Singida Fountain Gate yaipiga mikwara Yanga

By Adam Fungamwango , Nipashe
Published at 07:02 AM Apr 06 2024
Kocha Mkuu wa timu hiyo, Jamhuri Kihwelo 'Julio',.
Picha: Maktaba
Kocha Mkuu wa timu hiyo, Jamhuri Kihwelo 'Julio',.

ILI kuhakikisha inajiondoa katika hatari ya kushuka daraja, Singida Fountain Gate imesema haitakubali kupoteza mechi yake ya Ligi Kuu Tanzania Bara dhidi ya Yanga itakayochezwa Aprili 14, mwaka huu kwenye Uwanja wa CCM Kirumba jijini, Mwanza.

Ofisa Habari wa klabu hiyo, Hussein Massanza, amesema kuifunga Yanga ni moja kati ya ajenda zao 10 ambazo wanatarajiwa kuzitelekeza kabla ya kumaliza mechi za Ligi Kuu Tanzania Bara msimu huu.

Massanza alisema baada ya kupata ushindi wa bao 1-0 dhidi ya Namungo, ajenda hayo inayofuata namba mbili ni kushinda mechi hiyo dhidi ya Yanga ambayo itawaimarisha katika kutimiza malengo ya kubakia Ligi Kuu.

"Tulianzisha agenda 10, hizo ni mechi ambazo tumebakiwa nazo, tumeweka malengo ya kushinda mechi zote hizo, au kama ikipungua sana tuvune hata pointi moja, lakini si kupoteza hata mchezo mmoja, tulianza kwa Namungo, sasa tunakwenda kwa Yanga na wengine wote watakaokuja wajiandae," alisema Massanza.

Kocha Mkuu wa timu hiyo, Jamhuri Kihwelo 'Julio', amesema hawaihofii Yanga na watakwenda kupambana kwa tahadhari kwa sababu wanahitaji kuondoka na matokeo chanya.

"Tumejiandaa na tumejipanga vizuri, Yanga ni timu inayofungika kama tutakwenda kwa mipango na maelekezo. Siyo kama tukicheza na Yanga yaani tayari wameshatufunga, wanafungika kabisa hakuna matatizo yoyote, tutakabiliana nao kwa ajili ya kusaka ushindi," alisema Julio.

Baada nyingine za Singida Fountain Gate zilizobakia ambazo zimewekwa katika  mpango wao wa ajenda 10 ni dhidi ya Ihefu FC itakayochezwa Aprili 18, mwaka huu na baadaye itawakabili Mashujaa FC utakaopigwa Aprili 18 halafu itapambana na Coastal Union Mei 2, mwaka huu.

Mei 7, mwaka huu Singida Fountain Gate itakutana na Dodoma Jiji wakati mechi dhidi ya JKT Tanzania, KMC na Geita Gold bado hazijapangiwa tarehe lakini Mei 29, mwaka huu itakuwa na mchezo dhidi ya Kagera Sugar.

Yanga ndio vinara na mabingwa watetezi wa Ligi Kuu Tanzania Bara.