Simba yapania kuanza CAF kwa ushindi mnono

By Adam Fungamwango , Nipashe
Published at 10:08 AM Nov 11 2024
Meneja Habari na Mawasiliano wa klabu hiyo, Ahmed Ally .
Picha: Mtandao
Meneja Habari na Mawasiliano wa klabu hiyo, Ahmed Ally .

BAADA ya mapumziko ya siku nne, kikosi cha Simba kinaanza rasmi leo mazoezi kwa ajili ya kujiandaa na mchezo wa kwanza wa Kombe la Shirikisho Afrika hatua ya makundi dhidi ya Bravo do Maquis ya Angola, utakaochezwa Novemba 27, mwaka huu kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa jijini Dar es Salaam, huku ikipania kuanza na ushindi mnono nyumbani.

Meneja Habari na Mawasiliano wa klabu hiyo, Ahmed Ally, amesema wachezaji watakaoanza mazoezi ni ambao hawatokwenda kwenye timu zao za taifa ambazo zinapambana kwa ajili ya kusaka tiketi ya kucheza fainali za Mataifa ya Afrika (AFCON) 2025, zitakazofanyika nchini Morocco.

Akizungumza jana jijini Dar es Salaam, Ahmed alisema baada ya mapumziko ya siku nne ambayo wachezaji wa timu hiyo waliyapata baada ya kucheza mchezo wa Ligi Kuu dhidi ya KMC na kushinda mabao 4-0, kwenye Uwanja wa KMC Complex, Dar es Salaam, Jumatano iliyopita, wachezaji wa timu hiyo wanarejea rasmi mazoezini, Uwanja wa Mo Arena, Bunju, Dar es Salaam kujiandaa na mchezo huo chini ya kocha raia wa Afrika Kusini, Fadlu Davids.

"Kikosi kinarejea mazoezini Jumatatu baada ya siku nne za mapumziko, tukiliangalia Kombe la Shirikisho tuna uwezo wa kufanya vizuri msimu huu kwa mambo mawili. Kwanza kuanza michuano na ushindi mnono na pia tunaweza kuwa ndiyo klabu itakayokuwa inajaza mashabiki wengi zaidi kuliko zingine zinazocheza michuano hii katika michezo yote, na hili kwa mashabiki wa Simba linawezekana, deni litakalobaki ni kwa wachezaji wetu kupambana kutuletea ushindi tu," alisema Meneja Habari huyo.

Tayari Bodi ya Ligi imetangaza kuahirisha michezo ya Ligi Kuu ya Simba na Yanga ambazo zilitakiwa kucheza Novemba 21 kwa ajili ya kuzipa nafasi kujiandaa na michezo ya kimataifa.

Simba ilitakiwa kucheza dhidi ya Pamba Jiji, kwenye Uwanja wa CCM Kirumba jijini Mwanza, Novemba 21, mchezo ambao sasa umesogezwa mbele hadi utakapotangazwa tena.

Taarifa nzuri kwa Wanasimba ni urejeo wa kiungo mkabaji Yusuph Kagoma ambaye alisema yuko katika hatua za mwisho za matibabu na wiki mbili zijazo kabla ya mchezo huo atakuwa amepona na kuanza mazoezi na wenzake tayari kwa mchezo huo.

"Kuhusu Abdulrazack Hamza yeye ameshapona na ameitwa kwenye kikosi cha Timu ya Taifa ya Tanzania, Taifa Stars, hivyo tunakwenda kwenye mchezo dhidi ya Bravo do Maquis tukiwa kamili, itakuwa ni maamuzi kwa kocha tu ni mchezaji gani wa kumpanga na nani wa kusubiri," alisema Ahmed.

Alisema hamasa kueleka kwenye mchezo huo zitaanza Novemba 20 kuzunguka mitaani kwa ajili ya kuwaita mashabiki uwanjani.

Kabla ya mazoezi yatakayoanza leo, siku mbili zilizopita Fadlu alisema kuwa moja kati ya kazi atakazozifanya ni kuwasoma wapinzani wake ili kujua ni timu ya aina gani, inacheza vipi ili kuangalia ubora na udhaifu.

"Tutaangalia mifumo yao, jinsi wanavyocheza, ubora na udhaifu wao, ili kuwaelekeza wachezaji wetu jinsi ya kukabiliana na wapinzani wetu hasa katika mchezo huu wa kwanza ambao tutacheza nyumbani, tunataka ushindi wa kwanza na mkubwa," alisema kocha huyo raia wa Afrika Kusini.