Muhtasari Dira 2050 (1)

By Mwandishi Wetu , Nipashe
Published at 08:36 AM Jan 08 2025
Bwawa la kuzalisha umeme la Mwalimu Nyerere Rufiji.
Picha:Mtandao
Bwawa la kuzalisha umeme la Mwalimu Nyerere Rufiji.

RASIMU ya Dira ya Maendeleo ya Taifa ya 2050 inayoandaliwa na Ofisi ya Rais Tume ya Mipango, imefikia hatua ya kuhakikiwa kuanzia mwishoni mwa mwaka jana.

Dira hiyo imeainisha baadhi ya mambo muhimu yaliyoko ndani ya andiko hilo ambalo  ni malengo Tanzania inayojiwekea ili kuyatimiza ifikapo 2050 na kupata maendeleo. 

Nipashe inakuletea mambo muhimu yaliyoainishwa ili kujua kile taifa linachotarajia kufanya katika miaka 25 ijayo, lakini kwanza kwa kurejea dira inayomaliza muda wake.  

DIRA INAYOMALIZIKA 

Katika kipindi cha miaka 25 iliyopita, Tanzania imetekeleza dira ya maendeleo ya taifa 2025, ambayo ililenga kuinua uchumi wa nchi hadi hadhi ya kipato cha kati.

Dira hiyo ilijikita katika kuleta mageuzi kupitia kilimo cha kisasa, viwanda, ujenzi wa miundombinu na maendeleo ya kiteknolojia. 

Hadi mwaka 2020 taifa lilifikia hadhi ya nchi ya kipato cha kati ngazi ya chini, ikiwa na wastani wa mapato kwa kila mtu kufikia Dola za Marekani 1080 ambalo ni ongezeko la dola 180 tangu mwaka 2000.

Viwango vya hali ya maisha viliimarika kwa kiasi kikubwa huku kiwango cha umaskini kikishuka kwa asilimia 36 mwaka 2000 hadi asilimia 26 mwaka 2022. Sekta za afya na elimu ziliimarika zaidi, udumavu wa watoto chini ya miaka mitano ulipungua kutoka asilimia 48  mwaka 2005 hadi  asilimia 30 mwaka 2022.

Kwa upande wa vifo vya wazazi vilishuka kutoka 675 kwa kila vizazi hai 100,000 mwaka  2005 hadi kufikia 104 mwaka 2022.

Aidha, vifo vya watoto chini ya miaka mitano vilipungua kutoka 112 mwaka 2005 hadi 43 mwaka 2022 katika kila vizazi hai 1,000. Huku uandikishaji wa wanafunzi shule za msingi ukifikia asilimia 100 mwaka 2020 kukiwa na idadi kubwa ya wanafunzi wanaojiunga na sekondari.

Kwa muhtasari ndiyo mafanikio ya Dira ya 2025, lakini pamoja na juhudi hizo, jitihada zaidi zinahitajika kutokomeza maskini na kujenga uchumi imara na jumuishi, kuelekea mwaka 2050.

Tanzania inadhamiria kufanya mageuzi makubwa ya kimaendeleo ya kijamii na kiuchumi ambayo yatalingana au kuzidi ya nchi za kipato cha kati ngazi ya juu.

 Hata hivyo, kufikia malengo ya Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 jitihada zaidi zinahitajika ili kukabiliana na mabadiliko makubwa yatakayotokeza ikiwamo ongezeko la idadi ya watu ambalo linatarajiwa kuongezeka mara dufu hadi kufikia 140, zaidi ya nusu wakiwa wanaishi mijini.

Ongezeko la watu linaathiri kwa kiasi kikubwa upatikanaji na usalama wa chakula, makazi, ajira, elimu na huduma za afya, uwekezaji wa kimkakati katika sekta muhimu kama vile kilimo, madini, utalii, viwanda na tekinolojia utakuwa muhimu ili kukuza uchumi kwa zaidi ya mara nne ili kukidhi mahitaji ya kijamii ya wakati huo. 

Wakati huo huo, Tanzania italazimika kukabiliana na mabadiliko kadhaa yanayojitokeza duniani, ikiwamo ongezeko la tofauti za kiuchumi, mabadiliko ya tabianchi, ukuaji wa miji, tekinolojia zinazoibuka na mivutano ya kisiasa. Hata  hivyo fursa za kimaendeleo zinaendelea kujitokeza kama vile za kiteknolojia, mabadiliko kuelekea nishati safi na usawa wa kijinsia unaongezeka. 

Kwa kutumia idadi kubwa ya vijana wake, rasilimali asilia, nafasi yake kijiografia  hasa kuwa na  bahari na miundombinu ya usafirishaji , Tanzania inaweza kuendeleza ustawi wake huku ikichangia malengo ya maendeleo endelevu duniani.

Dira 2050 inaweka maono makubwa  kwa mustakabali wa taifa na mikakati ili kufikia maendeleo.

Inajengwa juu ya mafanikio na uzoefu wa utekelezaji wa dira 2025 na kuzingatia mabadiliko  mbalimbali  duniani. Dira 2050 inalenga kuifanya nchi kuwa yenye nguvu kiuchumi  brani Afrika na duniani  kwa ujumla.

Italiongoza  taifa kuwa nchi yenye nguvu kiuchumi barani Afrika na duaniani pia. Italiongoza taifa kuwa na mustakabali endelevu, unaozingatia usawa wa kijinsia hususan wa wanawake, vijana, na wenye ulemavu  na ustawi wa watu wake. 

 MUHTASARI DIRA 2050 

Dira ya Maendeleo ya Taifa 2025 inafikia ukomo na kufungua ukurasa mpya wa kuanza kutumika kwa nyingine itakayoifikisha Tanzania mwaka 2050. Andiko lake sasa limefikia kwenye hatua za rasimu kuhakikiwa na wadau mbalimbali.

 TAMKO

Inatamka kuwa inakusudia kuifanya Tanzania kuwa  taifa jumuishi lenye ustawi, haki na linalojitegemea, ikiweka mkazo katika maendeleo ya watu (kuwa na maisha bora kwa kila Mtanzania), kukomesha umaskini wa aina zote na kujenga taifa lenye uchumi imara. Halikadhalika dira inalenga kuwa na uchumi jumuishi, ulioshindani na utakaoboresha maisha ya watu mijini na vijijini. 

 MISINGI YA DIRA

 Mosi ni kila Mtanzania awe na jukumu la kudumisha Muungano wa Tanzania na Zanzibar, umoja na mshikamano wa taifa, msingi mwingine ni utu, kila mtu anastahili kuheshimiwa na kuthaminiwa pamoja na kulindwa utu wake.

Msingi wa tatu wa dira hii ni uhuru na haki, kwamba kila raia ana haki ya kufurahia haki zote na uhuru wa kulindwa kwa mujibu wa katiba.

Demokrasia ni msingi mwingine unaosisitizwa, ukieleza kuwa  kila mtu, jamii na taifa kuwa na jukumu la kuheshimu, kulinda na kudumisha demokrasia, utawala bora unaofuata sheria na unaoheshimu na kuzingatia katiba. 

 Ulinzi wa maliasili na rasilimali unatajwa kuwa msingi  muhimu wa dira hii unaosisitiza kulinda na matumizi endelevu ya rasilimali za Tanzania kwa ajili ya maendeleo ya watu wake.

 "Hivyo, malialisi na rasilimali za taifa zitalindwa, kusimamiwa na kutumiwa vyema kwa maendeleo endelevu na ustawi wa nchi na kwa manufaa ya kizazi cha sasa na vizazi vijavyo," rasimu ya dira inaeleza.

  Ulinzi na utamaduni wa maadili ya taifa ambao ni urithi wa tamaduni wa Watanzania, vitahifadhiwa, kukuzwa na kulindwa ili kujenga utambulisho wa kitaifa na umoja kwa vizazi vya sasa na vijavyo.

 MALENGO YA DIRA 

 Dira inalenga kuwa ifikapo 2050 taifa lifikie kuwa nchi ya kipato cha kati ngazi ya juu yenye uchumi, mseto stahimilivu, imara na jumuishi. Aidha, kutokomeza aina zote za umaskini hususan kwa wanawake, vijana na wenye ulemavu na kuimarisha maendeleo yanayolingana kwa kila mkoa. Kuwa na ubora wa hali ya juu wa maisha na ustawi kwa wote. 

Kujenga kikamilifu uwezo wa rasilimali watu hususan wanawake, vijana na watu wenye ulemavu ili kuchochea maendeleo ya taifa na kushiriki kama raia wa kimataifa wenye ubunifu, fikra tunduizi na kujiamini.

Lengo lingine la dira hiyo ni kuwa na mfumo wa utawala ulio jumuishi, wenye uwazi na uhaohakikisha amani ya kudumu, uhuru na usalama wa watu. Aidha, dira pia inalenga kuwa na mfumo imara na endelevu wa usimamizi thabiti na endelevu wa ikolojia na rasilimali ili kujenga ustahimilivu kwa mabadiliko ya tabianchi.

ITAENDELEA WIKI IJAYO