MABAO ya Awesu Awesu, Jean Charles Ahoua na Edwin Balua dhidi ya KMC jana kwenye ushindi wa mabao 4-0 yaliipandisha Simba kutoka nafasi ya tatu mpaka kileleni mwa msimamo wa Ligi Kuu Tanzania Bara baada ya kufikisha pointi 25, pointi moja zaidi ya Yanga ambao leo wana nafasi ya kurejea kileleni kama watapata ushindi dhidi ya Tabora United kwenye mchezo utakaochezwa uwanja wa Azam Complex.
Simba jana walianza mchezo huo kwenye uwanja wa KMC kwa kasi ambapo walikosa mabao dakika ya tatu na ya 17 baada ya Ahoua na Steven Mukwala kushindwa kuzitumia vizuri krosi za beki wa pembeni, Valentin Nouma, hata hivyo walifanikiwa kuibuka na ushindi huo mnono.
Simba walianza kuhesabu mabao yao katika dakika ya 24 kufuatia shambulizi lao lililozaa matunda ambapo Awesu alifunga bao la kwanza kwa shuti la juu akiwa ndani ya boksi baada ya kupokea pasi nzuri ya Mukwala.
Baada ya bao hilo KMC walijaribu kujipanga kulipiza mashambulizi lakini juhudi zao zilikuwa zikizimwa na viungo wa Simba wakiongozwa na Fabrice Ngoma na Fernandez Mavambo.
Zikiwa zimebaki dakika saba kabla ya kwenda mapumziko, Ahoua aliipatia Simba bao la pili kwa mkwaju wa penalti iliyotolewa na mwamuzi Shomari Lawi baada ya Shomari Kapombe kuangushwa kwenye eneo la hatari.
Mabao hayo mawili yalidumu mpaka kipindi cha kwanza kinamalizika.
Kipindi cha pili kilianza kwa kasi ambapo timu zote zilishambuliana huku KMC wakionekana kubadilika kwa kumiliki mpira, hata hivyo ni Simba walioendelea kuzifumania nyavu za wapinzani wao ambapo dakika ya 66, mtokea benchi, Balua aliyeingia dakika ya 60 kuchukua nafasi ya Awesu kuipatia Simba bao la tatu kwa shuti kali akiwa ndani ya boksi baada ya kupokea pasi ya Nouma.
Mbali na Balua, Simba pia iliwaingiza Mzamiru Yassin, Omary Omary na Kibu Denis kuchukua nafasi za Fernandez, Ngoma na Ladack Chasambi mabadiliko yaliyowaongezea nguvu.
Dakika ya 69, makosa ya beki wa KMC, Ismail Gambo yalitumiwa vizuri na Ahoua aliyeipatia Simba bao la nne kwa shuti la chini chini baada ya beki huyo kushindwa kurudisha vizuri mpira wa golikipa wake ambao ulinaswa na mfungaji.
Bao hilo limemfanya Ahoua kufikisha idadi ya mabao matano na 'assist' nne msimu huu akiwa nyuma kwa goli moja dhidi ya kinara wa mabao mpaka sasa, Seleman Mwalimu wa Fountain Gate mwenye mabao sita.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED