KOCHA Mkuu wa Singida Black Stars, Patrick Aussems, amesema kikosi chake kitafanya 'maajabu' msimu huu kutokana na aina ya wachezaji alionao.
Aussems aliliambia gazeti hili jana anaiona timu yake ikifanya vizuri msimu huu na kutoa ushindani kwa klabu kubwa hapa nchini katika mechi za Ligi Kuu Tanzania Bara inayoendelea.
"Nimekuwa hapa Tanzania kwa miaka kadhaa, naifahamu Ligi Kuu, najua timu kubwa zilizozeeleka ni Simba, Yanga na Azam lakini naiona timu yangu ikiwa kwenye mwelekeo mzuri, tunaweza tukafanya kitu ambacho wengi hawategemei," alisema Aussems.
Alisema kikosi chake kina wachezaji wenye uwezo mkubwa, wanaojituma na wanauwezo wa kuipa timu hiyo matokeo mazuri katika mechi zao zijazo.
Aliongeza lengo lake ni kuona timu inaendelea kufanya vizuri na kumaliza katika nafasi za juu ili kupata tiketi ya kushiriki mashindano ya kimataifa mwakani.
"Hili linawezekana kama tutaendelea kufanya kazi nzuri, wachezaji kujituma na uongozi kufanya kazi yao, hakuna kisichowezekana, naamini tutafanya vizuri," Aussems aliongeza.
Kabla ya mchezo wa jana kati ya Simba na KMC, Singida Black Stars ilikuwa ikishika nafasi ya pili katika msimamo wa Ligi Kuu Tanzania Bara ikiwa na pointi 23 kinindoni baada ya kucheza michezo 10.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED