KOCHA Mkuu wa Simba, Fadlu Davids, amesema kazi iliyobaki ni kuhamishia majeshi yake nchini Angola dhidi ya Bravos do Maquis, akisema anataka timu yake ifuzu hatua ya robo fainali ikiwa nchini humo, ili mechi ya mwisho dhidi ya CS Constantine ya Algeria iwe kama Tamasha la Simba Day.
Akizungumza nchini Tunisia baada ya kumalizika kwa mchezo wa raundi ya nne, Kombe la Shirikisho Afrika uliochezwa Uwanja wa Olympique Hammadi Agrebi jijini Tunis na kushinda bao 1-0 dhidi ya CS Sfaxien ya nchini humo, alisema katika mchezo huo utakaopigwa Jumapili ijayo, watahakikisha wanafanya kila njia ili wafuzu kwani wanahitaji ushindi au sare tu.
Alisema haitokuwa rahisi, lakini atakiandaa kikosi kucheza kama fainali katika mchezo huo.
"Tumefurahi, tumeshinda mchezo huu muhimu kwa sababu ilikuwa ni lazima, baada ya hapa kilichobaki ni kwenda Angola tukiwa na kazi moja tu ya kutinga hatua ya robo fainali tukiwa kwenye ardhi hiyo, kwa bahati nzuri tunahitaji matokeo mawili, ushindi au sare.
Ushindi utatufanya tufikishe pointi 12, na sare tutakuwa na pointi 10, tutanufaika na kanuni ya sisi na Bravo do Maquis tulipokutana, kwani hata kama akishinda mchezo wa mwisho dhidi ya CS Sfaxien na kufikisha pointi 10, sisi tutasonga mbele hata kama tutapoteza mechi ya mwisho," alisema kocha huyo.
Hata hivyo, Fadlu alisema kwa malengo ya awali aliyojiwekea kikosi chake kingekuwa kimeshafuzu mpaka sasa.
Alisema alihitaji pointi 10 hadi 12 awe nazo mpaka sasa, lakini kipigo cha mabao 2-1 dhidi ya Constantine nchini Algeria, kilitibua mipango na malengo yote aliyojiwekea.
"Nilihitaji hadi muda huu tuwe na pointi 10 au 12, baada ya mechi nne, hatukutaka kupoteza hata mchezo mmoja kwenye kundi hili, hesabu zilivurugika baada ya kufungwa na CS Constatine, pamoja na hayo tutahakikisha hatupotezi mchezo wowote ule kati ya miwili iliyobaki," alisema Fadlu.
Aliwasifu wachezaji wake kwa kucheza kwa maelekezo, kwani waliwajibika uwanjani huku wakikabiliwa na hali ya hewa ya baridi ambayo hawakuizoea zaidi ya wapinzani wao, lakini pia kupunguza makosa binafsi ambayo yaliwaathiri kwenye michezo kadhaa iliyopita.
Mfungaji wa bao hilo pekee, kiungo mshambuliaji raia wa Ivory Coast, Jean Charles Ahoua, alisema mchezo ulikuwa mgumu kwani walizihitaji mno pointi tatu, lakini sasa wanaangalia michezo iliyobaki.
"Tuna furaha kwa ushindi huu kwa sababu mechi ilikuwa ngumu sana, tulihitaji pointi tatu kwa njia yoyote ile kwa ajili ya kujiweka kwenye sehemu nzuri ili kuweza kufuzu, tuna furaha na mimi nina furaha kwa kuipatia timu yangu ushindi.
"Pamoja na hayo, tunapaswa sasa kuangalia michezo miwili iliyobaki, hasa dhidi ya Bravo do Maquis, ambayo tukifanya vema tutakuwa tumefuzu," alisema.
Mwenyekiti wa Klabu hiyo, Murtaza Mangungu, aliwasifu wachezaji kwa kupambana licha ya ugumu wa hali ya hewa.
"Hali ya hewa ilikuwa ngumu sana, ni baridi sana, pamoja na kwamba timu ilikuja mapema kwa ajili ya kuzoea hali ya hewa, lakini hali haikuwa nzuri sana.
"Tunashukuru kocha Fadlu Davids kwa kutengeneza 'plan' nzuri ya uchezaji, wachezaji nao wamejituma kwa kiasi kilichostahili na kuweza kuwadhibiti, wenzetu walikuwa wanacheza wakisema liwalo na liwe ni lazima wapate ushindi, na sisi tulihitaji ushindi pia," alisema.
Simba inashika nafasi ya pili ikiwa na pointi tisa sawa na CS Constantine inayoongoza, lakini inazidiwa kwa tofauti nzuri ya mabao ya kufunga na kufungwa, Bravo do Maquis ikiwa na pointi sita, nafasi ya tatu, CS Sfaxien ikiburuza mkia bila pointi.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED