UCHAGUZI SERIKALI ZA MITAA: Majaliwa awataka viongozi vyama vya siasa kukemea uvunjifu wa amani

By Mwandishi Wetu , Nipashe
Published at 12:15 PM Nov 11 2024

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa.
Picha: Mtandao
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa.

WAZIRI Mkuu, Kassim Majaliwa, ametoa wito kwa viongozi wa vyama vya siasa vitakavyoshiriki katika Uchaguzi wa Serikali za Mitaa, kuwa vinara katika kulinda amani na kukemea viashiria vyote vya uvunjifu wa amani.

"Hamasisheni wanachama wenu kushiriki katika uchaguzi huo huku wakizingatia kudumisha amani iliyoko. Wananchi wote waliojiandikisha katika orodha ya wapigakura wa Uchaguzi wa Mamlaka za Serikali za Mitaa, wajitokeze kwa wingi kupiga kura katika vituo vyao siku ya Jumatano tarehe 27 Novemba 2024. Siku hiyo itakuwa ya mapumziko maalumu kwa ajili ya uchaguzi huo," ameelekeza.

Ni wito aliotoa jana alipomwakilisha Rais Samia Suluhu Hassan katika Mkutano Mkuu na Kongamano la Umuhimu wa Amani kuelekea Uchaguzi wa Serikali za Mitaa, jijini Dar es Salaam. 

"Mheshimiwa Rais Dk. Samia amewasihi Watanzania na viongozi wa dini kuendelea kuitangaza amani ndani na nje," Waziri Mkuu Majaliwa alisema.

Katika kongamano hilo, ambalo linaratibiwa na Jumuiya ya Waislamu wa Madhehebu ya Shia Tanzania, Majaliwa alitumia fursa hiyo kuwasisitiza viongozi hao kuhamasisha wanachama wao kushiriki katika uchaguzi huo huku wakizingatia suala la kudumisha amani kwa muhimu mkubwa.

Majaliwa alisisitiza kwamba kila mtanzania mwenye sifa ajitokeze kupiga kura ili kuwachagua viongozi ambao ni mwenyekiti wa kijiji, mwenyekiti wa mtaa, mwenyekiti wa kitongoji na wajumbe wa serikali za vijiji na kamati za mitaa. 

"Ikumbukwe kuwa kupiga kura ni wajibu na haki ya kikatiba ya kila mtanzania," Majaliwa alisema katika kipindi ambacho kuna malalamiko ya vyama vya upinzani kutotendwa haki katika uteuzi wa wagombea katika maeneo mbalimbali nchini.

Waziri Mkuu aliongeza kuwa serikali inatambua, inaheshimu na kuthamini kazi kubwa inayofanywa na madhehebu ya dini pamoja na taasisi zote, ambapo licha ya kutoa mafundisho ya kiroho, taasisi za dini zimekuwa zinaunga mkono jitihada mbalimbali za serikali katika kutoa huduma za kijamii kwa wananchi.

Mwenyekiti wa Jumuiya ya Maridhiano Tanzania, Alhad Mussa Salum alipongeza Jumuiya ya Waislam wa Shia Tanzania kwa harakati zake za kuhakikisha amani na utulivu wa Tanzania unaendelea kukua. 

"Mimi ni shuhuda mzuri wa harakati za Shia wanazofanya ili kuhakikisha amani na usalama wa Tanzania unaendelea kuimarika," alisema.