Ramovic: Mchezo na TP Mazembe ni hatma yetu Ligi ya Mabingwa

By Faustine Feliciane , Nipashe
Published at 12:40 PM Jan 02 2025
Kocha wa Yanga, Sead Ramovic
Picha:Mtandao
Kocha wa Yanga, Sead Ramovic

KOCHA wa Yanga, Sead Ramovic, amesema mchezo wao wa jumamosi ijayo dhidi ya TP mazembe utaamua hatma yao kwenye michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika huku akiwaomba mashabiki kuujaza uwanja.

Jumamosi, Januari 4, Yanga itaumana na wakongo hao kwenye mchezo wamarudiano hatua ya makundi huku wawakilishi hao wa Tanzania wakihitaji ushindi kuweka hai matumaini ya kutinga hatua ya robo fainali.

Akizungumza juzi jijini Dar es Salaam, Ramovic, amesema kutokana na umuhimu wa mchezo huo angependa kuona mashabiki wanajitokeza kwa wingi kuwaongezea hamasa wachezaji wake ili kupata kile wanachokihitaji.

"Ni mchezo ambao tunahitaji ushindi sana, hatima ya sisi kuendelea kupambania kuchezea robo fainali ni kwenye mchezo huu na TP Mazembe, tutaendelea na maandalizi yetu mpaka siku ya mchezo," alisema Ramovic.

Aidha, alisema mchezo huo hautakuwa mwepesi kutokana na wapinzani wao nao kuhitaji ushindi.

"Tulifanikiwa kupata alama moja ugenini, TP Mazembe watakuja kwa lengo la kupata ushindi na wao, lakini sisi kuwa kwenye uwanja wa nyumbani utachangia sana kupambana kupata ushindi," alisema Ramovic.

Aidha, kuhusu maandalizi yao, Ramovic, amesema baada ya kuwaona wapinzani wao kwenye mchezo wa kwanza Lubumbashi ambao ulimalizika kwa kufungana bao 1-1, vipo vitu anavyoviongeza kwa wachezaji wake mazoezini.

"Utakuwa mchezo wa mbinu zaidi, yapo mambo ambayo nayafanyia kazi ili kuhakikisha tunapata ushindi, nimewaona wapinzani wetu ni timu nzuri na yenye uzoefu sasa lazima tujipange vizuri," alisema.

Kwenye lao la A la michuano hiyo, Yanga wanaburuza mkia kwa kuwa na pointi moja peke katika michezo mitatu waliyocheza, Al Hilal wanaongoza wakiwa na pointi tisa wakifuatiwa na Mc Alger wenye pointi nne huku TP Mazembe wakiwa nafasi ya nne na pointi mbili.

Kama Yanga watapoteza mchezo huo watakauwa wamejiweka katika mazingira magumu kutinga robo fainali ya michuano hiyo kwa mara ya pili kwani watabakiwa na pointi moja huku Mazembe wakiwa na pointi sita.

Yanga wakishinda watakuwa wameamsha matumaini ya kusonga mbele kwa kuwa watakuwa wamefikisha alama nne na kutakiwa kushinda mechi mbili zitakazokuwa zimebaki dhidi ya Mc Alger na Al Hilal.