Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) wilayani Kahama, mkoani Shinyanga, imebaini baadhi ya viongozi wa vyama vya siasa kutoa rushwa kwa wagombea ili wajiondoe na kuruhusu wagombea wao kupita bila kupingwa.Hali hiyo imetajwa kusababisha wananchi kupata viongozi wasiokuwa waadilifu.
Akizungumza na waandishi wa habari leo Novemba 11,2024, Mkuu wa TAKUKURU Kahama, Abdallah Urari, ameeleza kwamba uchunguzi wao umebaini baadhi ya viongozi wa vyama vya siasa wanawashawishi wagombea kwa kutoa rushwa ili wasirejeshe fomu au kujaza fomu vibaya na hatimaye kuenguliwa. Urari amesisitiza kuwa tabia hiyo ni kinyume na maadili ya uchaguzi na inalenga kuvuruga mchakato wa uchaguzi.
Urari ameongeza kuwa vitendo hivyo vinaathiri maendeleo ya wananchi, kwani viongozi wanaochaguliwa kwa njia hizo hawana uadilifu na wanaweza kujinufaisha binafsi kutokana na rushwa waliyotoa kipindi cha uchaguzi. TAKUKURU imeahidi kuchukua hatua za kisheria dhidi ya watakaobainika kuhusika na vitendo hivyo.
Aidha, Urari amefafanua kwamba baadhi ya viongozi wanaunda makundi maalum ya vijana, maarufu kama “machawa,” wanaotumiwa kugawa rushwa kipindi cha uchaguzi. Vijana hao wamekuwa wakiahidiwa nafasi za uongozi endapo wagombea wao watashinda. Pia, vijana hao wamekuwa wakifanya sherehe mara kwa mara na kupewa zawadi, ikiwa ni pamoja na kupelekwa mbuga za wanyama.
Urari amesema, "Tumebaini kuwa baadhi ya viongozi wanawaandaa vijana kwa kigezo cha timu kazi na kuwashawishi kugawa rushwa kwa wananchi. Sasa tutaanza kutoa elimu kwa vyama vya kisiasa kabla ya kuchukua hatua za kisheria ili kuimarisha maadili ya uchaguzi."
Ofisa Uchunguzi wa TAKUKURU, Happyness Bilakwate, ameongeza kuwa TAKUKURU pia inatoa elimu ya kuzuia rushwa kupitia mitandao ya kijamii kwa kutumia kurasa zao rasmi, na aliwahimiza wananchi kufuatilia kurasa hizo ili kujifunza zaidi kuhusu mbinu za kuzuia rushwa.
Mkazi wa Mhongolo, Manispaa ya Kahama, Kareny Msasy, amethibitisha uwepo wa kundi la vijana wanaotumiwa na viongozi wa kisiasa kwa minajili ya kampeni zisizo za kimaadili, na alitoa wito kwa viongozi wa makundi hayo kuwapatia vijana elimu juu ya athari za rushwa.
© 2024 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED