Tanzania yamaliza 2024, kwa rekodi, timu 7 zafuzu kimataifa

By Mwandishi Wetu , Nipashe
Published at 11:23 AM Dec 30 2024
Rais wa Shirikisho la Soka nchini (TFF), Wallace Karia
Picha: Mtandao
Rais wa Shirikisho la Soka nchini (TFF), Wallace Karia

MWAKA 2024 umeonekana kuwa ni wa mafanikio makubwa kwenye soka la Tanzania, ambapo timu zake mbalimbali za taifa zimefuzu kucheza michuano ya kimataifa kitu ambacho ni nadra sana kutokea huko nyuma kwenye mchezo wa mpira wa miguu.

Chini ya uongozi wa rais wa Shirikisho la Soka nchini (TFF), Wallace Karia, timu saba za taifa zimefuzu fainali zake ambazo zingine zimeshachezwa na zingine zitachezwa mwakani.

Wiki iliyopita, Timu ya Taifa Ya soka ya Vijana chini ya miaka 17, Serengeti Boys, ilifuzu kucheza fainali za AFCON chini ya miaka hiyo zitakazofanyika nchini Morocco mwakani.

Hii ni baada ya kuichapa, Sudan Kusini mabao 4-0, katika mchezo wa kusaka kucheza fainali hizo kutoka Ukanda wa Afrika Mashariki (CECAFA).

Tanzania pia mwaka huu ilifuzu fainali za Mataifa ya Afrika kwa Walemavu (BAFCON), yaliyofanyika mwaka huu nchini Misri, hata hivyo michuano hiyo haipo chini ya TFF, lakini moja ya mafanikio makubwa kwa taifa linaloongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan.

Kikosi cha Timu ya Taifa chini ya miaka 15, nacho kilifanikiwa kufuzu fainali za shule barani Afrika, huku Tanzania ikiwa mwenyeji.

Timu ya Taifa chini ya miaka 20, Ngorongoro Heroes nayo haikuwa nyuma, kwani imefuzu fainali za AFCON, ambazo zinatarajiwa kuchezwa nchini Ivory Coast.

Kikosi cha Timu ya Taifa ya Wanawake, Twiga Stars, nacho kimefuzu kucheza fainali za Mataifa ya Afrika (WAFCON), zinazotarajiwa kuchezwa nchini Morocco.

Kama vile haitoshi Tanzania imepeleka fainali timu mbili za soka wanaume, moja ya Wachezaji wa Ndani ya nchi na nyingine ni ya jumla, CHAN. 

Kwa upande wa CHAN, Stars ilifuzu fainali hizo zinazotarajiwa kupigwa mwakani katika nchi tatu za Tanzania, Kenya na Uganda kama mwenyeji.

Taifa Stars, timu kubwa ya soka Tanzania yenye wachezaji wote wa ndani na nje, yenyewe ilifanikiwa kufuzu (AFCON), zinazotarajiwa kuchezwa mwakani nchini Morocco.

Rais Samia amekuwa msaada mkubwa katika mafanikio hayo kwa kuzisapoti na kuzipongeza kwa fedha kila zinaposhinda.