BODI ya Ligi Tanzania Bara (TPLB), imeeleza kufurahishwa kwake na ushindani mkali unaooneshwa na timu mbalimbali kwenye michezo yake inayoendelea.
Akizungumza jana jijini Dar es Salaam, Ofisa Mtendaji Mkuu wa Bodi hiyo, Almasi Kasongo, alisema kwa raundi 10 ambazo timu zimecheza Ligi Kuu imekuwa na msisimuko mkali, huku ushindani ukiongezeka tofauti na msimu uliopita.
"Ligi imekuwa na ushindani mkubwa ukilinganisha na msimu uliopita, ipo kwenye raundi ya 10, timu zingine zikiwa zimecheza mechi 11, lakini unaweza ukaona kwamba timu zote walau zimepoteza mchezo mmoja, ukilinganisha na msimu uliopita katika kipindi kama hiki kulikuwa na timu ambazo bado zilikuwa hazijapoteza mchezo," alisema Kasongo.
Alisema sababu nyingine inayoonesha ligi ya msimu huu imekuwa ngumu zaidi ni baadhi ya matokeo ya mechi kuamuliwa dakika za mwisho.
"Vile vile unaweza kuona ni jinsi gani michezo ilivyokuwa na ushindani mkubwa, tumeona michezo mingi ikiamuliwa dakika za jioni, dakika za nyongeza, kwenye sekunde za mwisho kabisa, hii inadhihirisha ushindani mkubwa," alisema Ofisa Mtendaji Mkuu huyo.
Alisema hiki ndicho mashabiki wengi wa soka nchini na Watanzania walikuwa wakihitaji, kupata ligi ambayo ni ngumu, yenye ushindani, ambayo haitabiriki, huku akitabiri kuwa kadri inavyozidi kusonga mbele, ndivyo itakavyokuwa na ushindani zaidi kuliko huu uliopo sasa.
"Itoshe kusema kile ambacho Watanzania walikuwa wanakitarajia kupata ligi yenye ushindani sasa hivi kinaonekana, matarajio yetu ni kwamba hadi itakapofika Aprili na Mei ushindani utazidi kuwa mkali zaidi kuliko huu kwa sababu ni kipindi baadhi ya timu zitakuwa zinaelekea kwenye ubingwa, zingine kuwania nne bora kwa ajili ya kucheza mechi za kimataifa, kuna zitakazokuwa zinapambana kutocheza 'play off', na zipo ambazo zitakuwa zinapigana kutoshuka daraja," alisema.
Mpaka wakati ligi hiyo imesimama kupisha Kalenda ya FIFA, Simba inaongoza ikiwa imejikusanyia jumla ya pointi 25, Yanga iko nafasi ya pili ikiwa na pointi 24, Singida Black Stars ni ya tatu na pointi zake 23, huku Azam FC ikikamata nafasi ya nne, pointi zake 21.
© 2024 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED