FUKUTO la uchaguzi ndani ya CHADEMA kuwapata mwenyekiti taifa limepamba moto na hata kuibua makundi yanayosigana kuwaunga mkono au kuwapinga wagombea wa nafasi hiyo.
Vigogo hao Tundu Lissu na Freeman Mbowe, wanaitaka nafasi ya uenyekiti wakati wanaogombea nafasi ya makamu ni John Heche na Ezekiel Wenje.
Makundi yanayoonyesha msimamo ni la kumuunga mkono Lissu na jingine la Mbowe, yote yakikwaruzana kwenye majukwaa mitaani na kwenye mitandao ya kijamii. Wakijiita au ‘team Lissu’ ama ‘team Mbowe’
Hata hivyo, pamoja na kuwapo makundi hakuna upande unaorusha kejeli, matusi na kashfa dhidi ya mwingine, zaidi ya kujenga hoja za kuvuta wapiga kura.
Katika moja ya hotuba zake, Lissu ambaye awali anaonyesha kusudio la kutetea nafasi yake ya makamu, kabla ya kubatilisha uamuzi wa kuvaana Mbowe kuwa Mwenyekiti Taifa, anasema:
“Nimejitafakari nimeona kwa sasa ni wakati sahihi wa kuwania nafasi hiyo.”
Hata hivyo Lissu aliwahi kusema anania ya kuwania nafasi ya urais kwa awamu nyingine, japo vyanzo vya ndani ya chama hicho vinasema hajakubaliwa.
Hata hivyo, kushindikana kwa mpango huo, kunahusishwa na mpango wa Lissu kuutaka uenyekiti ili aweze kuwa na nafasi ya kuamua kutekeleza hilo.
Katika hotuba zake hivi karibuni Lissu amekuwa akisema mara nyingi iwapo uchaguzi huo hautofanyika kwa haki atakuwa na uamuzi mwingine ambao hakuuweka hadharani.
Udadisi wa gazeti hili kutoka kwa vyanzo ndani ya chama hicho, vinasema iwapo uchaguzi huo utakuwa na makandokando na Lissu akaanguka kwa viashiria visivyo vya haki huenda akajiunga na ACT Wazalendo.
Kutimia kwa hilo, pengine kutampa tena nafasi ya kuwania nafasi ya urais akiwa katika chama hicho kutokana na ukubwa wake na ushawishi wa kisiasa alio nao.
Lissu anaamini kama uchaguzi utafanyika kwa haki atashinda na kuendeleza mazuri yaliyofanywa na Mbowe kwa kipindi chote alichokaa madarakani.
“Kwasababu hiyo wana CHADEMA au mtu mwingine yeyote anayeona ajabu, au anayechukizwa au kukwazwa na uamuzi wangu wakutangaza nia ya kugombea uongozi ndani ya chama chetu atakuwa au amesahau, ama hajui na pengine hataki kuenzi na kue ndeleza urithi tulioachiwa wazee wetu Edwin Mtei na Bob Makani wakuachiana madaraka ya uongozi ndani ya chama kupitia uchaguzi huru na haki.”
Anaongeza: “Mtu wa aina hiyo anatakiwa kuelimishwa au kukumbushwa urithi wetu huu na kwa vyovyote vile asiruhusiwe kutuletea utamadani tofauti katika kubadilishana madaraka na uongozi katika chama chetu.” Anasema Lissu anapotangaza kuwania uenyekiti.
Kubadili kwake msimamo wa kuwa makamu mwenyekiti tangu alipoanza kushawishiwa kugombea nafasi hiyo mwaka 2015 kunatokana na mazingira ya siasa ya sasa ambayo yanahitaji kiongozi mwenye historia ya uadilifu na kukubalika na jamii, anaongeza.
“Ndugu zangu na wanachama tupo katika mazingira mapya katika siasa za nchi yetu…Hatua hii ya sasa inahitaji kiongozi mwenye historia ya uadilifu na kukubalika na jamii. Ninapenda kuamaini kwamba historia ya kukubalika kwangu kwa Watanzania inajulikana na wengi,” anasema.
Aidha, anasema hatua hiyo ya mapambano ya kidemokrasia inahitaji kiongozi aliyeonesha kwa maneno ya katiba kwa tabia na mwenendo wa uzalendo wa kupenda na kutetea nchi.
Kutokana na chama hicho kukua kwasasa hakuna budi kurudisha tena, utaratibu wa kikatiba wa ukomo wa madaraka katika chama hicho uliokuwapo mwanzo.
MSIMAMO WA MBOWE
Pamoja na kukiongoza chama kwa miongo miwili anasema ametafakari kwa kina jambo hilo na kuamua kutetea nafasi yake, kutokana na maoni kutoka kwa wadau tofauti.
“Nimetafakari kwa kina nimesema mara nyingi nilitamani kuondoka lakini siwezi kuondoka na minyukano ambayo ipo ndani ya chama kwa hiyo CHADEMA nipo, nitakuwapo, nitagombea na mimi na viongozi wenzangu wanaoniunga mkono na wasioniunga mkono naamini tutakutana kwenye mazungumzo tuweke mambo sawa, sijawahi kuzuia watu kugombea, anayetaka tukutane kwenye boksi.”
