161,020 'wakacha' mtihani kidato cha nne ukianza leo

By Romana Mallya , Nipashe
Published at 11:43 AM Nov 11 2024
Katibu Mtendaji wa Baraza la Mitihani la Tanzania (NECTA), Dk. Said Mohamed.
Picha: Mtandao
Katibu Mtendaji wa Baraza la Mitihani la Tanzania (NECTA), Dk. Said Mohamed.

MTIHANI wa Taifa wa Kidato cha Nne (CSEE) 2024 unaanza leo, lakini wanafunzi 161,020 sawa na asilimia 23.3 waliopaswa kuufanya, hawatakuwa miongoni mwa watahiniwa.

Katibu Mtendaji wa Baraza la Mitihani la Tanzania (NECTA), Dk. Said Mohamed, aliyasema hayo jana mkoani Dar es Salaam wakati akitangaza kuanza kwa mtihani huo utakaofanyika kuanzia leo hadi Novemba 29, mwaka huu.

"Mwaka juzi wakati wanafunzi hao wanafanya Mtihani wa Kidato cha Pili walikuwa 690,341, lakini walioandikishwa kufanya Mtihani wa Taifa wa Kidato cha Nne 2024 ni 529,321.

"Kuna upungufu wa takribani wanafunzi 161,000 waliofanya mtihani kidato cha pili ambao walitakiwa kufanya mtihani huu wa kidato cha nne na hawapo katika orodha ya waliosajiliwa mwaka huu," alisema.

Dk. Mohamed alisema ili kujua mahali walipo wanafunzi hao, ni suala la kujiridhisha kimkoa, halmashauri na katika ngazi ya kata kwa kila shule waliofanya Mtihani wa Upimaji Kidato cha Pili walikuwa wangapi na sasa waliofanya mtihani huu wako wangapi.

Akizungumzia mtihani huo wa kidato cha nne mwaka huu, Katibu Mtendaji huyo alisema jumla ya watahiniwa 557,731 wamesajiliwa kuufanya. Kati yao, watahiniwa wa shule ni 529,321 na wa kujitegemea ni 28,410.

Alisema kuwa kati ya watahiniwa wa shule waliosajiliwa mwaka huu, wavulana ni 250,562 sawa na asilimia 47.34 na wasichana ni 278,759 sawa na asilimia 52.66.

Dk. Mohamed alisema kuna watahiniwa wa shule 1,088 wenye mahitaji maalumu. Kati yao, wenye uoni hafifu ni 601, wasioona ni 56, wenye uziwi ni 209, wenye ulemavu wa akili ni 39 na wenye ulemavu wa viungo ni 183.

"Kati ya watahiniwa wa kujitegemea 28,410 waliosajiliwa, wavulana ni 11,167 sawa na asilimia 39.31 na wasichana ni 17,243 sawa na asilimia 60.69," alisema.

Dk. Mohamed alisema wapo watahiniwa wa kujitegemea wenye mahitaji maalumu 18. Kati yao, wenye uoni hafifu ni mmoja, wasioona ni 16 na mmoja mwenye ulemavu wa viungo.

Alisema mtihani huo utafanyika katika jumla ya shule za sekondari 5,585 na vituo vya watahiniwa wa kujitegemea 961.

Alisema maandalizi yote yamekamilika ikiwa ni pamoja na usambazaji mtihani, vijitabu vya kujibia na nyaraka zote muhimu zinazohusu mtihani katika mikoa ya Tanzania Bara na Zanzibar.

Katibu Mtendaji huyo alisisitiza suala la usalama wa vituo vya mitihani na kutoa wito kwa wasimamizi walioteuliwa kuisimamia kwa kufanya kazi zao kwa umakini, uadilifu na kwa kuzingatia weledi na kanuni na miongozo waliyopewa ili kila mtahiniwa apate haki yake.

Aliwataka wasimamizi kuhakikisha watahiniwa wenye mahitaji maalumu wanaifanya ipasavyo, ili wapate haki yao ya msingi, ikiwamo kuwapa mitihani yenye maandishi yaliyokuzwa kwa wenye uoni hafifu.

"Watahiniwa wenye mahitaji maalumu waongezewe muda wa dakika 20 kwa kila saa kwa somo la Hisabati na dakika 10 kwa kila saa kwa masomo mengine kama mwongozo wa baraza unavyoelekeza," alisema.

Kwa upande wa watahiniwa, Dk. Mohamed alisema baraza linaamini wamejiandaa vizuri, hivyo halitarajii mtahiniwa yeyote kujihusisha na vitendo vya udanganyifu, kwa kuwa atakayebainika, matokeo yake yatafutwa kwa mujibu wa kanuni za mitihani.

Kiongozi huyo pia aliwakumbusha wamiliki wa shule kutambua shule zao ni vituo maalumu vya mitihani na hivyo hawatakiwi kuingilia majukumu ya wasimamizi wa mtihani.

Alisema kwa kufanya hivyo, baraza halitosita kukifuta kituo chochote endapo litajiridhidhisha kuhatarisha usalama wa mtihani huo.

Baraza pia limetoa wito kwa jamii kutoa ushirikiano kuhakikisha mtu yeyote asiyehusika na mtihani huo haingii maeneo ya shule wakati wa mtihani.

Dk. Mohamed aliomba jamii kutoa ushirikiano kuhusu taarifa zote za udanganyifu kwa kuziwasilisha NECTA kupitia namba ya simu 0759 360 000 au barua pepe [email protected]