo imekuwa ikizidisha dau la uhamisho, lakini Yanga imekuwa kimya.
"Jambo hili ngoja nilitolee ufafanuzi, miaka ya nyuma ilionekana wachezaji wazuri kutoka nje hawawezi kucheza ligi yetu ya Tanzania, na ikitokea kwa uchache wao wakishakuwa na uwezo mkubwa, klabu zenye fedha zilikuwa zinakuja kutuchukulia wachezaji na kutudhoofisha, zimekuwa zikiturudisha nyuma katika michuano ya kimataifa, yaani mnafanya vema, wakazoa wale wazuri tegemezi mnaanza upya, inachukua tena misimu miwili au mitatu kukaa sawa.
"Sasa hivi klabu za Tanzania zinaweza kuleta wachezaji wazuri wakacheza Ligi Kuu, na pia sasa zina uchumi mzuri wa kuwazuia na kuwabakisha wachezaji bora, kwa hiyo si Mzize tu, mchezaji yeyote yule tegemeo Yanga haondoki mpaka azma yetu ya kutwaa ubingwa wa Afrika itakapotimia," alisema Kamwe.
Alisema mashabiki wa soka wasilichukulie suala hili upande wa hasi tu kuwa klabu yao ikatakaa kuuza au kuruhusu wachezaji wake, lakini pia wachukue upande wa chanya kwani una faida kubwa, timu yoyote inayotaka kufanya vema katika michezo ya kimataifa haipaswi kuondoa wachezaji wake bora, vinginevyo haitofika popote na kila mwaka itakuwa inashiriki badala ya kushindana.
Kamwe, pia amethibitisha klabu hiyo kuachana na winga wao raia wa Afrika Kusini, Mahlatse 'Skudu' Makudubela.
"Ni sahihi, mazungumzo yetu na Skudu yamefikia tamati, kwa sasa si tena mchezaji wa Yanga, tunamtakiwa kila lakheri," alisema.
Mchezaji huyo alisajiliwa kwa mbwembwe akitokea Marumo Galants ya Afrika Kusini, lakini hakucheza kwa mafanikio.
Wakati huo huo, kikosi cha Yanga kiliondoka jijini Dar es Salaam kwa mafungu juzi na jana kwa ndege, kuelekea mkoani Kagera kwa ajili ya mchezo wa raundi ya kwanza ya Ligi Kuu Tanzania Bara, dhidi ya Kagera Sugar, unaotarajiwa kuchezwa kesho katika Uwanja wa Kaitaba, Bukoba.
© 2024 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED