TIMU ya Taifa ya Tanzania, Taifa Stars imefungwa kwa mikwaju ya penalti 6-5 na Sudan katika mchezo wa kusaka tiketi ya kufuzu kucheza fainali za Mataifa ya Afrika kwa Wachezaji wa Ndani (CHAN), uliopigwa Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es Salaam jana.
Timu hizo zililazimika kupigiana penalti baada ya matokeo ya jumla kuwa bao 1-1 kwa michezo yote miwili, Sudan ikishinda bao 1-0 kwenye mchezo wa kwanza uliopigwa nchini Mauritania, kabla ya jana Stars nayo kushinda 1-0, lililowekwa ndani ya wavu na Crispian Ngushi dakika ya 32.
Penalti za Sudan zilifungwa na Walieldin Khidir, Mohamed Abdulrahman, Salaheldin Adil, Ramadan Agab na Ally Abdallah, huku za Stars zikizamishwa kimyani na Shekhan Ibrahim, Daud Brayson, Abdallah Said, Sabri Kondo na Abdulkarim Kassim, huku Paul Peter mkwaju wake ukipanguliwa na golikipa Ahmed El Fatih.
Nahodha wa Stars, Aishi Manula, ambaye mashabiki walikuwa na matumaini makubwa ya kumuona akiokoa penalti kama ilivyo sifa yake, lakini zote zilitinga wavuni.
Matokeo hayo yanaifanya Stars kushindwa kufuzu fainali za CHAN kwa uwezo wa uwanjani, badala yake imefuzu kutokana na uenyeji kwani fainali hizo zitachezwa mwakani hapa nchini, Kenya na Uganda, ikiwa ni majaribio ya maandalizi ya fainali za Mataifa ya Afrika (AFCON) 2027 katika nchi hizo.
Ushindi huo umeipa Sudan tiketi ya kufuzu fainali hizo, huku nchi hiyo ikiwa inacheza mechi zake za nyumbani nchini Mauritania kutokana na nchi yao kukubwa na vita vya wenyewe kwa wenyewe.
Katika mchezo wa jana, Stars ilitumia wachezaji wengi wa timu ya vijana, Ngorongoro Heroes, pamoja na wakongwe wachache akiwamo Manula ambaye ndiye nahodha wa kikosi hicho.
Ilikosa mabao maengi kupitia kwa mastraika wake, Selemani Mwalimu, Edgar William, na wengine ambao kwa kiasi kikubwa wameonekana kuwa na uchu wa mafanikio chini ya Kocha Bakari Shime.
Dakika moja kabla ya mechi kumalizika, straika Nassor Saadun, alizawadiwa kadi nyekundu baada ya kucheza rafu tatu mfululizo, moja alionywa, ya pili alipewa kadi ya njano na ya tatu nyekundu kwa dakika zisizozidi mbili mbili kila tukio.
Alikuwa ameingia kipindi cha pili kuchukua nafasi ya Hijjah Shamte. Straika huyo wa Azam FC, alicheza mechi ya pili mfululizo baada ya jana kuwa mmoja wa wachezaji waliocheza mechi ya Ligi Kuu Tanzania Bara, timu yake ikicheza dhidi ya Yanga na kushinda bao 1-0.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED