KLABU ya Simba imesema Jumapili ijayo inataka kurudia ilichokifanya mwaka 1993, ilipofanikiwa kufuzu fainali ya Kombe la CAF, ambalo sasa linaitwa Kombe la Shirikisho barani Afrika, ikiwa nchini Angola, dhidi ya Atletico Spotivo Aviacao.
Meneja Habari na Mawasiliano wa Klabu ya Simba, Ahmed Ally, amesema haitokuwa mara ya kwanza kushinda au kufuzu ikiwa nchini humo, kwani ilishawahi kushinda mwaka 2022 ikicheza na Primeiro de Agosto mechi ya Ligi ya Mabingwa Afrika, na ilifuzu mwaka 1993 ilipocheza dhidi ya Atletico Spotivo Aviacao.
"Safari hii tunataka kuingia robo fainali tukiwa ugenini, tunafahamu ugumu wa Bravo do Maquis hasa akiwa nyumbani kwake, lakini tumejipanga vizuri kwenda kupata matokeo Angola na hii haitakiwa mara ya kwanza kushinda au kufuzu, tumeshaenda kucheza pale na Primeiro de Agosto ambao ni wakubwa kuliko Bravo, na tumeshawahi kufuzu hapo hapo Angola dhidi ya Atletico Spotivo Aviacao mwaka 1993 kwenye Kombe la CAF," alisema Ahmed.
Historia inaonesha kuwa Simba ilifuzu hatua ya fainali ya Kombe la CAF ikiwa nchini Angola mwaka 1993, ilipolazimisha suluhu dhidi ya Atletico Spotivo Aviacao, ambapo ulikuwa ni mchezo wa marudiano baada ya ule wa kwanza kushinda mabao 3-1 kwenye Uwanja wa Taifa (sasa Uhuru), jijini Dar es Salaam.
Pia Simba ilishinda mchezo wake nchini Angola kwa mabao 3-1 dhidi ya Primeiro de Agosto, Oktoba 9, 2022, ikiwa ni raundi ya kwanza ya Ligi ya Mabingwa, na katika mchezo ya marudiano uliochezwa nchini, Oktoba 16, 2022, Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es Salaam, ilishinda bao 1-0, na kufanikiwa kutinga hatua ya makundi.
"Kama si kesho Jumatano, basi Alhamisi tutaondoka kuelekea kwenye mchezo wetu muhimu, michezo hii miwili iliyobakia inachezwa kwa hesabu kubwa sana, mchezo ujao ni kwa ajili ya kutinga robo fainali na wa mwisho dhidi ya CS Constantine ya Algeria ni maalum kwa kutaka kuongoza kundi," alisema.
Kocha Mkuu, Fadlu Davids, alisema ushindi walioupata Jumapili nchini Tunisia haukuwa rahisi kwani walicheza na moja ya timu kubwa barani Afrika, lakini pia uwanja haukuwa mzuri.
"CS Sfaxien ni moja kati ya timu kubwa barani Afrika, ina uzoefu, kwa hiyo haukuwa ushindi uliopatikana kirahisi, uwanja pia haukuwa mzuri sana, lakini kikubwa ni matokeo.
"Kwa sasa tunahitaji sare ili tufuzu, ingawa hatutacheza ili kusaka sare, bali ushindi na mechi ya mwisho tutataka tushinde ili tuongoze kundi, lakini haraka iwezekanavyo tunataka kufuzu kwenda robo, tutafanya kila linalowezekana lengo litimie," alisema Fadlu.
Simba ilirejea usiku wa kumkia jana ikitokea nchini Tunisia ambako iliifunga CS Sfaxien bao 1-0 lililowekwa ndani ya nyavu na Jean Ahoua na kuifanya kufikisha pointi tisa, ikiwa nafasi ya pili ya msimamo wa Kundi A.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED