Matukio 1,800 ya wanyamapori yadhibitiwa

By Grace Gurisha , Nipashe
Published at 11:58 AM Nov 11 2024
Ofisa Wanyamapori Mkuu wa Wizara ya Maliasili na Utalii, Antonia Raphael, akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam kuhusu mikakati ya Serikali ya kutatua migongano kati ya binadamu na wanyamapori katika Ukanda wa Ruvuma.
Picha: Grace Gurisha
Ofisa Wanyamapori Mkuu wa Wizara ya Maliasili na Utalii, Antonia Raphael, akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam kuhusu mikakati ya Serikali ya kutatua migongano kati ya binadamu na wanyamapori katika Ukanda wa Ruvuma.

MATUKIO 1,806 yamedhibitiwa Ukanda wa Ruvuma kupitia doria za udhibiti wa wanyamapori wakali na waharibifu katika kipindi cha kuanzia 2023/24 hadi 2024/25 zinazofanywa na Wizara ya Maliasili na Utalii.

Doria maalumu za udhibiti wa mifumo hifadhini katika kipindi hicho zilikuwa na jumla ya mifugo 2,152 iliyokamatwa katika maeneo ya hifadhi kwenye ukanda huo na hatua za kisheria zilichukuliwa.

Hayo yalisemwa mwisho wa wiki jijini Dar es Salaam na Ofisa Wanyamapori Mkuu kutoka Wizara ya Maliasili na Utalii, Antonia Raphael wakati akiwaeleza waandishi wa habari mikakati ya serikali katika utekelezaji mradi wa kutatua migongano baina ya binadamu na wanyamapori katika Ukanda wa Ruvuma.

Alisema mradi huo ni ushirikiano kati ya Serikali ya Tanzania na Ujerumani, waandishi wa habari wa Chama cha Waandishi wa Habari za Mazingira Tanzania (JET) wakishiriki katika mradi huo.

Alisema mikakati ya serikali inajumuisha kuchimba mabwawa 30 katika Hifadhi za Taifa za Serengeti (5), Nyerere (2), Saadani (2), Mikumi (2), Tarangire (2) na Mkomazi (3) na Pori la Akiba la Selous.

"Hatua iliyofikiwa, mabwawa saba yamechimbwa Hifadhi ya Nyerere (1), Mkomazi (1), Tarangire (1), Mikumi (1) na Serengeti (2) na Pori la Akiba Swagaswaga (1)," alisema Raphael. 

Mkurugenzi Msaidizi wa wizara hiyo, Dk. Fortunata Msofe, alisema jumla ya Sh. bilioni 45.1 zimetengwa kwa ajili ya kutekeleza mipango na mikakati mbalimbali ya kukabiliana na changamoto ya wanyamapori wakali na waharibifu mwaka 2024/25 nchi nzima.

Mwenyekiti wa JET, Dk. Ellen Otaru alisema waandishi wa habari wanatakiwa kuandika habari ambazo zitasaidia jamii na si sitakazowatisha, hasa katika suala la mgongano wa binadamu na wanyamapori kwa sababu imejikita katika wanyama.

"Habari zenu mziandike kwa stahili ya hadithi si za kuwatisha wananchi, utaona tembo kaua mtu, lakini kuna namna unaweza ukaandika ikawaondoa hofu," alisema Dk. Otaru.