Anasema wazee waasisi hawakuondoka madarakani kwa kuwa walitaka kung’atuka, waliamua kuondoka kwasababu walikuwa wametimiza wajibu wao mkubwa wa kujenga chama imara chenye itikadi na sera madhubuti.
Anakumbusha kuwa Edwin Mtei Mwenyekiti wa kwanza CHADEMA aliondoka akiwa na miaka 68, miaka mitano baadaye Bob Makani Mwenyekiti wa pili, aliondoka akiwa na miaka 67 wote waliondoka si kwasababu ya kushindwa bali baada ya kukamilisha kazi za kuimarisha sera.
“Nilipokea kijiti cha kuongoza Septemba 14, 2004, katika miaka hiyo 20 ni kipindi cha miaka 11 tu ya kwanza ambapo tulifanya kazi kikamilifu ya kujitoa ili kukijenga chama chetu kiwe makini na tukapata mafanikio ya kufanya tuwe chama kikuu cha upinzani Tanzania.
“Tumefanya mambo mengi ikiwamo kubuni vazi maarufu la chama ndiyo kombati na kuongeza thamani ya chama chetu kwa kuvuta wanasiasa makini kutoka vyama vyote na vyuoni hadi tukafananishwa na klabu ya Real Madrid inayovuta wacheza nyota ‘mastaa’ mbalimbali, tukapata wengi waliokuja kuongeza thamani ya CHADEMA,” anakumbusha.
VITA UMAKAMU
Haijaishia tu kwa wagombea nafasi ya uenyekiti sasa mtifuano upo katika nafasi ya makamu inayowaniwa na Mwenyekiti wa CHADEMA kanda ya Victoria, Ezekiah Wenje na aliyekuwa Mbunge wa Tarime, John Heche.
Hotuba za Wenje zinaonyesha anamuunga mkono Mbowe, anayataja matatizo ambayo atashughulika nayo kuwa ni pamoja na ubovu wa miundombinu, ukosefu wa ajira na kuinua sekta muhimu kwa ajili ya kukuza uchumi wa nchi.
Wenje anaiomba serikali kuweka mifumo rafiki ya elimu bunifu kwa wanafunzi ili kukabiliana na changamoto za maisha na kuanzisha mitaala ya kujifunza kwa vitendo.
Aidha, anakumbushia kuweka soko la pamoja katika mikoa ya Kanda ya Ziwa kwa ajili ya kusaidia kukuza mzunguko wa biashara na kuondoa usumbufu kwa wafanyabiashara kuendelea kutegemea soko la Kariakoo lililopo Dar es Salaam.
Heche anayemuunga mkono Lissu, anasema ana mrengo wa kutaka haki, ukweli na uwazi ndani ya chama hicho kikuu cha upinzani.
Anasema ‘Kambi ya Lissu’ wana uhakika wa kuchukua kiti na kuongoza chama hicho na kuwa hawako tayari kuona kinaongozwa na malengo ya watu binafsi kinyume cha madhumuni ya kuanzishwa kwake.
“Chama hiki kimeanzishwa kwa madhumuni maalumu ikiwa ni pamoja na kushinda dola na kuiondoa CCM, kulinda na kutumia rasilimali za nchi kwa manufaa ya Watanzania, kuwapatia huduma bora ikiwa ni pamoja na matibabu, elimu na umiliki wa rasilimali binafsi,” Heche anasema.
Anaeleza kuwa watu wengi wamefariki dunia kwa namna tofauti katika kuhakikisha wanapigania maslahi ya chama hicho, hivyo hawako tayari kuona kinaongozwa kwa malengo binafsi.
UCHAGUZI MKUU
Kuhusu chama hicho kushiriki uchaguzi mkuu mwaka huu, Heche anasema wakipata nafasi hiyo hawatakubali kushiriki bila kuwa na mabadiliko ya Tume Huru ya Uchaguzi (INEC).
“Tutapeleka nguvu ya umma na tuna imani watasimama nasi kama walivyofanya katika mabadiliko mbalimbali kuhakikisha tunashinikiza serikali kufanya mabadiliko INEC kabla ya uchaguzi mkuu na tutasimama katika msimamo wetu kuwa ‘no reform no election’ ikimaanisha kama hakuna mabadiliko hakuna uchaguzi,” anasema Heche.
KUKICHAFUA CHAMA
Kuhusu madai kwamba Lissu anachafua chama, Heche anaunga mkono kampeni za Lissu kuwasema na kuibua kashfa za baadhi ya watu wanaodaiwa kupokea rushwa ndani ya chama hicho.
“Kuna watu wanachafua viongozi wengine, wanamwita Lissu muongo, si kweli. Lissu ni mkweli na mtu safi. Anachokifanya ni kuwavua nguo wanaovua nguo chama na wala si chama chenyewe. Wananchi wakikwambia wanataka mchicha ukawaletea vitu vingine kwa madai zote ni mboga za majani, hawatakuelewa,” anasema Heche.
Anasisitiza kuwa anamheshimu mwenyekiti wa sasa, Freeman Mbowe kama baba yake na mlezi wa kisiasa na kuwa haitatokea kumkosea heshima.
Anasema anao mchango katika demokrasia ya taifa na chama chao lakini kwa sasa Lissu ni kimbunga, Tsunami akimaanisha ni wakati wa Mbowe kukaa pembeni.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED