UONGOZI wa mabingwa watetezi wa Ligi Kuu Tanzania Bara, Yanga ya jijini, Dar es Salaam umesema kiwango cha timu yao hakijashuka na ushindani unaoonekana katika mechi za ligi hiyo wanazocheza unatokana na wapinzani wao kuimarika zaidi msimu huu, imeelezwa.
Akizungumza na gazeti hili jana, Ofisa Habari wa Yanga, Ali Kamwe, amepinga kile kinachozungumzwa na baadhi ya mashabiki wa soka na wachambuzi wanaodai ubora wa wachezaji wao umeshuka.
Kamwe alisema timu yao kupata ushindi wa bao moja tofauti na ushindi wa magoli mengi kama walivyokuwa wanapata katika msimu uliopita na kuongeza hawaamini huko ni kushuka ubora.
"Tunaposema Yanga imeshuka kiwango tunakuwa tumezinyima nafasi timu nyingine ambazo zinashiriki Ligi Kuu, hatujaitengeneza kwa ajili ya kufunga watu mabao matano au 10, badala yake wapinzani nao wanaimarika.
Kwa hiyo kama wapinzani wetu katika ligi wakiimarika sio kama timu yetu ni mbovu, nadhani tungekuwa hatupati matokeo ndio mngesema tumeshuka kiwango," alisema Kamwe.
Aliongeza rekodi zinaonyesha Yanga msimu uliopita ilikuwa ikifunga mabao mengi tofauti na msimu huu, lakini pia msimu huu wameshinda michezo nane mfululizo kitu ambacho hakikufanyika msimu uliopita na wavu wa timu yao bado haujaguswa.
"Tumeshinda mechi nane mfululizo, hatujaruhusu bao mpaka sasa, hii ni rekodi ambayo msimu uliopita haikuwepo, utasemaje tumeshuka kiwango?
"Ninavyoona mimi wapinzani hivi sasa wanaimarisha timu zao hasa upande wa ulinzi, makocha wao wamekuwa wakifanya kazi kubwa kuizuia Yanga, lakini watu hawafanyi hivyo wanakuja kusema tu tumeshuka kiwango," Kamwe alisema.
Msimu uliopita Yanga ilipoteza mechi ya raundi ya nne, ikifungwa mabao 2-1 dhidi ya Ihefu na ndiyo ilikuwa mara ya kwanza kuruhusu wavu wake kuguswa, baada ya kuichapa KMC mabao 5-0, ikaifunga JKT Tanzania idadi kama hiyo halafu ikapata ushindi wa bao 1-0 dhidi ya Namungo, kabla ya kukutana na kipigo hicho.
Wakati huo huo, Kamati ya Uendeshaji wa Usimamizi wa Ligi ya Bodi ya Ligi Kuu Tanzania imeitoza Yanga faini jumla ya Sh. milioni 12 kutokana na makosa matatu waliyafanya katika mechi ya dhidi ya Simba iliyochezwa Oktoba 19, mwaka huu kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa, ikiibuka na ushindi bao 1-0.
Taarifa iliyotolewa na Shirikisho la Mpira wa Miguu Nchini (TFF), Yanga imetozwa Sh. milioni 10 kwa kutumia mlango usio rasmi wa kuingilia uwanjani siku ya mchezo kinyume na kanuni ya 17:62 ya Ligi Kuu.
Pia Yanga imetozwa faini ya Sh. milioni moja kwa kosa la kukataa kutumia chumba maalumu cha kubadilishia nguo kinyume na kanuni ya 17:62, na kosa la tatu imetozwa fainali ya Sh. milioni moja kutokana na kuwakilishwa na Kocha Mkuu pekee katika mkutano wa Wanahabari kinyume na natakwa ya kanuni ya 17:58 ya Ligi Kuu kuhusu taratibu za mchezo, inayotaka aambatane na nahodha ama mchezaji mwenye ushawishi kikosini.
Klabu hiyo pia imepewa onyo kwa kuchelewa kufika uwanjani huku meneja wake, Walter Harrison, amefungiwa michezo mitatu na kutozwa faini ya Sh. milioni moja kwa kosa la kuwataka waamuzi waliochezesha mchezo wao dhidi ya Coastal Union kufanya uamuzi kwa mujibu wa wa maoni yake, akitumia kompyuta ndogo kuwaonyesha marudio ya picha mjongeo (video) ya matukio mbalimbali ya mchezo huo kama ushahidi wa yale aliyokuwa akiyalalamikia, kitendo kilichotafsiriwa na kamati kama ni kushawishi, kuleta shari au vurugu uwanjani.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED