CHADEMA inaendelea na mchakato wa kujiandaa na uchaguzi wa viongozi wa safu ya juu baadaye mwezi huu, lakini vita vya kuwania uongozi kati ya mwenyekiti na makamu wake wanaogombea nafasi moja, vinawaibua washauri wanaowataka kupunguza kutuliza munkari.
Ni Januari 21 atakapochaguliwa Mwenyekiti Taifa na Makamu wake, wakati huu njia zote zikielekea kwenye uchaguzi huo, wanachama na wafuasi wamegawanyika makundi mawili.
Ni walio upande wa Mwenyekiti wa sasa Freeman Mbowe na wale wanaomuunga Makamu Mwenyekiti Tundu Lissu.
Hatua hiyo inatokea baada ya miamba hiyo miwili kuchukua fomu kuwania nafasi ya Mwenyekiti wa Taifa na kusababisha kuwapo kwa mgawanyiko huo.
Kuwapo mazingira hayo, mchambuzi wa siasa anayechipukia, Pawa Lufunga, anakuja na ushauri kwa chama hicho kwa lengo la kutaka kivuke salama kwenye uchaguzi ujao.
Pawa anashauri, ifanyike meza ya mazungumzo, wazee wa chama na washauri wa chama wakae nao kabla ya uchaguzi ili kuweka mambo sawa, kuwa na dira moja itakayosaidia kudhibiti makovu yanayoweza kujitokeza katika uchaguzi unaokuja.
"Lakini pia ni muhimu Lissu kuongozwa na hekima zaidi kwani yeye ni mgombea na si mshindi, hivyo huenda asishinde, ikitokea hajashinda maisha yake mbele ya viongozi aliowanyooshea vidole ili aweze kuongozwa nao itamlazimu kuwa na hekima zaidi," anasema.
Anasema hekima isipotumika ataamua aidha kudai amehujumiwa na kutumia nguvu ya kitaaluma ya sheria kuwapeleka mahakamani ambako huenda kukawa na anguko kubwa la chama.
Mchambuzi huyo anaongeza kuwa hali hiyo huenda pia ikatumiwa si tu kuangamiza chama bali kumwangamiza yeye mwenyewe, kwa kuwa katika historia anabaki kuwa sehemu ya wakosoaji wakubwa wa serikali wanaohofiwa kusumbua watawala.
"Kwa maana hiyo, ninarudia tena kuwe na meza ya mazungumzo kumaliza changamoto iliyopo, lakini pia hekima inahitajika kwake na kwa wale anaowanyooshea vidole ndani ya chama chao ili kusaidia kukivusha kuanzia wakati huu hadi wa uchaguzi," anasema Pawa.
Mchambuzi huyo anasema hakuna wakati mbaya na wa hatari kwa chama cha siasa kama wa uchaguzi, uwe wa ndani au nje ya chama kupata viongozi au makada wake wa kukipambania na kuvikabili vyama vingine.
"CHADEMA msikumbwe na tatizo hilo, kwani vyama vingi katika historia ya dunia vimepotea katika vipindi vya uchaguzi, yaani wakati wa kuteua wagombea kuchuana na wa vyama vingine katika nafasi ya urais, ubunge na udiwani au katika uchaguzi wa ndani," anasema mchambuzi.
Pawa anafafanua kuwa mgongano wa maslahi baina ya wanaharakati, kukosekana kwa fursa za kufikia malengo na kunyimwa fursa za kukua kisiasa huwaondoa wanasiasa katika vyama vyao.
"Watu wenye ushawishi mkubwa wakiondoka, hubomoa chama kwani huondoa wafuasi wa chama wanaoamini katika siasa zao na hivyo kuzorotesha chama. La muhimu CHADEMA Mungu awanusuru," anasema.
Pawa anaamini kuwa ushauri wake ukifanyiwa kazi, chama hicho kinaweza kuvuka salama katika mnyukano huo unaoendelea ambao umewagawa wanachama makundi mawili.
"Vyama vingine vinaweza kutumia mnyukano huo kupenyeza sumu ya kukisambaratisha kwa kuchochea mgogoro ambao hautafikia mwisho na kujikuta CHADEMA inakosa nguvu zama hizi za kuelekea kwenye uchaguzi mkuu," anasema.
Anasema migogoro ndani ya vyama ni sumu ya maendeleo ya vyama vyenyewe na kwamba chama hicho kisuruhusu kuwapo kwa hali kama hiyo itakayokinyong'onyeza na kukidhoofisha.
NGUVU MBOWE, LISSU
Mchambuzi huyo anasema Mbowe na Lissu ndio wanasiasa wenye ushawishi zaidi katika chama hicho kwa sasa, tena ni viongozi wa juu zaidi wenye wafuasi wengi ndani na nje ya CHADEMA.
Anasema ushawishi wao unawafanya wote kuwa watu muhimu, na kwamba wanahitajika ndani ya chama, huku Lissu, akiendesha kampeni ngumu kwa ustahimilivu wa chama.
"Lakini wengi hasa wa mashabiki na wafuasi hawawezi kuliona hili kutokana na umahiri wa Lissu katika kujenga hoja hasa za kukosoa, alianza kwa kukosoa chama chake, akiwa mmoja wa viongozi wa juu zaidi chamani, amekuwa akiibuka hadharani kulalamika juu ya kutokuridhishwa na miendendo ya ndani ya chama," anasema.
Anaongeza kuwa hali inakuwa ngumu zaidi pale Lissu anaposimama hadharani kuhoji na kukosoa usimamizi wa fedha za chama, na kwamba amekwenda mbali na kudai kuwa viongozi wenzake wanahongwa pesa huku akiwataja kwa majina baadhi yao.
"Kukataa hadharani kwa maridhiano ya chama hicho na serikali, kuwashutumu wenzake kwa majina kuwa wamehongwa na watu wa serikali, kuibua tuhuma za matumizi mabaya ya fedha za chama ni mambo yanayofanya Lissu asiposhinda uenyekiti na wale anaowatuhumu wakashinda itakuwa ngumu kwake kudumu chamani," anasema.
Anaongeza kuwa uamuzi huo inawataka wanachama kuwa na hekima zaidi, kwa kuwa wanaweza kujikuta wanamuona kama mpinzani ndani yao anayeivua nguo taasisi na wakaamua kumshughulikia kama muasi wa chama.
Anaonya kuwa hali hiyo inaweza kuzorotesha demokrasia yao na kuonyesha kuwa anashughulikia kwa kushindana na Mbowe.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED