KATIBU wa Itikadi, Uenezi na Mafunzo, wa Chama cha Mapinduzi (CCM) Amos Makalla, amewaomba wanachama katika maeneo ambayo wagombea wake wamewekewa mapingamizi, kuwa watulivu kwakuwa wanaamini haki itatendeka kwa vyama vyote.
Makalla ameyasema hayo leo wakati akizungumza na viongozi na wanachama wa CCM Wilaya ya Mkuranga mkoani Pwani, ambako amesisitiza kuwa CCM itaibuka na ushindi wa haki katika uchaguzi wa serikali za mitaa, vijiji na vitongoji unaotarajiwa kufanyika Novemba 27 mwaka huu.
“Niwaombe wana CCM, tupo katika hatua za mapingamizi. Sasa hivi kinachoendelea mitandaoni ni malalamiko ya vyama vya upinzani kuonyesha kama vile pekee ndiyo waliowekewa mapingamizi.
“Wanafanya hadaa, upotoshaji wa takwimu feki na kujisahaulisha kwamba hata wagombea wa CCM wamewekewa mapingamizi. Juzi nilisema tunaamini TAMISEMI itatenda haki kwa vyama vyote kuhakikisha uchaguzi unakuwa huru na haki na atakayeshinda atangazwe kwa haki.
“Kwa hesabu zetu na wagombea tuliowaweka, tunaamini CCM tutashinda kwa haki. Kwa hiyo rufaa zinaendelea, baada ya uteuzi wa wagombea CCM kitatoa taarifa baadaye,” amesema Makalla.
Ameongeza kwa kukemea tabia hiyo ya baadhi ya vyama vya upinzani kupotosha umma kwamba wagombea wa vyama hivyo pekee, ndiyo wamewekewa mapingamizi, wakati sio kweli.
Amesema kuwa vyama vyote, kikiwemo CCM, ambavyo wagombea wake wamewekewa mapingamizi ya kuteuliwa, vinaendelea kukata rufaa, kwa mujibu wa kanuni za uchaguzi wa serikali za mitaa.
© 2024 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED