Simba SC yaitisha Mashujaa

By Adam Fungamwango , Nipashe
Published at 08:15 AM Oct 31 2024
Meneja wa Habari na Mawasiliano wa Simba, Ahmed Ally
Picha:Mtandao
Meneja wa Habari na Mawasiliano wa Simba, Ahmed Ally

KLABU ya Simba imeipiga mkwara mzito Mashujaa FC, ikisema ni timu ambayo inataka kuwazoea, hivyo imepanga kuwapa 'kipigo kikali' katika mechi ya Ligi Kuu Tanzania Bara itakayochezwa kesho kwenye Uwanja wa Lake Tanganyika mkoani, Kigoma.

Meneja wa Habari na Mawasiliano wa Simba, Ahmed Ally, aliliambia gazeti hili jana, wamejipanga imara kuhakikisha wanarudisha heshima yao.

Ahmed alisema Mashujaa FC wamekuwa na 'dhihaka' kwao hasa baada ya msimu uliopita kuwatoa katika hatua ya 16 Bora ya mashindano ya Kombe la Shirikisho na Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), maarufu Kombe la FA.

Katika mchezo huo, Maafande hao wa Mashujaa waliwaondoa Simba kwa penalti 6-5 baada ya timu hizo kutoka sare ya bao 1-1 katika dakika 90 za kawaida.

Meneja huyo alisema wameenda Kigoma 'kuwafuta machozi' wanachama na mashabiki wao, ambao mara ya mwisho waliwaachia majonzi kutokana na matokeo ya kuumiza ya mchezo huo.

"Kikosi kitaondoka leo (jana), kwenda Kigoma, Mashujaa wanaonekana kutaka kutuzoea sasa, inampa kichwa kwa sababu walitutoa katika michuano ya Kombe la FA msimu uliopita, lakini wakumbuke Simba ile siyo hii ambayo ina maboresho makubwa, ni ya Fadlu Davis, Debora Fernandes Mavambo, Leonel Ateba, Moussa Camara, Jean Charles Ahoua na wengine.

Tunakwenda kuwafuta machozi wanachama mashabiki wa Simba Kigoma ambao mara ya mwisho tuliwaachia majonzi makubwa, safari hii tunakwenda kuchukua pointi tatu, hii ndiyo kampeni yetu kuanzia sasa," alisema Ahmed.

Hata hivyo, katika michezo ya Ligi Kuu Tanzania Bara, rekodi zinaonyesha Simba imeshinda michezo yote miwili ya msimu iliopita.

Ilishinda bao 1-0 kwenye Uwanja wa Lake Tanganyika mechi iliyofanyika Februari 3, mwaka huu kabla ya kushinda mabao 2-0 katika mchezo wa mzunguko wa pili uliochezwa Machi 15, mwaka huu kwenye Uwanja wa Azam Complex, Dar es Salaam.

Simba itashuka katika mchezo huo, baada ya kutocheza mechi dhidi ya JKT Tanzania ambao walipata ajali Jumapili iliyopita walipokuwa wakitoka Dodoma kuwakabili wenyeji Dodoma Jiji.

Baada ya Bodi ya Ligi (TPLB), kuahirisha mechi hiyo hadi itakapotangazwa siku nyingine, Simba iliendelea na mazoezi na jana asubuhi ilisafiri kwenda Kigoma ambapo iliwasili salama mkoani humo.

Naye Kocha Mkuu, Fadlu Davis, akisema kutokuwapo kwa mchezo huo kumesaidia kuwapa wachezaji wake mapumziko kwa sababu walikuwa na uchovu.

"Kutocheza mechi dhidi ya JKT Tanzania kwa upande wetu imetusaidia kuwapa nafasi ya kupumzika wachezaji wangu, kiukweli walikuwa wamechoka kwa sababu ya kucheza mechi nyingi ndani ya muda mfupi, na wengine ni majeruhi," Fadlu alisema.

Aliongeza wachezaji wengine ambao si majeruhi wako tayari kwa ajili ya kusaka pointi tatu muhimu.

"Najua hakuna mechi rahisi katika ligi, tuko tayari kupambana na kusaka matokeo mazuri, tunaamini tutafikia malengo yetu," alisema kocha huyo.

Wachezaji wa Simba ambao ni majeruhi na hawapo katika mpango wa mechi ya kesho ni Abdulrazack Hamza na Yusuph Kagoma, nyota hao waliumia katika mchezo wa watani wa jadi dhidi ya Yanga uliochezwa Oktoba 19, mwaka huu kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es Salaam.